Papa Leo XIV: Toba na Wongofu wa Ndani: Ufalme wa Mungu Umekaribia
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Majilio ni kipindi cha kumbukumbu na matumaini kwa Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake, ili kuweza kuinua utu na heshima yao, iliyokuwa imechakaa kutokana na dhambi, ili hatimaye, kuwakomboa kutoka katika dhambi na mauti. Hii ni hija ya maisha ya imani, matumaini na mapendo; inayowakumbusha waamini, Fumbo la Umwilisho na Siku ile ya mwisho, Kristo Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu; kama Kanisa linavyokiri na kufundisha kwenye Kanuni ya Imani. Kwa njia ya Kipindi cha Majilio, Mama Kanisa huwafungulia waamini utajiri wa uweza na mastahili ya Bwana wake Kristo Yesu na hivyo waamini huweza kuchota na kujazwa na neema ya wokovu. Mama Kanisa katika huruma na upendo wake wa daima anapenda kuwakomaza waamini kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili; Mafundisho, Sala pamoja na Matendo ya toba na huruma. Rej. Sacrosanctum concilium, 102-111. Kipindi cha Majilio: “Kwa kuadhimisha kila mwaka Liturujia ya Majilio, Kanisa linapyaisha kule kumngojea Masiha, likijiweka katika ushirika wa maandalizi marefu ya ujio wa kwanza wa mwokozi, waamini wakipyaisha tamaa ya ujio wake wa pili.” (KKK 524). Majilio ni kipindi cha upendo, matumaini, furaha na amani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Mishumaa minne inawakilisha Majuma manne ya Kipindi cha Majilio. Kwa kadiri ya Mapokeo ni kwamba, kila juma linawakilisha miaka elfu moja, kumbe, majuma manne ni sawa na miaka 4,000 kutoka kwa wazazi wetu wa kwanza Adamu na Eva hadi Kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu.
Mishumaa mitatu ni ya rangi ya zambarau na mmoja ni wa rangi ya waridi. Mishumaa ya zambarau huwakumbusha waamini kuwa kipindi cha majilio ni kipindi cha sala, toba, na matendo ya huruma: kiroho na kimwili ili kujitayarisha vema kumpokea Kristo Yesu anayezaliwa katika hali zote mbili: Ujio wa kwanza na wa pili. Mshumaa wa rangi ya waridi huwashwa Dominika ya tatu, Dominika ya furaha “Gaudete” kwa sababu waamini wamefika katikati ya Kipindi cha Majilio, utimilifu wa ahadi ya kuzaliwa Mwokozi ukaribu zaidi. Mwanga wa mishumaa unaashiria matarajio na tumaini linalozunguka ujio wa kwanza wa Bwana wetu ulimwenguni na matarajio ya ujio wake wa pili atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu. Dominika ya Pili ya Kipindi cha Majilio, Mwaka A wa Kanisa, waamini wanatangaziwa ujio wa Ufalme wa Mungu, ujumbe unaotangazwa na Yohane Mbatizaji, Mtangulizi wa Kristo Yesu, aliyekuwa anaishi jangwani. Mwaliko ni toba na wongofu wa ndani kwani Ufalme wa mbingu umekaribia. Rej Mt 3:1. Hii ni sehemu ya tafakari ya Dominika ya Pili ya Kipindi cha Majilio iliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 7 Desemba 2025. Itakumbukwa kwamba, katika Sala kuu ya Baba Yesu, waamini wanasali kama walivyofundishwa na Kristo Yesu wakiomba ujio wa Ufalme wa Mungu. Ni Mwenyezi Mungu anayeiandika historia na maisha ya binadamu, changamoto na mwaliko ya kujikita kwa mawazo na kwa kutumia nguvu kwa ajili ya huduma kwa Mwenyezi Mungu anayekuja kuhudumia na wala si kutawala, bali kuwakomboa wanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Hii ndiyo Habari Njema ya Wokovu inayowachangamotisha pamoja na kuwashirikisha waamini.
Yohane Mbatizaji alikuwa kweli ni mjumbe wa Habari Njema ya Wokovu na watu walimsikiliza kwa makini. Alitangaza ujumbe huu kwa mtindo wake wa maisha, akawataka watu watakatifu wa Mungu watubu na kumwongokea Mungu, Hakimu mwenye haki anayehukumu mintarafu matendo adili, nia njema ya moyo na wala si kwa kadiri ayaonayo kwa macho yake wala hayasikiayo kwa masikio yake. Yohane Mbatizaji alishangazwa sana na ufunuo wa Ufalme wa Mungu kwa njia ya Kristo Yesu uliosimikwa katika unyenyekevu na huruma, mfano wa shina la Yese, litakalovikwa mapaji ya Roho Mtakatifu. Kila mwamini anaweza kufikiri kuhusu mshangao alioupata katika maisha yake.Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, tajiriba ya Kanisa katika maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, uliohitimishwa miaka 70 iliyopita, imekuwa ni Pentekoste mpya kwa Kanisa Katoliki, kwa kutaka kusoma alama za nyakati, kusahihisha mapungufu yake, ili hatimaye, kuliwezesha Kanisa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kumletea mwanadamu maendeleo endelevu ya: kiroho na kimwili. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, lilikuwa ni tukio la matumaini ndani ya Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, wakatambua dhamana, wajibu na changamoto iliyokuwa mbele yao, wakaamua kujadili vipengele mbalimbali na hatimaye, kuvipigia kura. Ni Mtaguso uliowakusanya viongozi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kujadili maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, chini ya uongozi na usimamizi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, wakati huo akiwa ni Mtakatifu Yohane XXIII; Ukatafsiriwa kwa vitendo na Mtakatifu Paulo VI pamoja na Mtakatifu Yohane Paulo II.
Baba Mtakatifu Benedikto XVI akapyaisha mafundisho yake kwa Katekesi makini kuhusu: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Sala. Baba Mtakatifu Francisko akaendelea kujipambanua kwa kutaka ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu ili kuchangia katika maisha na utume wa Kanisa la Kristo Yesu kila mmoja kadiri ya karama, wito na dhamana yake ndani ya Kanisa: Moja, takatifu, katoliki na la mitume. Hili ni Kanisa linalotumwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili inayomwilishwa katika imani tendaji. Kanisa katika upendo, unyenyekevu na sadaka, linakabidhiwa utume wa kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Kristo na wa Mungu; kutangaza Habari Njema ya Wokovu sanjari na utamadunisho, ili kushiriki: furaha na matumaini; uchungu na fadhaa ya walimwengu. Kumbe, Maadhimisho ya kumbukizi ya Miaka 70 tangu kuzinduliwa kwa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican (1962 hadi 1965) imekuwa ni fursa ya ushiriki mkamilifu wa Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo kwa Mama Kanisa kujikita zaidi katika Nyaraka Kuu 4 za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yaani: “Dei verbum” yaani “Ufunuo wa Kimungu”, “Sacrosanctum concilium” yaani “Juu ya Liturujia”; “Lumen gentium” yaani “Fumbo la Kanisa” pamoja na “Gaudium et spes” yaani “Kanisa katika ulimwengu mamboleo.” Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kuupokea Ufalme wa Mungu na kuanza kujikita katika huduma kwa kwenda mbali zaidi, ili kutenda hata yale ambayo kwa macho ya binadamu hayawezekani kabisa, yaani Paradisi mpya: “Mbwamwitu ataishi pamoja na mwana-kondoo, naye chui atalala pamoja na mbuzi, ndama, mwana simba na ngʼombe wa mwaka mmoja watakaa pamoja, naye mtoto mdogo atawaongoza.” Isa 11:6.
Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, Ulimwengu unatamani kupata matumaini haya, kwani hakuna kitu kisichowezekana mbele ya Mungu, changamoto na mwaliko kwa waamini kujiandaa kwa ajili ya ujio wa Ufalme wa Mungu, utakaoongozwa na Mtoto Yesu, aliyewekwa mikononi mwa binadamu, tangu kuzaliwa kwake, akateswa na kufa Msalabani, lakini leo hii anang’ara kama Jua linalochomoza asubuhi, mwanzo wa siku mpya, watu wa Mungu wanapaswa kuamka na kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Yesu na kwamba, kila mwamini anaweza kuwa ni mwanga mdogo ikiwa kama atampokea Kristo Yesu katika maisha yake, mwanzo wa mapambazuko ya siku mpya. Waamini wajifunze kutenda hivi kama alivyofanya Bikira Maria, Mama wa Kanisa, Mwanamke wa imani na matumaini thabiti.