Papa Leo XIV Katekesi Kuhusu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican: Sala Katika Liturujia
Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV baada ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, anaendeleza Mzunguko wa Katekesi unaojikita katika Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Usomaji Mpya wa Nyaraka zake, ili kugundua tena uzuri na umuhimu wa tukio hili la Kikanisa, Kipindi cha neema ambacho kwa hakika, Mama Kanisa amekifaidi sana katika Karne ya ishirini. Kumbe, hiki ni kipindi cha Kanisa kujikita zaidi katika Nyaraka Kuu 4 za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yaani: “Dei verbum” yaani “Ufunuo wa Kimungu”, “Sacrosanctum concilium” yaani “Juu ya Liturujia”; “Lumen gentium” yaani “Fumbo la Kanisa” pamoja na “Gaudium et spes” yaani “Kanisa katika ulimwengu mamboleo.” Katiba ya “Sacrosanctum concilium” yaani “Juu ya Liturujia” inaelezea kanuni za jumla za marekebisho na ukuzaji wa Liturujia Takatifu; Fumbo Takatifu la Ekaristi, Sakramenti nyingine na visakramenti; Liturujia ya Vipindi; Mwaka wa Liturujia wa Kanisa, Muziki Mtakatifu; na hatimaye, ni Sanaa Takatifu na Vifaa vitakatifu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanafafanua nafasi ya Liturujia katika fumbo la Kanisa kwa kusema kwamba, maana kwa njia ya Liturujia, hasa Sadaka takatifu ya Ekaristi, “latimizwa tendo la ukombozi wetu.” Liturujia inasaidia kikamilifu waamini waoneshe katika maisha yao na kuwadhihirishia wengine fumbo la Kristo Yesu na pia maumbile halisi ya Kanisa la kweli. Kanisa kwa undani kabisa ni la kibinadamu na pia la kimungu, linaloonekana lakini lenye mambo yasiyoonekana ndani yake, lenye bidii kubwa katika matendo na uradhi katika kutafakari, lililopo ulimwenguni lakini kama mwenye kufanya hija. Hayo yote yamo ili yale ya kibinadamu ndani yake yaelekezwe kwa yale ya kimungu, yaonekanayo kwa yasiyoonekana, matendo kwenye kutafakari, yaliyopo yaelekee mji ujao tunakoelekea.
Katekesi ya Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 5 Agosti 2026 Kuhusu Waraka wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican: “Sacrosanctum concilium” yaani “Juu ya Liturujia” amechambua kuhusu: “Sala ya Kanisa Katika Liturujia” kwa kunogeshwa na sehemu ya Neno la Mungu kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso usemao: “kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote; pia na kwa ajili yangu mimi, nipewe usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya Injili.” Efe 6:18-19. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, tangu siku ile ya kwanza baada ya Roho Mtakatifu kuwashukia na kukaa na waamini wa Kanisa la Mwanzo, katika kila shughuli walizofanya, Roho Mtakatifu aliwafundisha kudumu katika sala na ndivyo ilivyokuwa hata kwa Jumuiya ya kwanza ya Waamini iliyozaliwa mjini Yerusalemu, baada ya Pasaka ya Bwana, daima ilikusanyika kuadhimisha Fumbo la Pasaka kwa kusali na kutafakari yale mambo yaliyomhusu Kristo Yesu. Katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, waamini walimshangilia Kristo Yesu aliyeshinda dhambi na mauti na kumshukuru Mungu kwa sababu ya kipawa chake wasichoweza kukisifu ipasavyo katika Kristo Yesu kwa sifa ya utukufu wake na kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Rej. SC. 6.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, katika nyakati hizi ndani ya muktadha unaotawaliwa na mawazo ya ufanisi na matumizi ya kawaida, sala inaweza kuonekana kuwa ni jambo ambalo halina maana. Na katika ulimwengu mamboleo ambapo sayansi na teknolojia zinadai kutoa majibu yote, sala inaweza kuonekana kama aina ya kukimbia uhalisia wa maisha. Inasikitisha kuona kwamba, sala katika familia nyingi za Kikristo imepoteza mvuto, kiasi hata cha kuchanganya sala na mbinu nyingine za kisaikolojia, kwa kuleta ustawi na mafao ya mtu binafsi. Lakini, ikumbukwe kwamba, sala ni kipimo cha msingi cha ubinadamu, kwa hiyo inastahili kupyaishwa tena ili kuirejesha katika ukweli wake wa asili. Ndiyo maana Mtakatifu Paulo VI alipokuwa anapitisha Katiba hii “Juu ya Liturujia” alisikika akisema kwamba, Mwenyezi Mungu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na kwamba, sala ni wajibu msingi kwa waamini wote na kwamba, Liturujia ya Kanisa ni chemchemi ya maisha ya Kimungu na shule ya kwanza ya maisha ya kiroho. Katika mageuzi yaliyofanywa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walikazia kwa namna ya pekee kabisa ushiriki mkamilifu wa waamini katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa.
Liturujia ni mahali muafaka pa waamini kukutana na Mwenyezi Mungu, aliyeonesha ukaribu na mwanadamu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, akatiwa mafuta kwa Roho Mtakatifu ili awahubirie maskini Habari Njema ya Wokovu, awagange na kuwaponya wale waliovunjika na kupondeka moyo. Kimsingi Liturujia ya Vipindi ni tendo la Kristo Yesu na la Kanisa lake. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vaticana wanasema, kwa kweli ni sala ya Kristo Yesu ambaye, pamoja na Fumbo la Mwili wake yaani Kanisa, humwomba Baba. Rej. SC. 84. Ni katika muktadha huu, Mtakatifu Paulo VI alitamani kuona kwamba, Liturujia ya Vipindi inaunganishwa na Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili kuwarutubisha waamini katika maisha yao ya kiroho. Huu ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, Sala ya Kanisa inamwilishwa katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku na katika jumuiya za waamini. Ni mahali ambapo waamini wanajifunza kusali, lakini zaidi kwa wakatekumeni, Sala ya Kanisa inaweza kuwa ni safari ya kujifunza Sala za Kanisa.
Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, maadhimisho ya Sala za Kanisa na Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya maisha na utume wa Kanisa na kwamba, Kristo Yesu anaunganisha naye jumuiya ya wanadamu wote mpaka washiriki naye katika kuinua wimbo huo wa Kimungu na wa sifa. Rej. SC, ili siku moja, waamini waweze kushirikishwa kikamilifu katika Fumbo la Pasaka kwa kufanana na Kristo Yesu. Mtakatifu Augustino anasema: "Tunapozungumza na Mungu katika sala, hatupaswi kumtenganisha Mwana naye; na mwili wa Mwana unapoomba, haupaswi kujitenga na Kichwa chake; hivyo, yeye ndiye Mwokozi yuleyule wa mwili wake, Bwana wetu Yesu Kristo, Mwana wa Mungu ambaye anatuombea, anaomba ndani yetu, na ambaye tunamwomba. Anatuombea kama Kuhani wetu; anaomba ndani yetu kama Kichwa chetu; tunamwomba kama Mungu wetu. Basi, na tutambue sauti yetu ndani yake, na sauti yake ndani yetu" (Enarr. in psalmum LXXXV: PL 37, 1081). Mintarafu maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ambayo hueneza mwanga wake, Sala za Kanisa hutakatifuza muda wa maisha ya waamini kila siku; asubuhi kwa kuanza siku kwa imani na moyo wa shukrani; Adhuhuri, waamini wanaomba nguvu ya kubaki waaminifu katika shughuli zao; Jioni wanapomaliza kazi, wanasali Sala ya Jioni “Vespers” inayoambatana na kuzama kwa jua. Usiku waamini wanalala huku wakijikabidhi kwa amani ya Mwenyezi Mungu. Mtakatifu Augustino anasema, kila saa ni tendo la matumaini katika safari yao ya hapa duniani, wanakesha wakingoja pamoja na Kanisa zima kurudi kwa Kristo Yesu katika utukufu wake.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika salam zake kwa makundi mbalimbali yaliyohudhuria Katekesi yake, amewataka waamini kudumu katika uaminifu wanapotekeleza dhamana, wajibu na majukumu, daima wakijiaminisha kwa Kristo Yesu. Vijana, wagonjwa na wanandoa wapya wajiimarishe katika katika fadhila ya matumaini, huku wakijizamisha na kujiachilia mikononi mwa Kristo Yesu ambaye kwa njia ya sadaka yake ya upendo, amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kwa waamini kutoka nchini Poland wanaofanya hija ya maisha ya kiroho kuelekea kwenye Madhabahu ya Bikira Maria ya Yasna Gòra (Yasina Gura), huku wakisindikizwa na Parokia zao katika hija, sala za pamoja kama sehemu ya mchakato wa kukutana na kuzungumza na Bikira Maria, awasaidie kuimarisha imani na matumaini katika familia na jumuiya zao. Baba Mtakatifu Leo XIV ametumia fursa hii kwa ajili ya kuombea amani sehemu mbalimbali za dunia, pamoja na miito mitakatifu ndani ya Kanisa, Waamini wamwombe Bikira Maria awaimarishe katika sala, kwa kumpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza. Kipindi hiki cha Likizo ya kiangazi, kiwe ni fursa ya kuyatakatifuza malimwengu kwa Neno la Mungu, Maisha ya Sala na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Waamini wajitafutie nafasi ya kukutana na jirani zao, ili kujenga na kudumisha udugu na mshikamano wa kibinadamu.
