Tafuta

Papa Leo XIV: Ushuhuda wa Yohane Mbatizaji: Mwanakondoo, Nuru ya Mataifa!

Kristo Yesu ndiye mwanakondoo anayekuja duniani kuondoa dhambi za ulimwengu kwa maana ya kuanzisha ufalme wa Mungu unaosimikwa katika kweli na uzima; ni ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Yohane Mbatizaji anamtambulisha Kristo Yesu kuwa ni Nuru ya Mataifa, Mwana wa Mungu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ushuhuda wake ni himizo kwamba, watu wote wanapendwa na kuthaminiwa na Mungu aliye juu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika Injili ya Dominika ya Pili ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa, Yohane Mbatizaji anamtambulisha Yesu kama Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za duniani. Yohane Mbatizaji sasa amemaliza kazi yake na sasa ni Yesu ndiye anayetembea na kutimiza utume wake. Kristo Yesu anapaswa kuongezeka na yeye Yohane Mbatizaji kupungua. Rej. Yn. 3:29-30. Yohane Mbatizaji alijua vema Maandiko Matakatifu na ndio maana anamtambulisha Kristo Yesu kama Mwanakondoo wa Mungu akirejea kama Mwanakondoo wa Pasaka ambaye damu yake ilipakwa katika miimo ya milango na hivi kuwaokoa Waisraeli. Na ndio Damu Azizi Kristo Yesu itamwagika kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Yn 19:14. Pia Yohane Mbatizaji anamtambulisha Kristo Yesu kama mwanakondoo akirejea unabii wa Isaya juu ya Mtumishi wa Mungu anayeteseka, atakaye pelekwa machinjioni kama mwanakondoo. Rej. Isa 53:7,12.

Kanisa la Ubatizo wa Bwana
Kanisa la Ubatizo wa Bwana

Kristo Yesu ndiye mwanakondoo anayekuja duniani kuondoa dhambi za ulimwengu kwa maana ya kuanzisha ufalme wa Mungu unaosimikwa katika kweli na uzima; ni ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani.  Yohane Mbatizaji anamtambulisha Kristo Yesu kuwa ni Nuru ya Mataifa, Mwana wa Mungu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ni Mkombozi wa ulimwengu, anayebeba dhambi za walimwengu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko uletao maisha na uzima wa milele. Pia Yohane Mbatizaji anarejea mwanakondoo yule ambaye Abrahamu alimtolea Mungu sadaka. Wakati wakiwa njiani mwanaye Isaka akamuuliza Abrahamu baba yake, “Baba, moto na kuni tunazo; lakini mwanakondoo wa sadaka ya kuteketezwa yuko wapi?” Mwa 22:7.

Ushuhuda wa Yohane Mbatizaji una mguso, mvuto na mashiko
Ushuhuda wa Yohane Mbatizaji una mguso, mvuto na mashiko   (@Vatican Media)

Yohane Mbatizaji anakiri kabisa akisema kwamba: “Wala mimi sikumjua; lakini yeye aliyenipeleka kubatiza kwa maji, huyo aliniambia, Yeye ambaye utamwona Roho akishuka na kukaa juu yake, huyo ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu.” Yn 1:33. Yohane Mbatizaji ni kiongozi aliyependwa sana na watu kutoka na mtindo wa maisha yake, angeweza kutumia fursa hii kujimwambafai, lakini mbele ya Kristo Yesu, akaonesha udogo wake, akitambua kwamba, ametumwa na Mungu kumwandalia njia na Kristo Yesu anapokuja kwa furaha na unyenyekevu, anamtambua na kumtambulisha kwa wanafunzi wake, ili Kristo Yesu aongezeke na yeye Yohane Mbatizaji apungue. Ushuhuda wa Yohane Mbatizaji una nguvu na mvuto mkubwa n ani ujumbe unaopaswa kuigwa na wengi katika Ulimwengu mamboleo. Ushuhuda wake si chanzo cha mafarakano, upinzani na maigawanyiko ya kijamii, bali ushuhuda wake unakita mizizi yake kwa waamini kutambua kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa na Mwenyezi Mungu, aliye juu mbinguni.

Kristo Yesu ni Mwanakondoo wa Mungu, Nuru ya Mataifa
Kristo Yesu ni Mwanakondoo wa Mungu, Nuru ya Mataifa

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV, Dominika tarehe 18 Januari 2026 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Upendo unaotangazwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu ni upendo ule ambao Mwenyezi Mungu hata katika ulimwengu mamboleo anapenda kuuonesha kwa kuja na kukaa kati ya waja wake, ili aweze kushiriki katika: uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya Mwenyezi Mungu anayependa kuwadhihirishia wanadamu kwamba, kwa hakika wanayo thamani kubwa mbele ya macho yake. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema anasema, Baba Mtakatifu Leo XIV kukita mawazo yao na kuanza kujifunza kutoka kwa Yohane Mbatizaji, ari na moyo wa kukesha, kwa kupenda mambo ya kawaida; kwa kuwa wakweli na kuishi kwa kiasi; kwa kutafuta na kuambata mambo msingi katika maisha. Hii ni changamoto ya kutafuta muda katika hali ya ukimya, ili kusali, kutafakari na kusikiliza; kwa maneno machache huu ni mwaliko wa kujitengenezea “Jangwa la maisha” ili kuweza kukutana na kuzungumza na Kristo Yesu, ili hatimaye, waweze kushinda pamoja naye! Baba Mtakatifu Leo XIV amehitimisha tafakari yake kwa kusema kwamba, Bikira Maria ni mfano wa maisha ya kiasi, hekima na unyenyekevu.

Papa Leo XIV: Mwanakondoo

 

18 Januari 2026, 15:00

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >