Hija ya 4 ya Kitume ya Papa Leo XIV Hispania: Muhtasari Wake!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mkataba wa Makubaliano kati ya Marekani na Iran unaolenga kukomesha vita huko Mashariki ya Kati, unatarajiwa kutiwa saini siku ya Ijumaa tarehe 19 Juni 2026 huko Burgenstock nchini Uswisi na kwamba, Mlango wa Bahari wa Hormuz utafunguliwa siku hiyo na meli zitaanza safari huku bei ya nishati ya mafuta ikianza kushuka kwa haraka. Vizuizi vya Marekani katika Bandari ya Iran vimeanza kuondolewa. Baba Mtakatifu Leo XIV akizungumza na waandishi wa habari huko kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, anasema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa hatua hii ya makubaliano kati ya Marekani na Iran, ingawa bado kuna mambo ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi. Kabla ya kukimbilia mtutu wa bunduki, viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa hawana budi kuanza kwa kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, makubaliano haya yatakomesha vita huko Mashariki ya Kati, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za nyuklia kwa ajili ya vita ni kinyume cha maadili na utu wema. Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Matumizi ya Silaha za Nyuklia, TPNW unalenga kujenga mazingira ya usalama, amani na utulivu bila ya kuwa na hofu ya mashambulizi ya silaha za maangamizi. Amani ya kweli inajengwa kwa njia ya majadiliano na mshikamano! Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, umefika wakati wa kufutilia mbali matumizi ya silaha za nyuklia, kwa kutafuta ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; Jumuiya ya Kimataifa itafute mbinu za kutatua matatizo na changamoto zake katika masuala ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 6 hadi 12 Juni 2026 amefanya Hija ya 4 ya Kitume nchini Hispania kwa kunogeshwa na kauli mbiu: "Alzad la mirada" Yaani "Inueni macho yenu.” Yn 4:35.” Baba Mtakatifu akizungumza na waandishi wa Habari kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo amewashukuru na kuwapongeza watu wa Mungu nchini Hispania kwa maandalizi makubwa, ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu na kwamba, hija hii ya kitume imekuwa ni chemchemi ya furaha kwa watu wa Mungu nchini Hispania. Amesema, Hispania inapitia katika hali ngumu na tete kisiasa kutokana na mpasuko uliopo, mwaliko ni kwa wanasiasa nchini Hispania kujikita katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili hatimaye kufikia muafaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani katika miaka ya hivi karibuni pamoja na kuibuka kwa misimamo mikali ya kisiasa inayofumbatwa katika utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; ubaguzi na chuki dhidi ya wageni ni kati ya changamoto zinazoendelea kutishia mpango mkakati wa Kanisa katika huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Kuna baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaotaka umaarufu wa kisiasa kwa kuonesha ubabe dhidi ya wakimbizi na wahamiaji. Kanisa Katoliki katika sera na mikakati yake kuhusu huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na wale wanaotafuta hifadhi ya kisiasa linapenda kukazia kwa namna ya pekee umuhimu wa: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi. Wakimbizi na wahamiaji ni baraka kwa Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Ni kielelezo cha umoja, ukatoliki wa Kanisa na ushuhuda wa utume wa Kanisa, na kwamba, wanaweza kuwa ni chachu ya utakatifu wa maisha; urafiki na kama sehemu ya majadiliano ya kidini na kiekumene yanayofumbatwa katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji.
Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa hija yake kitume huko kwenye Visiwa vya “Grand Canaria na Tenerife alizungumzia tema hii kwa kina na mapana. Ameyabanisha hayo tena mintarafu Mkataba wa Wahamiaji na Wakimbizi ambao kimsingi ni vifungu vya sheria zinazosimamia uhamiaji na kuanzisha mfumo wa pamoja wa hifadhi katika ngazi ya Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, ambao unatoa matokeo kwa kuzingatia kanuni maadili ya Ulaya. Hizi ni Sheria ambazo zimepyaishwa na kuimarishwa kwa kuzingatia sera muhimu za Umoja wa Ulaya, EU kuhusu: Uhamiaji, hifadhi, ulinzi na usimamizi wa mipaka na ushirikiano. Haki ya wakimbizi na wahamiaji, unyambulifu wa kushughulikia changamoto hususan zinazowakabili wakimbizi na wahamiaji pamoja na ulinzi wao. Mkataba huu mpya umeanza kutumika tarehe 12 Juni 2026 na kwamba, Mkataba ulipitishwa kunako mwaka 2024 na hivyo kurekebisha pamoja na kupyaisha jinsi ya Umoja wa Ulaya unavyopaswa kusimamia mipaka yake, kushughulikia maombi ya hifadhi; ugawanaji na uwajibikaji wa nchi wanachama katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji.
Mababa wa Mataguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema Kanisa ni Sakramenti ya wokovu na ni chombo cha upatanisho, umoja na mshikamano wa Kitaifa na Kimataifa. Jumuiya ya Mapadre wa Mtakatifu Pio X (kwa Kilatini: Fraternitas Sacerdotalis Sancti Pii X - FSSPX), “The Priestly Society of Saint Pius X (SSPX)” ilianzishwa na Askofu Marcel Lefebvre kunako mwaka 1970. Jumuiya hii inajulikana kwa kusimamia Mapokeo ya Kikatoliki, kuheshimu Ibada Misa Takatifu katika lugha ya Kilatini, na kukataa mabadiliko yaliyoletwa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Kumekuwepo na juhudi za makusudi za kutaka kuirudisha Jumuiya ya Mapadre wa Mtakatifu Pio X katika ushirika kamili na Kanisa Katoliki, tangu wakati wa uongozi wa Baba Mtakatifu Benedikto XVI, hadi wakati huu wa uongozi wa Baba Mtakatifu Leo XIV, juhudi zote hizi bado zinagonga mwamba na kwamba, Jumuiya imetanga mpango mkakati wa kuwaweka wakfu mapadre wanne kuwa Maaskofu, tarehe 1 Julai 2026 bila idhini ya Khalifa wa Mtakatifu Petro ambaye kwa wakati huu yuko katika nafsi ya Baba Mtakatifu Leo XIV huko Écône, nchini Uswissi. Kitendo hiki kitapelekea Jumuiya hii kujitenga moja kwa moja na Kanisa Katoliki na hivyo kuzidisha kinzani na mivutano ya miaka mingi. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Kanisa Katoliki linapania kutoa angalisho jingine tena, na kama Jumuiya hii ikilikataa, Kanisa litabidi kusonga mbele na maamuzi yake.
Maandiko Matakatifu yanasema, Mwenyezi Mungu baada ya kukamilisha kazi yake ya uumbaji alijipatia siku ya mapumziko, changamoto kwa binadamu kufurahia siku za likizo na mapumziko, ili kupata nafasi ya kutafakari na kujiwekea sera na mikakati kwa siku za usoni. Lakini kutokana na uchu wa mali na faida ya haraka haraka, leo hii binadamu amegeuzwa kuwa ni mtumwa wa kazi na wala hana hata wakati wa kujipumzisha. Ikumbukwe kwamba, Kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu, kumbe, inapaswa kuwa na uhusiano na sehemu nyingine za maisha ya binadamu. Likizo iwe ni fursa ya kuendeleza utamaduni, ari na moyo wa sala katika maisha. Kiwe ni kipindi cha kupyaisha na kunogesha maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili! Likizo ni nafasi muafaka ya kujenga, kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya dhati na Mwenyezi Mungu, kwa kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu, lakini zaidi kwa kuongozwa na Amri Kumi za Mungu kama dira na mwongozo wa maisha. Ni nafasi ya kutafakari kuhusu Fumbo la maisha ya binadamu, ili kubainisha ikiwa kama maisha yana alama na chapa ya uwepo endelevu na angavu wa Mwenyezi Mungu, ambaye kamwe hachoki kuwaongoza waja wake katika mapito ya maisha. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Likizo ya Kipindi cha Kiangazi, atakitumia kwa ajili ya: Mapumziko, Kusali, Kujisomea na Kujiandaa kwa ajili ya maisha na utume wake kwa siku za mbeleni. Ameonesha nia ya kutembelea nchini Mexico na Perù, ambako kama mmisionari ameishi na kufanya kazi huko kwa takribani miaka ishirini lakini bado mipango inaendelea kufanyika!
Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 6 hadi 12 Juni 2026 amefanya Hija ya 4 ya Kitume nchini Hispania kwa kunogeshwa na kauli mbiu: "Alzad la mirada" Yaani "Inueni macho yenu.” Yn 4:35.” Wakari wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 17 Juni 2026, Baba Mtakatifu ametoa muhtasari wa hija yake ya kitume nchini Hispania kwa kunogeshwa na sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Yohane 4:35.38. “Hamsemi ninyi, Bado miezi minne, ndipo yaja mavuno? Tazama, mimi nawaambieni, Inueni macho yenu myatazame mashamba, ya kuwa yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno… Mimi naliwatuma myavune yale msiyoyataabikia; wengine walitaabika, nanyi mmeingia katika taabu yao.” Baba Mtakatifu anasema, alipata nafasi ya kutembelea Madrid, Abasia ya Montserrat pamoja na visiwa vya “Gran Canarie.” Baada ya kufanya hija yake ya kitume Barani Afrika, akiwa Barani Ulaya Baba Mtakatifu Leo XIV amekutana na bahari ya watu wa Mungu, waliomtia shime kama Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwa upande wake akawatia moyo kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu na kwamba, waamini wamempokea Baba Mtakatifu kwa furaha kubwa, ari na moyo mkuu, wakiwa tayari kumsikiliza na kwamba, anawashukuru watu wa Mungu katika ujumla wake. Watu wa Mungu wameonesha na kushuhudia furaha ya Injili na kwamba, amewahasa kuvuka kinzani na migawanyiko na badala yake, wajikite katika ujenzi wa ushirika unaosimikwa katika majadiliano na umoja katika tofauti zao msingi. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, leo hii imani haina budi kutangazwa, kushuhudiwa na kutamadunishwa kwani huu ni mchakato wa uinjilishaji wa tamaduni na utamadunisho wa Injili unaoiwezesha Habari Njema ya Kristo Yesu kuingia na kupenyeza mizizi yake katika tamaduni mbalimbali, ikiikubali, ikiisafisha, na kuipatia maana mpya bila kuharibu utambulisho wa watu huku wakiendelea kujikita katika kutafut ukweli na kuzima kiu ya haki na amani.
Kanisa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Mtumishi wa Mungu Antoni Gaudì Cornet alipofariki dunia. Kazi yake inayojulikana zaidi ni Kanisa la Malipizi ya Dhambi la “Sagrada Familia.” Antonio Gaudí Cornet, aliyezaliwa tarehe 25 Juni 1852, pengine huko Reus, alikubali kusimamia ujenzi wa Kanisa hili mwaka mmoja mara baada ya kuwekwa kwa jiwe la msingi, kunako mwaka 1883, akiwa na umri wa miaka 31. Tangu wakati huo na kuendelea, alijisadaka maisha yake yote kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa hili, Nyumba ya Ibada, ambapo alionesha ujuzi wake wa kisanii, hisia zake za maisha ya kiroho na kidini. Kanisa hili kubwa limebuniwa kama safari ya kiroho inayosimulia maisha, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Jiwe la msingi liliwekwa rasmi tarehe 19 Machi 1882 na kutabarukiwa na Baba Mtakatifu Benedikto XVI mwaka 2010 na kwamba, ujenzi wa Kanisa hili bado unaendelea, ili kuwakumbusha waamini kwamba, maisha ya Kikristo ni safari endelevu kama sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Mungu. Kanisa la Malipizi ya Dhambi la “Sagrada Familia” ni kielelezo cha umoja, amani na utulivu; Nyumba ya Mungu, mahali pa sala kwa wadhambi, Msalaba unakuwa ni ufunuo wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu. Kanisa hili ni kielelezo cha mkutano kati ya Mambo ya Kale na Mambo mapya, kielelezo cha mafumbo ya Kanisa. Hii ni amana na utajiri unaopaswa kutunzwa na kulindwa na kuendelea kuwekeza katika kukabiliana na changamoto mamboleo za ujenzi wa: wa haki na amani; Ikolojia endelevu na maendeleo fungamani ya binadamu; kwa kuheshimu na kuthamini: utu, haki msingi za binadamu; ustawi na maendeleo ya wengi. Hizi ni changamoto zilizoibuliwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na kufanyiwa kazi na viongozi wa Kanisa tangu wakati huo hadi nyakati hizi.
Waraka wa kwanza wa Kitume wa Baba Mtakatifu Leo XIV: “Magnifica humanitas” yaani: “Utu wa kupendeza" Juu ya Hifadhi ya Mwanadamu Katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde” kwa kifupi “MH” umezinduliwa rasmi tarehe 25 Mei 2026, Kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa. Katika Waraka huu wa Kitume, Baba Mtakatifu Leo XIV anazungumzia kuhusu: Mtazamo thabiti wa uaminifu kwa Injili; misingi na kanuni za Mafundisho Jamii ya Kanisa; Teknolojia na utawala. Ukuu wa ubinadamu katika nuru ya ahadi za teknolojia ya akili unde; Kulinda utu wa binadamu wakati wa mabadiliko: na hatimaye ni kuhusu: Ukweli, kazi, uhuru; utamaduni wa nguvu na ustaarabu wa upendo. Mwishoni mwa Waraka wake wa Kitume, Baba Mtakatifu Leo XIV anapendekeza programu ya maisha ya Kikristo inayosimikwa katika kiasi, lakini inayohitaji nguvu ya kuweza kukabili mabadiliko ya teknolojia wakati wowote kwa mwanga wa Injili. Njia hii inawezekana kwa waamini kutafakari mpango wa Mungu katika maisha yao, kwa kujenga na kudumisha umoja na ushirika wa Kikanisa kwa ushiriki mkamilifu katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu sanjari na kujikita katika ujenzi wa Ulimwengu unaozingatia wema wa wote na kuendelea kusali katika umoja na Bikira Maria Mama wa Kanisa. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini kujenga utamaduni wa kusikiliza na hatimaye, kumwilisha Injili ya matumaini, kuishuhudia katika uhalisia wa maisha na hatimaye, kutambua nyuso za maskini, dhaifu na waathirika wa nyanyaso za kijinsia, wafungwa bila kuwasahau vijana wa kizazi kipya; wakimbizi na wahamiaji; wote hawa wanapaswa kusikilizwa kwa makini.
Kwenye Visiwa vya “Gran Canarie,” Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, amekutana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, wanaolazimishwa kuzikimbia nchi zao kutokana na hali ngumu ya maisha, umaskini, athari za mabadiliko ya tabianchi, biashara ya binadamu na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo na kwamba, wengi wao ni wale wanaotoka Barani Afrika, changamoto na mwaliko kwa waamini kuisoma Injili ya matumaini katika Ulimwengu mamboleo, kwa kubadilishana tajiriba, uzoefu na mang’amuzi ya maisha; kwa kuheshimu na kuthamini asili na tamaduni za watu kwani huu ndio amana na utajiri wa ujumbe wa Kristo Yesu, mwaliko kwa watu wa Mungu kuendeleza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, ili kujenga ari na mwamko wa udugu wa kibinadamu, hali inayohitaji utashi na msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili kwa pamoja waweze kutembea katika upendo wa kiraia.
Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 6 hadi 12 Juni 2026 amefanya Hija ya 4 ya Kitume nchini Hispania kwa kunogeshwa na kauli mbiu: "Alzad la mirada" Yaani "Inueni macho yenu.” Yn 4:35.” Haya ni maneno ya Kristo Yesu mwenyewe kwa wanafunzi wake wa kwanza alipokuwa anawafundisha kuwaangalia watu na umati mkubwa wa watu uliokuwa na kiu ya kumwilisha Injili ya uhai, ukweli na utimilifu wa maisha. Baba Mtakatifu Leo XIV anakiri kwamba, maneno haya yameugusa undani wa maisha yake wakati wa Hija ya Kitume nchini Hispania. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuinua macho yao mbinguni, Wajifunze kutoka kwa Kristo Yesu wa kuwatazama majirani zao na watu wengine kwa jicho la Kimungu, yaani katika upendo, kwa kuwaheshimu na kuwathamini pamoja na kuwahurumia. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru na kuwapongeza wale wote walioshiriki katika sala ili kuifanikisha hija hii ya kitume kwa kiwango cha hali ya juu kabisa. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anazishukuru Jumuiya za watawa wa ndani nchini Hispania. Waamini waendelee kusali ili kwa maombezi na tunza ya Bikira Maria, mbegu ya imani, matumaini na mapendo iliyopandwa nchini Hispania iweze kuzaa matunda mengi ya ajabu.
