Tafuta

Papa Leo XIV: Katekesi Maadhimisho Jubilei ya Mwaka 2025 wa Ukristo: Fumbo la Pasaka

Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari kwa makini kuhusu Fumbo la Kifo na Uzima wa milele kwa matumaini na kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka, amewatangulia mbele yao katika jaribu la kifo, akashinda kifo na mauti na hatimaye, akawafungulia milango ya maisha na uzima wa milele. Anasema Pasaka ya Bwana ni jibu makini la mwisho kuhusu Fumbo la Kifo kwa Mwanadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu ameliangazia Fumbo la mateso na Kifo cha binadamu, kwa njia ya ushuhuda wa maisha na matendo yake, hasa pale, watu wanapoondokewa na wapendwa wao! Hata Kristo Yesu, mbele ya kaburi la rafiki yake Lazaro alitoa machozi, ushuhuda kwamba, Yesu yuko karibu sana na waja wake kama ndugu! Kwa uchungu mkubwa alimwombea Lazaro kwa Baba yake wa mbinguni, chemchemi ya uhai na hatimaye, akamwamuru Lazaro aliyekufa kutoka nje ya kaburi! Huu ndio mwelekeo wa matumaini ya Kikristo katika kukabiliana na Fumbo la Kifo! Kristo Yesu “anasimama dede” kupambana na kifo ambacho kimejitokeza katika kazi ya uumbaji kinyume kabisa cha upendo wa Mungu na Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu ambaye ameganga na kuponya Fumbo la Kifo katika maisha ya mwanadamu. Mababa wa Kanisa wanasema, maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo. Mkristo anayekufa katika Kristo Yesu huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi! Waamini wanahamasishwa kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu. Matumaini ya Kikristo yawasaidie waamini kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na matumaini na kwamba, hata ustaarabu wa watu wa kale umepitia katika fumbo hili na kwa hakika, ibada ya kifo ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu.

Fumbo la Pasaka ya Bwana Kwa mwaka 2025
Fumbo la Pasaka ya Bwana Kwa mwaka 2025

Kifo kinayaanika maisha ya binadamu kwa kumwondolea kiburi na kuwahimiza watu kujenga na kudumisha upendo, kutafuta na kuambata mambo msingi katika maisha, ili sadaka na majitoleo yao yaweze kuwapatia amani na utulivu wa ndani wanapokabiliana na Fumbo la Kifo!  Kristo Yesu anapenda kuimarisha matumaini ya waja wake kwamba, Yeye ndiye ufufuo na uzima! Jambo la msingi ni wao kumwamini. Mbele ya Fumbo la Kifo binadamu ni mnyonge na ni “mdogo sana kama kidonge cha piliton.” Lakini, neema katika hali na mazingira kama haya, inaweza tena kuamsha imani na Yesu mwenyewe kuwashika mkono watu wake na kuwaambia “Talitha kum” tafsiri yake “Msichana, nakuambia, inuka.” Haya ni maneno ambayo Yesu anapenda kumwambia kila mtu, simama na fufuka tena! Haya ndiyo matumaini ya Kikristo mbele ya Fumbo la Kifo. Kwa mwamini hili ni lango ambalo liko wazi; lakini kwa mwenye mashaka, ni giza linalomwandama na kumtumbukiza mtu katika majonzi na msiba mkuu. Kwa kila mwamini, hii itakuwa ni neema siku ile mwanga huu utakapoangaza. Kifo ni sehemu ya matukio ya maisha ya mwanadamu, ni urithi na kumbukumbu. Tangu pale mwanadamu anapozaliwa, anaanza safari ya kuelekea katika Fumbo la kifo, changamoto na mwaliko kwa waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwajalia kufa kifo chema badala ya kujifungia katika muda na ubinafsi wao! Mama Kanisa anawataka watoto wake kujiandaa vyema ili kukabiliana na Fumbo la kifo katika maisha yao. Kifo ni urithi unaofumbatwa katika ushuhuda ambao unapaswa kutolewa kwa wale wanaobaki.

Ufufuko wa Kristo Yesu ni Kweli ya imani ya Kikristo
Ufufuko wa Kristo Yesu ni Kweli ya imani ya Kikristo   (ANSA)

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani “Mahujaji wa matumaini.” Ni katika mwendelezo wa Injili ya Matumaini, Baba Mtakatifu Leo XIV tayari amekwisha kugusia kuhusu maisha na utume wa Kristo Yesu, tangu kuzaliwa; mateso, kifo na ufufuko uletao maisha na uzima wa milele na kwamba, matumaini ya waamini yanasimikwa katika Fumbo la Pasaka, kielelezo cha ukweli wa maisha na historia ya mwanadamu sanjari na changamoto zake: katika furaha, hofu, woga na wasiwasi. Kiini cha imani yetu na moyo wa tumaini letu anasema Baba Mtakatifu Leo XIV vimekita mizizi katika ufufuo wa Kristo Yesu. Kwa kusoma Injili kwa uangalifu, tunatambua kwamba fumbo la Pasaka ni la kushangaza, si kwa sababu tu Kristo Yesu, Mwana wa Mungu alifufuka kutoka wafu, bali pia kwa sababu ya njia aliyochagua kufanya hivyo. Kwa kweli, ufufuo wa Kristo Yesu si ushindi wa kishindo, wala si kulipiza kisasi dhidi ya adui zake bali ni ushuhuda wa ajabu jinsi upendo unavyoweza kuinuka tena baada ya kushindwa sana kuendelea na safari yake isiyozuilika. Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka wafu; kilele cha ukweli wa imani katika Kristo Mfufuka; Ni ufunuo wa Uungu wa Kristo Yesu unaowapatia waamini maisha ya uzima mpya na hivyo kuhesabiwa haki pamoja na kufanywa wana wateule wa Mungu. Ufufuko wa Kristo ni msingi wa ufufuko wa miili na uzima wa milele ijayo! Ndiyo maana Pasaka ni Sherehe kubwa katika Kanisa. Hii ni Sherehe ya upendo, huruma na msamaha wa Baba wa milele unaofumbatwa katika Msalaba. Ufufuko wa Bwana umesimikwa katika fadhila ya unyenyekevu, katika hali na mazingira ya wafuasi wake! Kimsingi huu ni muhtasari wa Katekesi ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo: Kristo Yesu ni tumaini letu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Ufufuko wa Kristo Yesu ni chemchemi ya matumaini ya waja wake, yanayowawezesha kuonja furaha na amani ya kweli inayotolewa na Kristo Yesu, hadi milele yote!

Ufufuko wa Kristo Yesu ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo
Ufufuko wa Kristo Yesu ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo   (@VATICAN MEDIA)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika Katekesi yake, Jumatano tarehe 10 Desemba 2025 anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari kwa makini kuhusu Fumbo la Kifo na Uzima wa milele kwa matumaini na kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka, amewatangulia mbele yao katika jaribu la kifo, akashinda kifo na mauti na hatimaye, akawafungulia milango ya maisha na uzima wa milele. Anasema Pasaka ya Bwana ni jibu makini na la mwisho kuhusu Fumbo la Kifo kwa Mwanadamu. Tafakari hii imenogeshwa na sehemu ya Neno la Mungu kuhusu kuzikwa kwa Kristo Yesu, tukio lililotekelezwa na Yusufu wa Arimathaya: “Mtu huyo alikwenda kwa Pilato, akataka kupewa mwili wa Yesu. Akaushusha, akauzinga sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililochongwa mwambani, ambalo hajalazwa mtu bado ndani yake. Na siku ile ilikuwa siku ya Maandalio, na sabato ikaanza kuingia.” Lk 23:52-54. Fumbo la kifo linaweza kuonekana kuwa ni jambo la kawaida kwani kifo ni sehemu ya maisha ya binadamu na kwamba, kila kiumbe kinapitia kifo. Kifo pia ni Fumbo kutokana na hamu ya binadamu kutaka kupata maisha na uzima wa milele; mitazamo miwili inayokinzana. Katika Ulimwengu mamboleo, kifo kinaonekana kuwa ni tukio linalopaswa kuwekwa mbali, tukio ambalo watu wanapaswa kulizungumzia kwa sauti ya chini, kwani linatikisa na kuvuruga hisia za binadamu, hali ambayo inawafanya sasa watu wengi kushindwa kutembelea makaburi, ili kuwaombea ndugu zao waliolala katika usingizi wa amani wakiwa na tumaini katika ufufuko, maisha na uzima wa milele. Lakini Fumbo la kifo halina sauti ya mwisho katika maisha ya mwanadamu, hata kama kila mtu ataonja kifo. Hili ni tukio ambalo kamwe mwanadamu hapaswi kulifumbia macho, ni kielelezo cha unyonge wake. Mtakatifu Alfonsi Maria de’ Liguori anasema kifo ni mwalimu mkuu wa maisha, changamoto na mwaliko kwa waamini kuchagua mambo msingi katika maisha, ili hatimaye kuishi katika ukweli na ukamilifu kwa kutambua kwamba, mwanadamku hapa duniani ni mpita njia na kwamba, hana makao ya kudumu, hivyo anapaswa kujiandaa kwa ufufuko na maisha ya uzima wa milele!

Kifo haina neno la mwisho  kwa wanao amni
Kifo haina neno la mwisho kwa wanao amni   (@VATICAN MEDIA)

Si jambo la kushangaza leo hii anasema Baba Mtakatifu Leo XIV kuona kwamba bado maono mengi ya sasa ya kianthropolojia yanaahidi kutokufa, nadharia ya kurefushwa kwa maisha ya kidunia kupitia teknolojia. Hii ni hali inayojitokeza kama moja ya changamoto katika Ulimwengu mamboleo. Je, kweli kifo kinaweza kushindwa na sayansi? Lakini basi, Je, sayansi hiyo hiyo inaweza kutuhakikishia kwamba maisha bila kufa pia ni maisha yenye furaha? Tukio la Ufufuo wa Kristo Yesu linatufunulia kwamba, kifo hakipingani na uzima, lakini ni sehemu yake muhimu kama njia ya uzima wa milele. Pasaka ya Bwana Yesu Kristo inatupa mwonjo wa mbele, katika wakati huu ambao bado umejaa mateso na majaribu, ya utimilifu wa kile kitakachotokea baada ya kifo. Mwanga unaochomoza katika giza la kifo, Mwinjili Luka anasema: “Na siku ile ilikuwa ni siku ya Maandalio, na sabato ikaanza kuingia” Lk 23:54, huo ndio “Mwanga wa Sabato,” Mwanga mpya wa Ufufuko wenye uwezo wa kuangaza Fumbo la kifo na hivyo kuwa ni chemchemi ya matumaini, kwani kifo si tukio la mwisho katika maisha ya mwanadamu, bali ni njia ya kuelekea kwenye mwanga angavu, yaani furaha ya maisha na uzima wa milele. Baba Mtakatifu Leo XIV anahitimisha Katekesi kuhusu Pasaka ya Bwana kuwa ni jibu makini la mwisho kuhusu Fumbo la Kifo kwa Mwanadamu kwa kusema kwamba, Kristo Yesu Mfufuka amewatangulia waja wake katika jaribu kuu la Fumbo la kifo, akaibuka kidedea na mshindi kutokana na nguvu ya Upendo wa Kimungu. Hivyo, akawatayarishia waja wake mahali pa pumziko la milele, makao wanayongojea kwa matumaini; na hatimaye akawakirimia utimilifu wa maisha ambayo hakuna tena vivuli na migongano. Shukrani kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka tena kwa ajili ya upendo, pamoja na Mtakatifu Francisko wa Assis, waamini wanaweza kuliita Fumbo la kifo: “Dada.” Huu ni mwaliko wa kuweza kuingoja siku hii kwa tumaini la hakika la Ufufuko wa wafu na hivyo kuwahifadhi kutokana na hofu ya kutoweka milele, huku akiwatayarishia furaha ya maisha ya milele.

Papa Leo Fumbo la Pasaka

 

 

10 Desemba 2025, 15:16

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >