Papa Leo XIV: Yohane Mbatizaji Shuhuda wa Ukweli na Haki
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mara nyingi Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro alipenda: kutembelea, kusali na kuzungumza na wafungwa, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu unaoponya na kumwokoa mwanadamu, ili hatimaye aweze kugeuka na kuwa mtu mpya zaidi. Baba Mtakatifu alifanya yote haya kuwaonesha na kuwaonjesha wafungwa uwepo wake wa kibaba kwa njia ya sala katika shida na mahangaiko yao ya ndani, ili waweze kuwa na matumaini mapya katika maisha yao kwa siku za baadaye. Mama Kanisa katika maisha na utume wake kwa wafungwa magerezani anakazia hasa: Umuhimu wa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wafungwa magerezani, kwa kutambua kwamba, wafungwa na askari magereza ni vyombo na mashuhuda wa Injili. Askari magereza wawe na ujasiri wanapotekeleza dhamana na utume wao miongoni mwa wafungwa. Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza askari magereza kila wakati wanapotekeleza dhamana na utume wao kwa ajili ya ulinzi na usalama kwa maskini na wanyonge zaidi katika jamii, yaani wafungwa, ili kuhakikisha kwamba, haki, amani, ulinzi na usalama vinatawala ndani ya jamii.
Hii ni dhamana inayowataka siku kwa siku kuwa ni wajenzi wa haki na wajumbe wa amani kwa kuwakumbuka wafungwa hao waliofungwa kana kwamba, wamefungwa pamoja nao na kama wanadhulumiwa, basi hata wao wahisi haya madhulumu mwilini wao. Maisha ya gerezani ni magumu na mara nyingine yanaweza kukatisha tamaa, kwa mfungwa kuelemewa na upweke hasi, hali ya kukata tamaa na hatimaye kushindwa kuona hatima ya maisha yake. Gereza ni mahali pa mahangaiko ya binadamu. Askari magereza wanatumia muda mrefu kuwa magerezani, ili kulinda na kudumisha ulinzi na usalama, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinalindwa barabara. Askari magereza wawe ni walinzi wa ndugu zao wafungwa, wawe ni madaraja kati ya magereza na jamii katika ujumla wake kwa kuonesha upendo unaowawajibisha, ili kuondoa wasiwasi na kashfa ya kutowajali wengine. Askari magereza ni kutambua uzito wa kazi na wajibu wao kwa wafungwa pamoja na familia zao wenyewe. Kumbe, inawapasa kusaidiana na kushikamana ili kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa zinazopatikana kutokana na kazi na utume wao.
Ni katika muktadha wa maisha gerezani, Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mama Kanisa katika Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya tatu ya Kipindi cha Majilio Mwaka A wa Kanisa, tarehe 14 Desemba 2025 anawaalika waamini kumtembelea Yohane Mbatizaji gerezani, alikokuwa amefungwa kutokana na mahubiri yake. Rej Mt 14:3-5. Licha ya kufungwa gerezani, Yohane Mbatizaji hakupoteza kamwe matumaini na akaendelea kuwa ni alama na sauti ya kinabii iliyokita mizizi yake katika ukweli na haki. Akiwa gerezani, Yohane Mbatizaji alisikia matendo yake Kristo Yesu, kiasi cha kuwatuma wafuasi wake wakamuulizie ikiwa kama Yeye ndiye Masiha wa Bwana au wamtazamie mwingine? Yohane Mbatizaji alikuwa anatafuta ukweli na haki ndiyo maana anatuma wafuasi wake kumuulizia Kristo Yesu ikiwa ndiye Mwokovu aliyetumwa na Baba yake wa milele. Jibu la Kristo Yesu linawagusa watu aliowapenda upeo na aliokuwa anawahudumia yaani: Maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, wagonjwa, viziwi na kwamba, wafu wanafufuliwa, kielelezo cha Mungu anayehudumia na kuwaokoa waja wake. Hiki ndicho kiini cha Habari Njema, yaani kuwatangazia maskini Habari Njema na kwamba, matendo makuu ya Mungu yanaonekana!
Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV, “Dominica gaudete” yaani “Dominika ya furaha. Kristo Yesu anawaokoa waja wake kwa neno lake na kwamba, unabii wote unapata utimilifu katika maisha na utume wa Kristo Yesu, kiasi cha kuwafunulia watu utukufu wa Mungu, kwa kuwapatia ujasiri katika neno lake wale wote wanaodhulumiwa na kuteswa; kuwarejeshea sauti wale wasiokuwa na sauti na hivyo kushinda itikadi, kwa kujikita katika ukweli na haki; kwa kuponya yale mambo yanayoharibu mwonekana wa nje wa mwili. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Neno wa Mungu chemchemi ya maisha anamkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi linaloutesa moyo wa mwanadamu na hatimaye, kumsababishia kifo.
Huu ni mwaliko kutoka kwa Kristo Yesu kwa ajili ya wafuasi wake, kuungana pamoja naye, katika kipindi hiki cha Majilio, Kipindi cha subira ya ujio wa Mkombozi, kwa kuonesha vipaumbele vya Mwenyezi Mungu Ulimwenguni, kielelezo cha hali ya juu cha furaha ya kukombolewa na hivyo kukutana na Mkombozi wake ili aweze kufurahi daima: "Gaudete in Domino semper” kwa kujikita katika: Unyenyekevu, upole na maisha ya sala, ikisisitiza kwamba Bwana yu karibu. Huu ndio mwaliko unaotolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Dominika ya Tatu ya Kipindi cha Majilio. Kristo Yesu ni chemchemi ya matumaini kwa waja wake, wakati wa shida, mahangaiko na changamoto za maisha na hasa pale ambapo maisha yanapoteza na kukosa ladha, kiasi kwamba, mambo yote yanaonekana kuwa ni giza; kwa kukosa maneno na hivyo kugumisha hata ile hali ya kumsikiliza jirani! Mwishoni Baba anawaalika waamini kumwangalia Bikira Maria, kielelezo cha kungoja, usikivu na furaha, ili awasaidie kuiga utume wa Mwanawe kwa kuwagawia maskini chakuka cha Injili.