Tafuta

Papa Leo XIV: Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili

Baba Mtakatifu Leo XIV katika Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 8 Desemba 2025 amekazia kuhusu furaha ya Mama Kanisa kwa zawadi ya Bikira Maria aliyekingiwa dhambi ya asili, kielelezo cha usafi na utakatifu ili aweze kumzaa, Kristo Yesu, Mwana wa Mungu kwa ajili ya wokovu wa walimwengu. Sherehe hii ilitangazwa tarehe 8 Desemba 1854 na Papa Pio IX.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kipindi cha Majilio ni fursa adhimu kwa waamini kulitafakari kwa namna ya pekee, Fumbo la Umwilisho, Kristo Yesu alipozaliwa kwa mara ya kwanza katika historia na maisha ya mwanadamu na kwamba, atakuja tena kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Hiki ni kipindi cha subira, imani na matumaini yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini. Majilio ni kipindi kinachomwandaa mwamini kuadhimisha vyema Fumbo la Umwilisho. Kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu ni chemchemi ya matumaini, imani na furaha; tema muhimu sana wakati huu na kwamba, Bikira Maria anayo nafasi ya pekee katika maadhimisho ya Kipindi cha Majilio. Tarehe 8 Desemba 2025, Kanisa linaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, kiini cha Kipindi cha Majilio. Maadhimisho haya ni kielelezo cha matukio muhimu sana yaliyojiri katika maisha na utume wa Bikira Maria, aliyekingiwa dhambi ya asili hata kabla ya Kristo Yesu kuzaliwa. Tangu kutungwa kwake mimba, Bikira Maria alikingiwa dhambi ya asili, kielelezo cha upendo wa Mungu unaotakatifuza na hivyo kumkinga na kila doa la dhambi ya asili ambayo binadamu wote wameirithi. Papa Pio IX kunako tarehe 8 Desemba mwaka 1854 katika Waraka wake wa Kitume “Ineffabilis Deus”, alitangaza rasmi kwamba, Mwenyeheri kabisa Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee wa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Haya ni mafundisho tanzu ya Kanisa, kielelezo cha mng’ao wa utukufu wa Bikira Maria! Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Desemba. Sherehe hii haitukuzi tu usafi, uzuri na utakatifu wa Bikira Maria bali ni fundisho la imani ambalo waamini wanapaswa kuliamini kina. Haya ni mafundisho tanzu ya Kanisa, kielelezo cha mng’ao wa utukufu wa Bikira Maria! “Mwezi wa sita, Malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani?

Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili
Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili   (@VATICAN MEDIA)

Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.” Lk 1:26-38. Baba Mtakatifu Leo XIV katika tafakari yake, kama sehemu ya Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 8 Desemba 2025 amekazia kuhusu furaha ya Mama Kanisa kwa zawadi ya Bikira Maria aliyekingiwa dhambi ya asili, kielelezo cha usafi na utakatifu wa hali ya juu kabisa ili aweze kumzaa, Kristo Yesu, Mwana wa Mungu kwa ajili ya wokovu wa walimwengu. Huu ni upendeleo wa pekee na muujiza mkubwa kabisa, uliomwezesha Bikira Maria, kujaa neema na hivyo kuwa tayari kuukubali na kuupokea mpango wa Mungu katika maisha yake! Katika maoni yake, Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa anasema, Bikira Maria aliamini, na ndani yake kile alichoamini kilitimia na kwamba, karama ya utimilifu wa neena katika Bikira Maria iliweza kuzaa matunda kwa sababu Bikira Maria, katika uhuru wake, aliupokea na kuukumbatia mpango wa Mungu katika maisha yake, katika uhuru kamili.

Papa Leo XIV Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili
Papa Leo XIV Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili   (@Vatican Media)

Hii ni changamoto na mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, yale yaliyotimia ndani ya Bikira Maria, yapate pia nafasi katika maisha na utume wa waamini, ili yaweze kuwafaa pia. Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, inawafanya waamini kufurahia uzuri usio na doa wa Mama wa Mungu, na mwaliko wa kuamini kama alivyoamini yeye kwa kutoa kibali chao cha ukarimu kwa maisha na utume ambao Kristo Yesu anawakarimia kila mmoja. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, ule muujiza wa Bikira Maria kutungwa mimba bila dhambi ya asili unapyaishwa tena kwa ajili ya waamini kwa kutakaswa na dhambi ya asili kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na hivyo waamini wanafanyika kuwa ni watoto wa Mungu, Makao yake na Hekalu la Roho wake Mtakatifu na hivyo kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini wanamkaribisha Kristo Yesu ili aweze kuishi ndani mwao na hivyo kujenga umoja, tayari kushirikiana na Mama Kanisa katika maisha na utume wa kila mwaamini katika kuleta mageuzi katika Ulimwengu mamboleo. Zawadi ya kutungwa mimba bila dhambi ya asili ni kubwa kama ilivyo pia Sakramenti ya Ubatizo. Ndiyo ya Bikira Maria ni ajabu, lakini pia ukubali wa waamini unaweza kupyaishwa kwa uaminifu kila siku; kwa shukrani, unyenyekevu na uvumilivu; katika sala na matendo madhubuti ya huruma: kiroho na kimwili hadi katika huduma za kawaida na za kila siku, ili Kristo Yesu ajulikane, akaribishwe na kupendwa kila mahali, ili hatimaye wokovu wake uweze kuwafikia watu wote! Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sala na kwa maombezi ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, ili muujiza huu uweze kutendeka katika maisha ya waamini, kwa kuongozwa na maneno ambayo Bikira Maria mwenyewe aliweza kuyaamini.

Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili
08 Desemba 2025, 16:05

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >