Tafuta

Sherehe ya Watakatifu Wote: Heri za Mlimani Ni Utambulisho wa Watakatifu: Mashuhuda wa Amani

Heri za Mlimani ni kitambulisho cha watakatifu wa Mungu, waliojitahidi kusoma alama za nyakati, wakajitosa na kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa amani ambayo ni dhamana kubwa, inayohitaji ushirikiano na uvumilivu. Waamini wajitahidi kupandikiza mbegu ya amani nyoyoni mwao ili iweze kuchipusha uhai, kukua katikaa matendo ya haki na huruma: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu wote, tarehe 1 Novemba ya kila Mwaka, Mama Kanisa anapenda kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa, shukrani na utukufu kwa ajili ya watakatifu wote hata wale ambao bado hawajatambuliwa rasmi na Kanisa lakini ni sehemu ya umati mkubwa wa wateule wa Mungu “Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-Kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao.” Ufu 7:9. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema kwamba, watu wote wanaitwa kuwa ni watakatifu na wakamilifu kama alivyo Baba yao wa mbinguni. Wafuasi wa Kristo wanaitwa kuwa watakatifu kadiri ya neema na hivyo kuhesabiwa haki katika Kristo Yesu katika Ubatizo wa imani unaowafanya kuwa kweli ni watoto wa Mungu na washiriki wa tabia ya Mungu, na hivyo watakatifu halisi. Kumbe, wanapaswa kujivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu na wawe na matunda ya Roho ili wafanywe watakatifu. Watambue kwamba, huku bondeni kwenye machozi, mara nyingi wanajikwaa ndiyo maana wanapaswa kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu. Rej. Lumen gentium 40. Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu wote ni kutambua utakatifu wa Kanisa unaosimikwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Rej. Lumen gentium 39.

Sherehe ya Watakatifu wote ni ushuhuda wa Utakatifu wa Kanisa
Sherehe ya Watakatifu wote ni ushuhuda wa Utakatifu wa Kanisa

Sherehe ya Watakatifu Wote imekuwa ikiadhimishwa na Makanisa ya Mashariki tangu Karne nne. Ni katika uongozi wa Papa Gregori IV (827 – 844) akatamka wazi kwamba, tarehe 1 Novemba ya kila mwaka itakuwa ni Sherehe ya Watakatifu Wote. Wafuasi wa Kristo Yesu wanaalikwa kuliishi kikamilifu Fumbo la Ukombozi kutoka katika utumwa wa dhambi kwa kumtafuta Roho Mtakatifu bila ya kuchanganya mambo. Heri za Mlimani zilizotangazwa na Kristo Yesu ni muhtasari wa Mafundisho yake makuu kwa wanafunzi wake. Kristo Yesu, anawataka kwa namna ya pekee wawe na huzuni na umaskini wa roho; wawe na njaa na kiu ya haki; wawe na rehema, wenye moyo safi na wapatanishi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, waamini wanapaswa kutambua kwamba, wana heri kwa sababu wao ni watoto wateule wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika Sherehe ya Watakatifu wote kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amesema kwamba, Heri za Mlimani ni chemchemi ya furaha ya upendo aminifu wa Mungu unaobubujikia maisha ya waamini! Hii ni furaha endelevu ambayo hakuna mtu wala mazingira yanayoweza kuwapoka watu wateule wa Mungu.

Heri za Mlimani ni muhtasari wa Mafundisho ya Yesu na Utambulisho wa waamini
Heri za Mlimani ni muhtasari wa Mafundisho ya Yesu na Utambulisho wa waamini

Heri za Mlimani ni kitambulisho cha watakatifu wa Mungu, waliojitahidi kusoma alama za nyakati, wakajitosa na kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa amani, badala ya kutaka kuishi katika amani na raha mstarehe pasi na matatizo. Amani ni dhamana kubwa, inayohitaji ushirikiano na uvumilivu. Waamini wajitahidi kupandikiza mbegu ya amani katika sakafu ya nyoyo zao, ili iweze kuchipusha uhai, na kuendelea kukua katika hali ya ukimya kwa njia ya matendo ya haki na huruma: kiroho na kimwili, kama wanavyoshuhudia watakatifu angavu wanaosherehekewa leo hii na Mama Kanisa. Kristo Yesu anapenda kuwakumbusha waja waje kwamba, amani ya kweli kamwe haiwezi kufumbatwa katika matumizi ya nguvu wala kwa “ncha ya upanga.” Maisha ya Kristo Yesu na yale ya watakatifu wake yanaonesha kwamba, mbegu ya amani ili iweze kukua na kuzaa matunda yanayokusudiwa lazima kwanza, ife. Amani ya kweli haiwezi kupatikana kwa mashambulizi ya silaha au kwa kumshinda adui! Ujenzi wa amani unaanza kushika kasi yake kutoka katika sakafu ya moyo wa mwanadamu, changamoto ikiwa ni kuondokana na mawazo ya vita na vurugu; maneno makali kama “ncha” ya upanga; kwa kuondokana na tabia ya kutowajali wengine na kutaka kujilinda kwa kuta ndefu na uzio wa umeme. Ili mbegu ya amani iweze kuchipua na kuzaa matunda yanayokusudiwa haina budi kutoa nafasi kwa Kristo Yesu ambaye kimsingi ni “amani yetu.” Efe 2:14.

Waamini wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa amani duniani
Waamini wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa amani duniani

Msalaba wa Kristo Yesu ni kiti cha amani! Ni vyema kupokea kutoka kwake ungamo la “msamaha na amani. Utakatifu wa maisha na upatanishi ni neema na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuchunguza dhamiri zao ili kuangalia ikiwa kweli ni wapenda amani katika maeneo yao kazi, wanakosoma na kuishi. Au wamekuwa ni sababu ya kinzani na mipasuko ya kijamii. Huu ni mwaliko kwa waamini kujielekeza zaidi katika njia ya amani, kwa kusamehe na kusahau; kwa kuwajali na kuwathamini maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Wajizatiti katika kusimamia haki na kurekebisha udhalimu pamoja na kuwasaidia wale wanapongukiwa. Baba Mtakatifu anasema, hii ndiyo njia bora zaidi ya mchakato wa ujenzi wa amani, kwa sababu heri wapatanishi kwa kuwa wataiwa ni watoto wa Mungu. Mt 5: 9. Watu kama hawa katika ulimwengu mamboleo wanaweza kuonekana kana kwamba, wamepitwa na wakati, kwa sababu wanakwenda kinyume cha mantiki ya matumizi ya nguvu na kushinda. Amani ndiyo matamanio halali ya watu wa Mungu katika ulimwengu mamboleo. Bikira Maria Malkia wa Amani, awasaidie waamini kuwa kweli ni vyombo na wajenzi wa amani katika uhalisia wa maisha ya kila siku.

Kanisa Takatifu

 

 

 

01 Novemba 2022, 15:01

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >