Tafuta

Papa Leo XIV: Heri za Mlimani Ni Habari Njema ya Wokovu Kwa Wote

Heri za Mlimani ni Habari Njema ya Wokovu inayotangazwa kwa watu wote wa Mataifa. Ni nuru na mwanga unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, ili kuangazia sehemu za giza ya historia ya mwanadamu, kwa kufunua mpango wa Ukombozi wa mwanadamu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, uliotekelezwa kwa njia ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, na kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Huu ni muhtasari wa Injili, Dira na Mwongozo wa maisha ya Kikristo hapa duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Heri za Mlimani mintarafu Injili ya Mathayo 5: 1-12 ni: Katiba, Mwongozo, dira ya maisha na muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu na ni lengo la kila mwamini. Heri hizi ni kiini cha mahubiri ya Kristo Yesu, muhtasari wa ahadi za Mungu kwa Taifa teule kuanzia Ibrahimu, nazo zatimiliza ahadi hizo si kwa kuzipanga tena kwa ajili ya kupata nchi, bali kwa ajili ya Ufalme wa Mungu unaosimikwa: katika kweli na uzima; ni ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Heri hizi zachora uso wa Yesu Kristo na kufafanua mapendo yake, zaonesha wito wa mwamini anayeshiriki: Utukufu wa Mateso na Ufufuko wake, zinaangaza matendo na hali zilizo za maisha ya Kikristo, zinatoa ahadi za matumaini katika taabu, zikitangaza baraka na tuzo ya wokovu, yaani, maisha ya uzima wa milele mbinguni (Rej. KKK 1716-1717.) Kimsingi sifa za Heri huzijumlisha na kuzikamilisha ahadi za Mwenyezi Mungu tangu kwa Ibrahimu Baba yetu wa imani kwa kuzielekeza kwenye Ufalme wa mbinguni. Nazo zajibu hamu ya furaha ambayo Mungu ametia katika moyo wa mwanadamu. Sifa za heri zinawafundisha waamini lengo la mwisho ambalo Mwenyezi anawaitia waja wake: Ufalme, kumwona Mungu jinsi alivyo, kushiriki katika hali ya umungu, maisha na uzima wa milele; kufanya waana; pumziko katika Mungu. Heri ya uzima wa milele ni paji la Mungu tu; ni paji la kimungu kama ilivyo neema inayowaelekeza huko. Sifa za heri zinawaweka mbele ya uchaguzi mkataa kuhusu mambo ya duniani: Zatakasa nyoyo za waamini na hivyo kuwawezesha kumpenda Mwenyezi Mungu kupita vitu vyote. Heri za mbinguni huweka vigezo vya utambuzi katika kutumia mambo ya dunia kulingana sheria ya Mwenyezi Mungu. Rej. KKK 1725-1739.

Heri Maskini wa Roho Maana Ufalme wa Mbingu ni wao
Heri Maskini wa Roho Maana Ufalme wa Mbingu ni wao   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika tafakari yake, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe Mosi, Februari 2026 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amesema, kwa hakika Heri za Mlimani ni Habari Njema ya Wokovu inayotangazwa kwa watu wote wa Mataifa. Ni nuru na mwanga unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, ili kuangazia sehemu za giza ya historia ya mwanadamu, kwa kufunua mpango wa Ukombozi wa mwanadamu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, uliotekelezwa kwa njia ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, na kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Pale Mlimani, Kristo Yesu anawakabidhi Mitume na wafuasi wake Amri Mpya inayokita mizizi yake katika sakafu ya mioyo yao na wala si katika mawe. Hii ni Amri inayopyaisha maisha ya waamini na hivyo kuwafanya kuwa watu wema, hata kama ulimwengu unaonekana kana kwamba, umeshindwa na wala hautamaniki tena. Furaha ya kweli ipo katika kumtafuta Mungu na kuziishi Heri za Mlimani. Mtakatifu Augustino anasema furaha ya kweli inadumu na wala haitokani na vitu bali inatokana na ushirika wa kudumu na Mwenyezi Mungu mwenyewe. Mwenyezi Mungu ndiye wema mkuu (Summum bonum), ndiye lengo la mwisho la maisha ya binadamu (Finis ultimus). Mwenyezi Mungu ndiye mwenye haki ya kutoa heri kwa maskini wa roho na wenye kiu ya haki, kwani Mwenyezi Mungu ndiye Hakimu mwenye haki, chanzo na hatima ya amani ya kweli. Heri wenye rehema na wenye moyo safi watapata furaha, kwani Mwenye Mungu ni ukamilifu wa matamanio yote ya binadamu. Katika mateso, dhuluma na nyanyaso, Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya faraja na ukweli ndiyo maana Kristo Yesu anawaambia wafuasi wake: kufurahi na kushangilia kwa kuwa thawabu yao ni kubwa mbinguni. Rej. Mt 5:12.

Heri wenye njaa na kiu ya haki maana hao watashibishwa
Heri wenye njaa na kiu ya haki maana hao watashibishwa

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Kristo Yesu anafunua Heri za Mlimani kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, kwa wale wanao mwamini Kristo Yesu, atawakirimia furaha ya milele na kwamba, hili si wazo la kufikirika. Kristo Yesu katika anawashirikisha wote katika umaskini wake; wale wanaoudhiwa kwa ajili ya haki; Kristo Yesu ni chanzo cha amani, aliyedhulumiwa na kuteseka hata kifo cha Msalaba. Hivi ndivyo Kristo Yesu anavyoangazia maana ya historia ya mwanadamu na jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anatenda ili kuwaokoa wanaoteseka na kunyanyasika. Mwana wa Mungu anauangalia ulimwengu kwa jicho la upendo wa Baba wa milele, kwani Yeye ni chanzo cha matumaini kwa waja wake na kwamba, Mwenyezi Mungu anawakirimia matumaini haya maskini wa roho na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mwishoni mwa tafakari yake Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, ni katika muktadha huu, Heri za Mlimani kwa waamini zinakuwa kama ni jaribio la furaha ya kweli, kwa kumweka Kristo Yesu mbele, kwani Yeye ndiye anayegeuza mateso na mahangaiko ya binadamu kuwa ni chemchemi ya furaha kwa waamini, kwani anawakirimia neema na baraka wakati wa mateso na mahangaiko yao. Heri za Mlimani zinawanyannyua na kuwakweza maskini na wanyonge na kuwaangusha wakuu kutoka katika viti vyao vya enzi. Rej. Kl 1:51-52. Huu ni mwaliko kwa waamini kukimbililia tunza na maombezi ya Bikira Maria, Mtumishi mwaminifu wa Mungu, ambaye vizazi vyote wanamwita mbarikiwa!

Papa Leo XIV Heri za Mlimani
01 Februari 2026, 15:21

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >