Papa Leo XIV: Epifania ya Bwana: Dhahabu, Uvumba na Manemane
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Sherehe ya Tokeo la Bwana, “Epifania ya Bwana” inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Januari, ni ufunuo wa Kristo Yesu kama Masiha wa Israeli, Mwana wa Mungu na Mwokozi wa Ulimwengu; ni Nuru na Mwanga wa Mataifa; chemchemi ya furaha na matumaini kwa watu wa Mungu; Anayewaweka huru na kuwakomboa. Mamajusi wanawakilisha dini za mazingira ya kipagani. Injili inaonesha matunda ya kwanza ya watu wa Mataifa wanaopokea Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho. Mamajusi: Gaspari, Melkiori na Baltazari ni Mamajusi, yaani Watu wenye busara kutoka Mashariki ambapo baada ya kuiona nyota na kwamba Bwana amezaliwa, walienda Yerusalemu kumwabudu. Wanaonesha ile kiu ya watu wa Mataifa kutafuta kwa Israeli mwanga wa Masiha kwa nyota ya Daudi atakayekuwa Mfalme wa Mataifa. Kumbe, Epifania ni Sherehe ya Mwanga na Mwanga huo ni Kristo Yesu; mwanga unaoangaza. Mwangaza huo umewaangaza watu wote na unaendelea kuangaza. Hii ni Sherehe ya mafumbo ya Utoto wa Kristo Yesu – KKK 528. Hiki ni kielelezo cha watu wa Mataifa wanaotaka kumwabudu, kumsujudia na kumwamini kama Mwana wa Mungu na Mwokozi wa Ulimwengu. Rej. KKK 528. Mamajusi walipomwona Mtoto Yesu pamoja na Mariamu Mama yake, wakaanguka na kumsujudia, wakamtolea tunu: Dhahabu, Uvumba na Manemane. Zawadi walizochukua zilipatikana huko kwao. Rej Yer 6:20.
Sherehe ya Tokeo la Bwana inaviashilia vingi vinavyogusa undani wa maisha na utume wa Kristo Yesu hapa duniani: yaani: dhahabu, uvumba na manemane. Dhahabu ni madini yenye thamani kubwa yaliyokuwa ni sehemu ya wasifu na mapambo ya Wafalme katika Agano la Kale. Zawadi ya dhahabu inayotolewa na Mamajusi ni kuungama Ufalme wa Kristo, aliyezaliwa katika mazingira duni. Huyu si Mfalme kadiri ya mwono wa kibinadamu, bali Yeye ni Mfalme wa: Kweli na uzima; Utakatifu na neema; Haki, upendo na amani. Ni Mfalme wa uhai, matendo mema na anayeongoza historia ya maisha ya mwanadamu.
Uvumba ni kielelezo cha sadaka inayompendeza Mungu, changamoto kwa waamini kutolea harufu nzuri ya ushuhuda wa maisha yao; kwa kujikita katika ufuasi uliotukuka, uthabiti katika imani, matumaini na mapendo. Manemane ni mafuta ya gharama kubwa, yaliyokuwa na hafuru nzuri. Ni mafuta kadiri ya Injili waliyotumia wale wanawake wachamungu walipojihimu asubuhi na mapema siku ya kwanza ya Juma, kwenda kuupaka mwili wa Yesu ili usiharibike. Tendo hili na zawadi ya manemane iliyotolewa na Mamajuzi ni kielelezo cha Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Kumbe kwa njia ya Mamajusi kutoka Mashariki, Kanisa lina mtambua Kristo Yesu kuwa ni: Mfalme, Kuhani na Mkombozi wa mwanadamu. Katika Maadhimisho ya Sherehe ya Epifania yaani Tokeo la Bwana, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Januari, Mama Kanisa pia anaadhimisha Siku ya Utoto Mtakatifu, iliyoanzishwa na Papa Pius XII, kunako mwaka 1950, aliyetaka waamini kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi na makuzi ya watoto wao kama Kristo Yesu, alivyowapatia nafasi ya pekee, katika maisha na utume wake. Huu ni ukweli unaomshirikisha mwanadamu.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika tafakari yake kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Sherehe ya Epifania, tarehe 6 Januari 2026 anasema: Dhahabu, Uvumba na Manemane ni tunu zinazowafikirisha sana waamini hasa baada ya kufunga Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo, umuhimu wa kujitoa na kujisadaka kama alivyofanya yule Mwanamke mjane, Rej Lk 21:1-4 na kama wanavyoshuhudia Mamajusi kutoka Mashariki. Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yamewakumbusha waamini juu ya uadilifu unaokita mizizi yake kwenye ukarimu; changamoto na wito wa kupanga upya kuishi kwa pamoja; kugawana ardhi na rasilimali za dunia katika haki na usawa sanjari na "kile tulichonacho" na "tulivyo" mintarafu ndoto za Mungu, ambazo ni kubwa zaidi kuliko ndoto za binadamu!Huu ni mwaliko wa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini inayokita katika maisha ya watu wa Mungu, hapa duniani; Injili ya matumaini inayotoka mbinguni, lakini inazalisha duniani historia mpya. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema katika karama na zawadi kutoka kwa Mamajusi wa Mashariki, kila mwamini anaweza kuangalia kile anachoweza kushirikisha, ili Kristo Yesu aendelee kukua kati ya waja wake na Ufalme wake uweze kutamalaki, kwa kuhakikisha kwamba, Neno lake linamwilishwa katika maisha ya watu sehemu mbalimbali za dunia: Maadui wanapatana na hivyo kuwa ndugu wamoja; mahali ambapo kuna ukosefu wa haki na usawa; unakuwa ni uwanja wa kujenga na kudumisha usawa; viwanda vinavyozalisha silaha sehemu mbalimbali za dunia, vinageuzwa kuwa ni kwa ajili ya ujenzi wa haki na amani duniani. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuwa ni vyombo na wajenzi wa amani kwa njia tofauti. Rej Mt 2:12.