Papa Leo XIV Katekesi Kuhusu Mtaguso Mkuu wa Pili Vatican: Mabadiliko ya Liturujia!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV baada ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, anaendeleza Mzunguko wa Katekesi unaojikita katika Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Usomaji Mpya wa Nyaraka zake, ili kugundua tena uzuri na umuhimu wa tukio hili la Kikanisa, Kipindi cha neema ambacho kwa hakika, Mama Kanisa amekifaidi sana katika Karne ya ishirini. Kumbe, hiki ni kipindi cha Kanisa kujikita zaidi katika Nyaraka Kuu 4 za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yaani: “Dei verbum” yaani “Ufunuo wa Kimungu”, “Sacrosanctum concilium” yaani “Juu ya Liturujia”; “Lumen gentium” yaani “Fumbo la Kanisa” pamoja na “Gaudium et spes” yaani “Kanisa katika ulimwengu mamboleo.” Katiba ya “Sacrosanctum concilium” yaani “Juu ya Liturujia” inaelezea kanuni za jumla za marekebisho na ukuzaji wa Liturujia Takatifu; Fumbo Takatifu la Ekaristi, Sakramenti nyingine na visakramenti; Liturujia ya Vipindi; Mwaka wa Liturujia wa Kanisa, Muziki Mtakatifu; na hatimaye, ni Sanaa Takatifu na Vifaa vitakatifu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanafafanua nafasi ya Liturujia katika fumbo la Kanisa kwa kusema kwamba, maana kwa njia ya Liturujia, hasa Sadaka takatifu ya Ekaristi, “latimizwa tendo la ukombozi wetu.” Liturujia inasaidia kikamilifu waamini waoneshe katika maisha yao na kuwadhihirishia wengine fumbo la Kristo Yesu na pia maumbile halisi ya Kanisa la kweli. Kanisa kwa undani kabisa ni la kibinadamu na pia la kimungu, linaloonekana lakini lenye mambo yasiyoonekana ndani yake, lenye bidii kubwa katika matendo na uradhi katika kutafakari, lililopo ulimwenguni lakini kama mwenye kufanya hija. Hayo yote yamo ili yale ya kibinadamu ndani yake yaelekezwe kwa yale ya kimungu, yaonekanayo kwa yasiyoonekana, matendo kwenye kutafakari, yaliyopo yaelekee mji ujao tunakoelekea.
Mwaka wa Liturujia wa Kanisa: Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Mama Kanisa takatifu huchukulia wajibu wake kuadhimisha kwa kumbukumbu takatifu kazi ya ukombozi ya Bwanarusi wake aliye Mungu katika siku zilizopangwa katika mwenendo wa mwaka mzima. Kanisa linaadhimisha Jumapili, “Dominika” yaani “Siku ya Bwana”. Hii ni Siku ya Mwenyezi Mungu alipokamilisha kazi ya uumbaji na kujipumzisha. Ni Siku ya Kristo Yesu kwa sababu Kanisa linakumbuka Ufufuko wale uletao uzima wa milele. Ni Siku ya Kanisa kwa sababu waamini wanakusanyika kuadhimisha Liturujia ya Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu, tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Dominika ni siku ya binadamu kwa sababu, hii inapaswa kuwa ni siku ya mapumziko kwa walio wengi. Ni siku ya kutafakari kuhusu mambo ya nyakati! Katika mzunguko wa mwaka mzima Mama Kanisa anakunjua Fumbo la Kristo Yesu: tangu Umwilisho na kuzaliwa; hadi kupaa mbinguni, mpaka siku ya Pentekoste na kungojea kwa tumaini lenye heri kurudi kwake, ili kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Ni katika muktadha huu, Kanisa huwafungulia waamini wake utajiri na uweza wa mastahili ya Bwana wake. Kwa njia hii uwepo wa mafumbo haya unakuwapo kwa nyakati zote, ili kutoka humo waamini waweze kuchota na kujazwa neema ya wokovu. Kwa kuadhimisha katika mzunguko huo wa kila mwaka mafumbo ya Kristo Yesu, Kanisa humheshimu kwa upendo mkuu Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa; huwakumbuka watakatifu na mashahidi wa imani. Kumbe, Mama Kanisa katika vipindi mbalimbali vya Mwaka wa Kanisa na kadiri ya utaratibu wa Kimapokeo, linatimiza wajibu wake wa kuwakomaza waamini kwa njia ya matendo ya kiroho na kimwili; mafundisho, sala pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili; toba na wongofu wa ndani! Rej. SC 102 -105.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema Muziki Mtakatifu ni nyenzo ya thamani kubwa inayotumika kumsifu Mwenyezi Mungu na kuonesha furaha ya maisha mapya katika Kristo Yesu. Muziki mtakatifu ni hazina yenye thamani kubwa kwa sababu kuimba kukiungana na maneno, ni sehemu ya lazima na ya ndani ya Liturujia ya sherehe. Kuimba ni amana na utajiri mkubwa kutoka katika Maandiko Matakatifu, Mapokeo hai ya Mama Kanisa pamoja na “Magisterium ya Kanisa” yaani “Mamlaka fundishi ya Kanisa kuanzia kwa Papa Pio X wamekazia kwa dhati karama na huduma ya Muziki Mtakatifu katika Ibada ya Liturujia, kwani unafanya sala kuwa tamu zaidi na kuonesha umoja wa mioyo, unaleta heshima zaidi katika Maadhimisho Matakatifu. Muziki Mtakatifu ni kielelezo cha utukufu wa Mungu na kutakatifuzwa kwa waamini. Kuimba na kucheza Muziki Mtakatifu ni kielelezo cha sala, kinachomwezesha mwamini kufungua moyo wake kwa neema na baraka za Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Muziki mtakatifu ni kielelezo cha ushirika, ufunuo wa Kanisa na kwamba, hii ni sehemu muhimu sana ya asili ya Kanisa. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakazia wajibu wa watunga Muziki Mtakatifu, wasukumwe na roho ya Kikristo, wajione kuwa wameitwa kuustawisha Muziki Mtakatifu na kukuza hazina yake. Pia watunge melodia zinazolingana na sifa za Muziki Mtakatifu na ambao unaweza kuimbwa na waamini wote, kama sehemu yao ya ushiriki mkamilifu katika Liturujia ya Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, mtunzi wa Muziki Mtakatifu anahimizwa kufahamu na kuhifadhi amana na urithi wa Muziki wa Kanisa, akichota msukumo kutoka humo ili kutunga kazi mpya kwa ajili ya Liturujia, huku akizingatia hisia za nyakati za sasa na tamaduni mbalimbali ili kuitakasa ibada kutokana na kasoro za kimtindo, njia duni za kujieleza, pamoja na muziki na maandishi yasiyojali na yasiyoendana na utukufu wa tukio linaloadhimishwa, na hivyo kuhakikisha heshima na ubora wa namna ya uwasilishaji katika Muziki wa Liturujia.
Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, maneno yaliyomo katika nyimbo yalingane na Mafundisho ya Kanisa Katoliki, zaidi yachukuliwe hasa katika Maandiko Matakatifu, Vitabu vya Liturujia sanjari na Tasaufi ya Kanisa. Rej. SC, 121. Kanuni hii ya “lex orandi lex credendi” yaani “Sheria ya Sala ni Sheria ya imani. Baba Mtakatifu Benedikto XVI anakazia sana “Actuosa participacio” yaani “Ushiriki hai wa waamini” katika Liturujia ya Kanisa. Huu ni ushiriki hai, mkamilifu na wenye tija kwa Taifa zima la Mungu katika adhimisho la Ekaristi Takatifu. Ushiriki huu unaambatana na ufahamu mkubwa wa Fumbo linaloadhimishwa na uhusiano wake na maisha ya kila siku. Kumbe, waamini hawapaswi kushiriki Liturujia ya Kanisa kama wageni au watazamaji bubu, bali washiriki hai na kwa uchaji. Rej. Sacramentum caritas, 52. Kila mwamini anayo nafasi yake maalum katika maadhimisho ya Liturujia, kila mmoja kadiri ya hali yake na waamini wafundishwe kutenda yote kufuatana na kanuni na taratibu zilizowekwa na Mama Kanisa.
Katekesi ya Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 26 Agosti 2026 imehitimisha Katekesi na tafakari juu ya: “Sacrosanctum concilium” yaani Katiba “Juu ya Liturujia” ambayo inaelezea kanuni za jumla za marekebisho na ukuzaji wa Liturujia Takatifu; Fumbo Takatifu la Ekaristi, Sakramenti nyingine na visakramenti; Liturujia ya Vipindi; Mwaka wa Liturujia wa Kanisa, Muziki Mtakatifu; na hatimaye, ni Sanaa Takatifu na Vifaa vitakatifu. Baba Mtakatifu Leo XIV ametumia fursa hii kufafanua sababu zilizopelekea Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kufanya marekebisho makubwa katika Liturujia ya Kanisa, kwa kunogeshwa na sehemu ya Neno la Mungu kutoka katika Waraka kwa Waebrania: “Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati), ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili. Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.” Ebr 10: 8-10. Kardinali Giovanni Battista Montini, akiwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Milano anasema, “Liturujia ya Kanisa ni dhihirisho la kweli la mambo ya kimungu na ya kibinadamu kwa pamoja. Ni lugha. Kwa upande mmoja, ni chombo cha mafundisho ya kimungu, na kwa upande mwingine, ni sauti ya mazungumzo na Mungu. Ni wazi kuwa haiwezi kuacha jukumu lake la kufundisha, wala haiwezi kushindwa kuipa imani na uchaji fursa ya kujieleza kwa namna iliyo wazi na ya hiari.” Kwa kuongozwa na imani hii, Kardinali Montini baadaye ndiye aliyekuja kuwa ni Baba Mtakatifu Paulo VI alisisitiza kuwa waamini “hawawezi na hawapaswi kuendelea kuwa kimya na kutochukua hatua. Uwepo wao wa kimwili hauwezi kupatanishwa na kutokuwepo kwao kiroho.”
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican mintarafu Liturujia ya Kanisa wanasema: “Kwa sababu hiyo, Mama Kanisa anajibidisha kwa namna nyingi kusudi waamini wasihudhurie fumbo hilo la imani kama wageni au watazamaji bubu, bali waishiriki ibada takatifu kwa akili, kwa moyo na kwa matendo, wakielewa vizuri fumbo hilo kwa njia ya matendo ya kiliturujia na sala. Waamini waelimishwe katika Neno la Mungu, walishwe katika karamu ya Mwili wa Bwana; wamtolee Mungu shukrani; wakitolea hostia isiyo na doa, siyo kwa mikono ya Padre tu, bali pia pamoja naye, wajifunze kujitolea wenyewe. Tena siku kwa siku, kwa njia ya Kristo Yesu mshenga, wakamilishwe katika umoja na Mungu na kati yao, ili hatimaye Mungu awe yote katika wote.” SC, 48. Sehemu hii inabainisha lengo kuu la mabadiliko ya Liturujia ya Kanisa kadiri ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican: Yaani: Ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu kwa maneno, matendo na sala katika Liturujia. Amana na utajiri huu unabubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu na Sala na kwamba, Liturujia katika maisha na utume wa Kanisa daima imeendelea kupyaishwa kwa kusoma alama za nyakati, lakini kwa kuheshimu na kutunza amana na utajiri wa Mapokeo ya Kanisa, ili hatimaye, kufanya marekebisho katika Vitabu vya Liturujia ya Kanisa. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakaza kusema: Ili kuhakikisha kuwa wakristo wanapata wingi wa neema katika Liturujia Takatifu, watambue kwamba, ipo sehemu isiyo badilika kwa sababu imewekwa na Mungu na zipo sehemu zinazoweza kubadilika kwa kusoma alama za nyakati na inapoonekana inafaa. Katika marekebisho hayo, inabidi kuratibu matini na madhehebu ya ibada ili zioneshe kinaganaga zaidi mambo matakatifu zinayoisharisha, nao wakristo waweze kuyaelewa kwa urahisi iwezekanavyo na kuyaishi kikamilifu, kwa bidii na kama jumuiya. Rej. SC, 21. Papa Pio XII anakazia umuhimu wa kutofautisha katika Liturujia Takatifu: Sehemu isiyo badilika katika Liturujia na Sehemu inayoweza kubadilika baada ya kupitishwa na uongozi wa Kanisa.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Marekebisho ya Liturujia ya Kanisa yanyotekelezwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yanapata chimbuko lake tangu karne ya ishirini mintarafu “vuguvugu la Liturujia ya Kanisa” lililokazia pamoja na mambo mengine ushiriki mkamilifu wa waamini katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Papa Pio XII akarekebisha Mpangilio wa Maadhimisho ya Ibada za Juma Kuu mintarafu matukio halisi ya Sherehe ya Pasaka. Mtakatifu Yohane XXIII akarahisisha kanuni za Sala ya Kanisa na Misale ya Altare; Kanuni ambazo zilikuwa ni msingi wa marekebisho ya Liturujia ya Kanisa kadiri ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Ni katika muktadha huu mageuzi yaliyotekelezwa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni sehemu ya Mapokeo Hai ya Kanisa, changamoto na mwaliko wa kukataa matumizi mabaya ya mageuzi haya, maelezo kupita kiasi au kutoeleweka kwa kanuni msingi za mageuzi hayo yenyewe. Kuhusu Kanuni zitokanazo na tabia ya Kidaraja na ya Kijumuiya ya Liturujia ya Kanisa Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, matendo ya Kiliturujia ni Maadhimisho ya Kanisa, ambalo ni Sakramenti ya umoja, yaani Taifa Takatifu linalokusanywa na kuratibishwa chini ya uongozi wa Maaskofu. Kwa sababu hiyo matendo hayo ni ya mwili wote kabisa wa Kanisa, nayo hudhihirisha na kuuimarisha. Aidha kila mmoja wa wanakanisa anahusika kwa namna tofauti, kadiri ya utofauti wa daraja, wa majukumu, na wa ushiriki kiutendaji. Rej. SC, 26.
Baba Mtakatifu Leo XIV imehitimisha Katekesi na tafakari juu ya: “Sacrosanctum concilium” yaani Katiba “Juu ya Liturujia” kwa kusema kwamba, jukumu kuu la viongozi wa Kanisa pamoja na waamini katika ujumla wao ni kulinda na kukuza liturujia, huku ikizingatia kanuni za Kiliturujia inang’aa kwa unyenyekevu mtukufu na kuonesha Kanisa kuwa ni moja, takatifu, katoliki na la mitume. Liturujia ya namna hii, ni chombo cha uinjilishaji, na chombo cha neema, ambacho kupitia kwacho, waamini wanaweza kujifunza kujisadaka bila ya kujibakiza na kwa njia ya upatanishi wa Kristo Yesu, ili kukamilishwa katika umoja na Mwenyezi Mungu pamoja na wao kwa wao. Rej. SC, 48.Baba Mtakatifu Leo XIV akizungumza na makundi mbalimbali ya mahujaji yaliyohudhuria wakati wa Katekesi yake, amewataka kufungua akili na nyoyo zao wakati wa maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa na hivyo kudhihirisha kupitia ushiriki wao hai, mabadiliko ya ndani yanayobubujika kutoka katika Ibada, Ishara, Nyimbo na Vipindi vya ukimya ambavyo kwa pamoja vinafumbua uwepo hai na angavu wa Kristo Yesu. Huu ni mwaliko kwa waamini kushiriki Ibada takatifu wakiwa na ufahamu kwamba, hiki ndicho kilele cha utendaji wa Kanisa na chemchemi ya maisha na nguvu ya Kanisa na kwa njia hii, waamini wanaelekeza sifa zao zisizo na mwisho kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kujiandaa kupokea neema na baraka kwa ajili ya utakaso wao.
