Tafuta

Papa leo XIV Kristo Yesu ni Hazina na Lulu ya Thamani Kubwa Maishani

Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana amesema, kiini cha mafundisho ya Kristo Yesu katika Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 17 ya Mwaka A wa Kanisa ni Fumbo la Ufalme wa Mungu, ambao Injili inaufananisha na lulu na hazina ya thamani kubwa, Kristo Yesu ndiye hazina na lulu hii ya thamani! Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanajibidiisha kuitafuta na kuipata kwa udi na uvumba katika hija ya maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kiini cha mafundisho ya Kristo Yesu katika Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 17 ya Mwaka A wa Kanisa ni Fumbo la Ufalme wa Mungu, ambao Injili inaufananisha na lulu na hazina ya thamani kubwa. Rej Mt 13:44-52. Mifano hii inaonesha mshangao wa wale wanaopata kitu ambacho hawakuwahi hata kukitarajia kiasi kwamba kuuza au kuacha kila kitu nyuma hakuonekani tena kuwa ni sadaka, bali faida. Hakika, tangu kurasa za mwanzo kabisa, Waandishi wa Injili wanaelezea wito wa Kristo Yesu wa kumfuata kuwa wenye mvuto usiozuilika: kwani huu ni wito wa hiari, bila shaka, lakini wa dharura na wenye uwezo wa kuchochea mwitikio wa haraka unaotokana na hamu pamoja na msukumo wa ndani. Hii ni sehemu muhimu ya jinsi Mwenyezi Mungu anavyojikaribisha na kuruhusu kupatikana kwake: kukutana na Ufalme wake ni tukio muhimu linalobadilisha maisha ya mwanadamu; kwani haliyabani maisha, bali huyafungua na kuyapanua zaidi. Ikiwa kuna jambo lolote linalopaswa kubadilika sasa, ni kwa ajili ya kupata fursa kubwa zaidi. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, akiwa Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, Dominika tarehe 26 Julai 2026.

Papa Leo XIV akitoa tafakari wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana
Papa Leo XIV akitoa tafakari wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV anaendelea kusema kwamba, kuna kipengele cha pili ambacho kinaonekana kuwa na umuhimu mkubwa kwa Kristo Yesu yaani: mtu anayepata hazina iliyofichwa shambani huenda ni mkulima; kwa upande mwingine, lulu hutambuliwa kuwa na thamani kubwa na mfanyabiashara labda msafiri. Mifano mingine miwili inafuata, ikihusisha wavuvi na mwandishi wa sheria mwenye ujuzi wa mambo ya kale na mapya. Kuna mingine pia, ambapo Ufalme unaweza kuonekana kupitia mwanamke anayekanda unga, mwingine anayepanga nyumba yake, mfalme anayepanga vita, mtu anayebuni ujenzi wa mnara, wasimamizi wanaoshughulikia malipo au uwekezaji, pamoja na wachungaji na wakulima. Kwa ufupi, Ufalme wa Mungu unafunua uzuri wake usio na kifani katika medani mbalimbali za maisha lakini unatoa mwaliko kwa kila mtu: wanaume na wanawake, vijana na wazee, maskini na matajiri ili kupyaisha maisha yao kwa kina kwani kila mtu anaweza kuuelewa Ufalme wa mbinguni na kuhisi kuvutiwa nao.

Papa Leo XIV akisalimiana na waamini pamoja na mahujaji
Papa Leo XIV akisalimiana na waamini pamoja na mahujaji   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, hata leo hii, Kanisa ni Ushirika wa watu wenye asili, tamaduni, ujuzi na viwango tofauti vya uwajibikaji, lakini wote wanaitwa na Kristo Yesu kujitambua kuwa ni “wamoja” katika Kristo Yesu kwani: Yeye ndiye ile hazina iliyofichwa, lulu ya thamani, na wavu unaokusanya wale waliotawanyika. Kwa hakika, tangu mwanzo kabisa, Kristo Yesu aliwaita na kuwakusanya karibu naye watu ambao, katika hali ya kawaida, wasingewahi kushirikiana wala kuchangamana. Kwa kufanya hivyo, alionesha kwamba Mwenyezi Mungu hana upendeleo na kwamba chaguo lake ni la upendo wa pekee, hasa kwa wanyenyekevu, waliotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Papa Leo XIV akitoa baraka kwa mtoto mdogo
Papa Leo XIV akitoa baraka kwa mtoto mdogo   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV amehitimisha tafakari yake huku akitoa mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuomba zawadi ya hekima na busara kama iliyoombwa na Mfalme kijana Sulemani. Rej. 2 Nya 2:1–12; 1 Fal 3:5, 7–12. Hiyo ni zawadi inayomwezesha mwamini kutambua lulu ya thamani kubwa, kutambua hazina ambayo kwa ajili yake inafaa kuuza kila kitu. Huu ni mwaliko kwa waamini kujifunza kuthamini mambo ya msingi yaani: kukuza na kudumisha hazina ya uhusiano wao na Mwenyezi Mungu, ambayo huwafungulia malango ya furaha na kuwasaidia kuishi vyema katika mahusiano na jirani zao. Kwa maombezi ya Bikira Maria, Kikao cha hekima awasaidie waamini kuelekeza hamu yao ya maisha kwa Kristo Yesu ili iweze kutimizwa kikamilifu.

Kristo Yesu ni Hazina
26 Julai 2026, 15:15

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >