Papa Leo XIV: Kristo Yesu Ni Utimilifu wa Torati na Unabii: Haki na Upendo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Heri za Mlimani mintarafu Injili ya Mathayo 5: 1-12 ni: Katiba, Mwongozo, dira ya maisha na muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu na ni lengo la kila mwamini. Heri hizi ni kiini cha mahubiri ya Kristo Yesu, muhtasari wa ahadi za Mungu kwa Taifa teule kuanzia Ibrahimu, nazo zatimiliza ahadi hizo si kwa kuzipanga tena kwa ajili ya kupata nchi, bali kwa ajili ya Ufalme wa Mungu unaosimikwa: katika kweli na uzima; ni ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Heri hizi zachora uso wa Yesu Kristo na kufafanua mapendo yake, zaonesha wito wa mwamini anayeshiriki: Utukufu wa Mateso na Ufufuko wake, zinaangaza matendo na hali zilizo za maisha ya Kikristo, zinatoa ahadi za matumaini katika taabu, zikitangaza baraka na tuzo ya wokovu, yaani, maisha ya uzima wa milele mbinguni (Rej. KKK 1716-1717.) Kimsingi sifa za Heri huzijumlisha na kuzikamilisha ahadi za Mwenyezi Mungu tangu kwa Ibrahimu Baba yetu wa imani kwa kuzielekeza kwenye Ufalme wa mbinguni. Nazo zajibu hamu ya furaha ambayo Mungu ametia katika moyo wa mwanadamu. Sifa za heri zinawafundisha waamini lengo la mwisho ambalo Mwenyezi anawaitia waja wake: Ufalme, kumwona Mungu jinsi alivyo, kushiriki katika hali ya umungu, maisha na uzima wa milele; kufanya waana; pumziko katika Mungu. Heri ya uzima wa milele ni paji la Mungu tu; ni paji la kimungu kama ilivyo neema inayowaelekeza huko. Sifa za heri zinawaweka mbele ya uchaguzi mkataa kuhusu mambo ya duniani: Zatakasa nyoyo za waamini na hivyo kuwawezesha kumpenda Mwenyezi Mungu kupita vitu vyote. Heri za mbinguni huweka vigezo vya utambuzi katika kutumia mambo ya dunia kulingana sheria ya Mwenyezi Mungu. Rej. KKK 1725-1739.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kwa hakika Heri za Mlimani ni Habari Njema ya Wokovu inayotangazwa kwa watu wote wa Mataifa. Ni nuru na mwanga unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, ili kuangazia sehemu za giza ya historia ya mwanadamu, kwa kufunua mpango wa Ukombozi wa mwanadamu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, uliotekelezwa kwa njia ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, na kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Pale Mlimani, Kristo Yesu aliwakabidhi Mitume na wafuasi wake Amri Mpya inayokita mizizi yake katika sakafu ya mioyo yao na wala si katika mawe. Hii ni Amri inayopyaisha maisha ya waamini na hivyo kuwafanya kuwa watu wema, hata kama ulimwengu unaonekana kana kwamba, umeshindwa na wala hautamaniki tena. Furaha ya kweli ipo katika kumtafuta Mungu na kuziishi Heri za Mlimani. Mtakatifu Augustino anasema furaha ya kweli inadumu na wala haitokani na vitu bali inatokana na ushirika wa kudumu na Mwenyezi Mungu mwenyewe. Mwenyezi Mungu ndiye wema mkuu (Summum bonum), ndiye lengo la mwisho la maisha ya binadamu (Finis ultimus). Mwenyezi Mungu ndiye mwenye haki ya kutoa heri kwa maskini wa roho na wenye kiu ya haki, kwani Mwenyezi Mungu ndiye Hakimu mwenye haki, chanzo na hatima ya amani ya kweli. Heri wenye rehema na wenye moyo safi watapata furaha, kwani Mwenye Mungu ni ukamilifu wa matamanio yote ya binadamu. Katika mateso, dhuluma na nyanyaso, Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya faraja na ukweli ndiyo maana Kristo Yesu anawaambia wafuasi wake: kufurahi na kushangilia kwa kuwa thawabu yao ni kubwa mbinguni. Rej. Mt 5:12.
Hotuba ya Mlimani au Heri za Mlimani (Rej. Mt 5: 17-37) ni: dira na mwongozo wa maisha ya Kikristo. Ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wanafunzi wake anayewataka kwa namna ya pekee: Wawe na huzuni na umaskini wa roho; wawe na njaa na kiu ya haki; wawe na rehema, wenye moyo safi na wapatanishi. Hotuba hii ni faraja ya Roho Mtakatifu kwa wale ambao wamekombolewa na kuweka nyoyo zao wazi kwa ajili ya kupokea neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kiasi kwamba, wako huru. Heri za Mlimani ni chemchemi ya furaha ya upendo aminifu wa Mungu unayobubujikia maisha ya waamini! Hii ni furaha endelevu ambayo hakuna mtu wala mazingira yanayoweza kuwapokonya watoto wapendwa wa Mungu. Hotuba hii ni kiungo kati ya Agano la Kale na Agano Jipya; ni utimilifu wa Torati na Unabii; ni chemchemi ya furaha ya kweli, dira na mwongozo wa kufikia furaha ya kweli, maisha na uzima wa milele; kielelezo cha imani tendaji inayomwilishwa katika huduma; ushuhuda wa upendo wa Mungu na binadamu. Baada ya Kristo Yesu kuwafundisha wafuasi wake kuhusu Hotuba ya Mlimani, maarufu kama Heri za Mlimani, anafafanua jinsi ambavyo mwamini anapaswa kuanzisha mahusiano na Mwenyezi Mungu kwa kuzingatia Sheria na Manabii, mambo ambayo yanapata utimilifu wake katika Kristo Yesu, kielelezo cha upendo na haki ya Mungu ambayo inavuka utekelezaji wa Amri za Mungu inayokita msingi wake katika upendo kwa Mungu na hivyo kuwabidiisha waamini kupendana.
Hii ni sehemu ya tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya Sita ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa iliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 15 Februari 2026, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kristo Yesu anafafanua kuhusu utimilifu wa Sheria ya Ufalme wa Mungu na Sheria ya kidini: “Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa… bali mimi nawaambieni.” Sheria na Unabii vimetolewa na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Musa, kama njia ya kuweza polepole kumfahamu Mwenyezi Mungu na Mpango wake wa ukombozi kwa mwanadamu na historia yake. Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa anasema, watu walikuwa wamefungwa chini ya Sheria mpaka pale imani itakapofunuliwa na kwamba, Torati imekuwa ni mwongozo wa kuwapeleka watu wa Kristo Yesu na kwamba, kwa sasa wote wamekuwa ni waana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu, utimilifu wa Sheria na Torati (Rej. Gal 3: 23-25) na hivyo kufanyika kuwa ni ndugu na jamaa wa Kristo Yesu. Haki ya kweli anasema Baba Mtakatifu Leo XIV inafumbatwa katika upendo unaomwilishwa katika matendo kwa kuthamini: utu, heshima na haki zake msingi. Kwa wanandoa haitoshi kuwa waaminifu ikiwa kama katika mahusiano na mafungamano yao ya ndoa kunakosekana: huruma, kusikilizana, kuheshimiana, kujaliana, na kutembea pamoja katika lengo moja. Hii ni mifano kutoka kwa Kristo Yesu, waamini wanaweza kuongeza mifano mingine zaidi. Fundisho kuu ni hili, haki ndogo haitoshi; upendo mkuu unahitajika, jambo ambalo linawezekana kutokana na uweza wa Mwenyezi Mungu. Mwishoni, mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuungana kwa pamoja na kumwomba Bikira Maria aliyemzaa Kristo Yesu kwa ulimwengu, Kristo Yesu aletaye na kutimiza mpango wa ukombozi, awaombee na kuwasaidia kuingia katika mantiki ya Ufalme wa Mungu na kuishi kazi yake.