Tafuta

Papa Leo XIV:Msibweteke kwa Mafanikio, Msikate Tamaa Kwa Magumu: Imani Thabiti!

Papa Leo XIV anasema, Kristo Yesu, kamwe hawezi kuwaacha, waamini wakimkaribisha kwa moyo wa unyenyekevu ndani ya mashua ya mioyo yao kwa njia ya: Sala, Sakramenti za Kanisa, Kwa kusoma, Kutafakari na Kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha na kwamba, kwa njia hii, wataweza kupata amani na utulivu, pamoja na mwanga na nguvu ya kuendelea na safari ya maisha. Waamini wasibweteke kwa mafanio, wala kukata tamaa kwa magumu! Imani!

Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema miujiza iliyotendwa na Kristo Yesu ililenga kuwaimarisha Mitume na wafuasi wake katika imani, matumaini na mapendo; kuonesha uwezo wake wa Kimungu, na hatimaye, kufunua upendo na huruma kwa wenye shida. Miujiza hii ilithibitisha mamlaka yake juu ya asili, magonjwa, na hata kifo, ikawasaidia wanafunzi wake kumwamini Yeye kama Mwana wa Mungu. Ni katika muktadha huu, Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 19 ya Mwaka A wa Kanisa inawaonesha Mitume wa Yesu wakitaabika sana na mawimbi na Kristo Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari. Rej. Mt 14:22-33. Tukio hili linakuja baada ya Kristo Yesu kuwalisha watu zaidi ya elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili. Kristo Yesu aliwalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng’ambo na yeye akatumia muda huu kwa ajili ya kusali peke yake, lakini wanafunzi wake walijikuta wanatishika sana kutokana na mawimbi makubwa yaliyokuwa yakikipiga chombo chao.

Waamini kamwe wasibweteke kwa mafanio wala wasikate tamaa kwa magumu
Waamini kamwe wasibweteke kwa mafanio wala wasikate tamaa kwa magumu   (ANSA)

Hawa Mitume walikuwa wameshuhudia muujiza mkubwa uliotendwa na Kristo Yesu. Wakawa ni mashhuhuda wa matendo makuu ya Mungu, lakini kwa sasa mbele yao wanatishiwa na mawimbi makubwa, wakasinyaa sana, kwani upepo ulikuwa wa mbisho. Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku, Kristo Yesu akawaendea kwa miguu na walipomwona akitembea, wakafadhaika sana na kuanza kupiga makelele kwa hofu. Lakini Kristo Yesu akawaambia: “Jipeni moyo, ni mimi msiogope.” Uwepo wa Kristo Yesu ukaleta mabadiliko makubwa, kiasi hata cha Mtakatifu Petro kuthubutu kumwomba Kristo Yesu aende kwake akitembea juu ya maji, lakini alipouona upepo, akaogopa, akaanza kuzama, akapiga kelele akisema, Bwana niokoe, mara Kristo Yesu akanyoosha mkono wake, akamshika, nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma na wanafunzi wake wakamsujudia wakisema: “Hakika wewe u mwana wa Mungu.” Mt 14: 33.

Mkaribisheni Yesu Moyoni mwenu kwa unyenyekevu!
Mkaribisheni Yesu Moyoni mwenu kwa unyenyekevu!   (@Vatican Media)

Hii ni sehemu ya tafakari yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican Dominika tarehe 9 Agossti 2026. Kiri hii ya imani ni matokeo ya Mitume kushuhudia muujiza ule wa kuwalisha watu zaidi ya elfu tano, wakapitia na kuonja udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu na hatimaye, wakaona na kutambua uwepo angavu wa Mwenyezi Mungu kati yao na mara macho na mioyo yao ikafunguka na hatimaye, wakapata amani na utulivu wa ndani kati kati ya mawimbi makubwa na upepo wa mbisho. Hili ni tukio ambalo limmeonesha imani haba ya Mitume wake, kiasi kwamba, siku moja atawaambia: “Mkiwa na imani, msipokuwa na shaka, mtafanya si hilo la mtini tu, lakini hata mkiuambia mlima huu, Ng'oka, ukatupwe baharini, litatendeka.” Mt 21:21. Ni katika muktadha huu anasema Baba Mtakatifu Leo XIV Mitume wa Yesu wakapata amani na utulivu moyoni. Muujiza huu unatoa fundisho kubwa kwa waamini kwamba, kamwe wasiruhusu mafanikio yawafanye kujivuna na kujiona wao kuwa ni bora kupita kiasi; wasikate tamaa hata kati kati ya nyakati za giza, wanapohisi kukosa nguvu mbele ya matatizo, shida na changamoto mbalimbali za maisha, kiasi kwamba, licha ya juhudi zao za kusonga mbele, lakini wanajikuta wakirudi nyuma badala ya kusonga mbele.

Mkaribisheni Yesu Nyoyoni mwenu: Kwa Sala, Neno, Sakramenti na Ushuhuda
Mkaribisheni Yesu Nyoyoni mwenu: Kwa Sala, Neno, Sakramenti na Ushuhuda   (AFP or licensors)

Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, yote haya ni tisa, kumi ni kwamba, Kristo Yesu, kamwe hawezi kuwaacha, waamini wakimkaribisha kwa moyo wa unyenyekevu ndani ya mashua ya mioyo yao kwa njia ya: Sala, Sakramenti za Kanisa, Kwa kusoma, Kutafakari na Kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha na kwamba, kwa njia hii, wataweza kupata amani na utulivu, pamoja na mwanga na nguvu ya kuendelea na safari ya maisha. Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa awasaidie waamini kuishi kwa namna hii, kwa kujikabidhi na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu kwani ni kwa njia ya imani thabiti, Bikira Maria alitangazwa kuwa ni Mwenyeheri. Re. Lk 1:45.

Miujiza ya Yesu
09 Agosti 2026, 14:43

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >