Tafuta

Papa Leo XIV: Kristo Yesu Ni Ufunuo wa Huruma, Upendo na Ukarimu wa Mungu

Muujiza wa mikate mitano na samaki wawili kule jangwani ni ushuhuda kwamba, Kristo Yesu ndiye Mkate wa uzima ulioshuka kutoka mbinguni, anayewakirimia waja wake mahitaji yao kiasi hata cha kuweza kukusanya vikapu kumi na viwili vya mabaki ya chakula kielelezo cha makabila kumi na mawili ya Israeli. Hiki ni kielelezo kwamba, zawadi ya Mungu ni kwa ajili ya watu wote na kamwe haiwezi kupungua amesema Papa Leo X1V wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana.

Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.

Muujiza wa ukarimu unaosimuliwa katika Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 18 ya Mwaka A wa Kanisa mintarafu Injili kama ilivyoandikwa na Mt 14:13-21, ni sehemu ya maisha na utume wa Kristo Yesu hapa Ulimwenguni. Kristo Yesu anajipambanua kuwa ni Masiha wa Bwana kama ilivyokuwa kwa Musa katika Agano la Kale ambaye amekuja kuganga na kuponya magonjwa yanayomwandama mwanadamu; kuwashibisha watu wenye njaa na kuwanywesha wenye kiu ya haki na amani. Kristo Yesu ni ushuhuda wa ufunuo wa Mungu ambaye ni mwingi wa huruma na mapendo; na ana ukarimu usiokuwa na mfano, kwani anawakirimia wanadamu wote neema na baraka zake bila ya ubaguzi wala choyo. Huu ni mwaliko kwa waamini hata wao katika safari ya maisha yao kujitahidi kumwiga Kristo Yesu ambaye amekuja kumletea mwanadamu ukombozi, kwa kumpatia maana ya maisha na kumkomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kristo Yesu Mkombozi wa ulimwengu ndiye anayewajalia vipofu kuweza kuona tena, na visiwi kuweza kusikia tena na viwete anawajalia uwezo wa kutembea tena.

Yesu Kristo ni Mkate Ulioshuka kutoka mbinguni
Yesu Kristo ni Mkate Ulioshuka kutoka mbinguni   (@Vatican Media)

Ushuhuda wa Kristo Yesu kwa kipofu anayejaliwa uwezo wa kuona tena; kwa kuwashibisha wenye njaa na kuwanywesha wenye kiu; ni sehemu ya mchakato wa kukutana na Kristo anayewajalia tajiriba mpya. Muujiza wa mikate mitano na samaki wawili kule jangwani ni ushuhuda kwamba, Kristo Yesu ndiye Mkate wa uzima ulioshuka kutoka mbinguni, anayewakirimia waja wake mahitaji yao msingi kiasi hata cha kuweza kukusanya vikapu kumi na viwili vya mabaki ya chakula kielelezo cha makabila kumi na mawili ya Israeli. Hiki ni kielelezo kwamba, zawadi ya Mungu ni kwa ajili ya watu wote na kamwe haiwezi kupungua. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo X1V wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 2 Agosti 2026.

Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma, upendo na ukarimu wa Mungu
Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma, upendo na ukarimu wa Mungu   (@Vatican Media)

Kristo Yesu ndiye anayezima njaa ya binadamu anayetafuta ukweli na uzima na kwamba, katika muujiza wa kulisha watu elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili, fundisho ni kwamba, hakuna kitu kinachoweza kupotea iwapo kitagawanywa vyema, changamoto kwa waamini ni kuondokana na uroho na uchu wa mali, na kwamba, watumie mali na vyote walivyonavyo kwa ajili ya huduma kwa jirani zao, wawalishe wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu na kuwajalia amani, wale wote wanaoteseka kwa vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika jangwa la vita na kiburi cha mwanadamu, wajifunze jinsi ambavyo Kristo Yesu "alivyotazama juu mbinguni," "akabariki," na "akaimega mikate na kuwapa" wanafunzi wake ili wawagawie umati.

Ufunuo wa upendo wa Mungu umefikia kilele chake kwenye Karamu ya Mwisho
Ufunuo wa upendo wa Mungu umefikia kilele chake kwenye Karamu ya Mwisho   (ANSA)

Katika muujiza huu wa: huruma, upendo na ukarimu wa Mungu unafikia kilele chake kwenye Karamu ya Mwisho, Kristo Yesu anapokabidhi maisha yake kama ndugu katika ubinadamu. Furaha ya Ekaristi Takatifu iwasaidie waamini kushuhudia uzuri na utakatifu wake katika matendo ya maisha ya kila siku, kwa kugawana baraka ya mezani kwa chakula cha kimwili. Waamini wakiwa wameambatana na Kristo Yesu, hata sikukuu zinaweza kuwa ni fursa ya amani na ujenzi wa udugu wa kibinadamu, kwa kuwajali jirani zao wenye mahitaji wanaowazunguka. Bikira Maria Mama anayejali, awasaidie waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukua katika fadhila ya upendo, ili kamwe asiwepo mtu anayekufa kwa baa la njaa sehemu yoyote ile duniani.

Ekaristi Takatifu
02 Agosti 2026, 14:28

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >