Papa Leo XIV: Kristo Yesu Ni Chemchemi na Kiini Cha Matumaini Yetu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Makanisa yamefunga tayari Malango ya Jubilei ya Matumaini, kama hitimisho la Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Lakini Kristo Yesu ni Lango la Matumaini kwa waja wake, ataendelea kubaki akiwa anaambatana na watu wake, ni Lango linalowapeleka watu wa Mungu katika maisha ya Kimungu. Mtoto aliyezaliwa ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, anayekuja kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko uletao maisha na uzima wa milele. Kristo Yesu anakuja kuganga na kuponya madonda yanayo mwandama mwanadamu na kwa wale waliovunjika na kupondeka nyoyo wanapata amani na utulivu wa ndani. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema katika maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana tarehe 6 Januari 2025 Lango la Maadhimisho ya Jubilei ya Matumaini kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican linafungwa rasmi. Pango la Noeli ni mchakato unaojikita katika kueneza na kurithisha imani katika hatua mbalimbali za maisha na utume wa Kristo Yesu. Huu ni mwaliko wa kutafakari, kuhisi na kuonja uwepo angavu na endelevu wa Mungu kwa binadamu; kuhisi na kuonja uwepo angavu wa Mungu kati pamoja na waja wake.
Pango la Noeli ni mahali ambapo panaonesha alipozaliwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, alama hai ya Injili, mwaliko wa kutafakari Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipofanyika mwanadamu, ili kukutana na watu wote, kuwaonjesha huruma na upendo wake na hatimaye, waweze kuunganika pamoja naye. Fumbo la Umwilisho ni kiini cha matumaini ya Kikristo kama anavyosema Mwinjili Yohane katika Dibaji ya Injili yake: “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.” Yn 1:14. Matumaini ya Kikristo ni mchakato ambao Mwenyezi Mungu ameamua kuufanya pamoja na binadamu kwa kutemba pamoja naye, kwani kwa njia ya Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili, Mwenyezi Mungu ameamua kukaa pamoja na binadamu na kwamba, ameamua kwa daima kuwa ni “Mungu pamoja nasi.”
Kristo Yesu ameamua kuja kukaa katika unyonge na udhaifu wa binadamu, changamoto na mwaliko kwa mwanadamu kumwelekea Mwenyezi Mungu na binadamu katika maisha yake. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, tarehe 4 Januari 2026, Dominika ya Pili ya Kipindi cha Noeli, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Mwanadamu anapaswa kumwelekea Mungu kwa sababu, amemua kukaa pamoja na binadamu dhaifu, changamoto na mwaliko wa kuanza kumtazama Kristo Yesu na hivyo kutoruhusu mawazo yao kuzagaa kwenye ombwe. Huu ni mwaliko kwa waamini kuchunguza tasaufi na kuangalia jinsi wanavyotangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu; Imani ambayo inamwilishwa kwa jinsi ya kufikiri, kusali, kumtangaza na kumshuhudia Mungu anayekuja kwa waja wake kwa njia ya Kristo Yesu. Huyu ni Mungu ambaye amekuwa jirani na anaishi katika ardhi hii dhaifu na anaendelea kujionesha kwa sura ya jirani zao na hivyo kujionesha katika hali mbalimbali kila kukicha.
Baba Mtakatifu Leo XIV anaendelea kusema, kwa ubinadamu, ahadi ya waamini lazime iwe thabiti na sawa. Ikiwa Mwenyezi Mungu alifanyika kuwa sawa na binadamu, kumbe mwanadamu ni mfano wake, hubeba ndani mwake mfano wake, huifadhi cheche za mwanga wake; na huu ni mwaliko kwa kila mtu kutambua ndani ya kila mtu hadhi isiyoweza kuharibika na hivyo kuwafanya kujikita katika nchakato wa wao kupendana. Ni katika muktadha huu, Fumbo la Umwilisho linawataka waamini kujizatiti zaidi katika kukuza na kudumisha: Udugu wa kibinadamu na ushirika ili kwamba, mshikamano uwe kigezo cha mahusiano ya kibinadamu, kwa ajili ya haki na amani, kwa ajili ya kuwatunza na kuwatetea wanyonge zaidi. Mwenyezi Mungu alifanyika mwili, kwa hivyo hakuna ibada ya kweli kwa Mwenyezi Mungu bila kujali: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema wakati huu wa furaha ya Sherehe za Noeli, iwatie moyo kuendelea na safari yao, huku wakimwomba Bikira Maria awasaidie kuwaweka tayari kumtumikia Mungu na jirani zao.