Papa Leo XIV: Mtakatifu Stefano Shuhuda wa Kristo Na Kanisa Lake
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika tafakari yake, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican anasema, Tarehe 26 Desemba ya kila mwaka ni "siku ya kuzaliwa, natus in caelo" kwa Mtakatifu Stefano Shahidi, kama vizazi vya kwanza vya Wakristo walivyokuwa wakisema. Kuuawa kwa misingi ya imani ni kuzaliwa mbinguni: mtazamo wa imani, kwa kweli, hauoni tena giza tu hata katika kifo. Mtakatifu Stefano Shemasi Shahidi ni shuhuda wa kwanza kuyamimina maisha yake kwa ajili ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni kati ya Mashemasi saba waliochaguliwa na Mitume wa Yesu kwa ajili ya huduma kwa Jumuiya ya Wakristo wa kwanza. Utume ambao aliutekeleza kwa muda mfupi sana ikilinganishwa na matumaini ya Mitume wa Yesu. Mtakatifu Stefano alikuwa ni mwema, mwenye kujawa na Roho, na hekima. Alitenda maajabu na ishara, kisha akafungwa. Akabahatika kuwa ni shuhuda wa Yesu pamoja na kupewa neema ya kutafakari utukufu wa Kristo Mfufuka, kiasi hata cha kutangaza Umungu wake. Kabla ya kifo chake, akajiaminisha kwa huruma na upendo wa Kristo Yesu. Katika mateso makali akathubutu kuwasamehe watesi wake, mbele ya Kristo Yesu ili asiwahesabie dhambi hii, akiisha kusema haya akalala usingizi wa amani. Liturujia ya Neno la Mungu inajikita zaidi katika hatua ya mwisho mwisho wa maisha ya Mtakatifu Stefano, alipokamatwa na kupelekwa mbele ya baraza na huko akafunguliwa mashitaka ya uongo juu ya kufuru kwa mahali patakatifu na juu ya torati. Simulizi katika Matendo ya Mitume linashuhudia kwamba wale waliomwona Stefano akitembea kuelekea kuuawa kwa imani walistaajabishwa na nuru iliyokuwa usoni mwake na maneno yake. “Watu wote walioketi katika ile baraza wakamkazia macho yao, wakamwona uso wake kuwa kama uso wa malaika.” Mdo 6:15. Huu ni uso wa mtu anayekikabili kifo kwa upendo na kwamba, maisha yake yote yaliakisi upendo wa Kimungu uliofunuliwa ndani ya Kristo Yesu, Nuru ya Mataifa inayoangazia giza la maisha ya waamini. Katika muktadha wa Sherehe ya Noeli, kwa baadhi ya watu Siku kuu ya Mtakatifu Stefano, Shahidi inaweza kuonekana kuwa hapa si mahali pake. Lakini mwamini akizama zaidi, atagundua kwamba, hapa ni kiini cha maana ya kweli ya Sherehe ya Noeli.
Hapa ni mahali ambapo mauaji ya kikatili yanashindwa na upendo; Injili ya uhai inapeta zaidi kuliko utamaduni wa kifo na kwamba, huu ni ushuhuda wa hali ya juu kabisa unaomwezesha Mtakatifu Stefano kumtafakari Kristo Mfufuka na hatimaye, kuwa na ujasiri wa kuweza kuwasamehe watesi wake. Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, kuzaliwa kwa Kristo Yesu Mwana wa Baba wa milele, ni mwaliko kwa waamini kuwa ni watoto wa Mungu kama ilivyokuwa wakati wa kuzaliwa kwa mtoto Yesu kwa kujikita katika fadhila ya unyenyekevu kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, kwa Mtakatifu Yosefu na wachungaji kule mjini Bethlehemu, lakini uzuri wa Yesu na wa wale wanaoishi kama Yeye ni uzuri uliokataliwa. Huu ni mvuto mkali kama sumaku na unachochea mwitikio wa wale wanaoogopa nguvu zao wenyewe, kwa wale ambao ukosefu wao wa haki unafichuliwa na wema unaofunua mawazo ya nyoyo za. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, hakuna nguvu, hata hivyo, hadi sasa, inayoweza kushinda kazi ya Mungu. Popote duniani wapo wanaochagua haki hata ikiwagharimu, ni watu wanaotanguliza amani mbele ya hofu zao, wanaojisadaka katika kutoa huduma kwa maskini kuliko nafsi zao na hapa unachukua ni mwanzo wa kuchipua kwa fadhila ya matumaini, hali inayoleta maana ya kusherehekea Noeli. Kwenye Ulimwengu mamboleo kuna watu wanaoteseka na wala hawana uhakika wa maisha yao na kwamba shangwe ingeonekana kuwa ni jambo lisilo wezekana. Wale wanaoamini katika amani leo na wamechagua njia isiyo na silaha ya Yesu na wafia dini mara nyingi hudhihakiwa, na kusukumwa nje ya mazungumzo ya hadhara, na mara nyingi hushutumiwa kuwapendelea wapinzani na maadui.
Wakristo, hata hivyo, anasema Baba Mtakatifu Leo XIV, hawana adui, bali ndugu ambao hubaki hivyo hata wanapoelewana vibaya. Fumbo la Noeli ni chemchemi ya furaha, ile furaha inayochochewa na ukakamavu wa wale ambao tayari wanaishi katika undugu wa shikamano wa kibinadamu, wa wale ambao tayari wanatambua karibu nao, yupo Kristo Yesu hata katika adui zao, hadhi isiyofutika ya mwana wa Mungu. Hii ndiyo sababu Stefano alikufa akiwa anatoa msamaha, kama Kristo Yesu: kwa nguvu ya kweli kuliko ile ya silaha. Ni nguvu isiyo na kifani, ambayo tayari iko katika moyo wa kila mtu, ambayo huwashwa tena na kuwasilishwa kwa njia isiyozuilika wakati mtu anapoanza kumtazama jirani yake kwa njia tofauti, ili kutoa umakini na utambuzi. Ndiyo, hii inazaliwa upya, hii inakuja kwenye nuru tena, hii ni ndiyo Noeli ya waamini. Stefano, Shahidi kijana na mhudumu wa Injili alikua amejaa Roho Mtakatifu, akafanikiwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu ambaye alitimiza ahadi yake kwa wafuasi wake, kwa kumpatia nguvu ya Roho Mtakatifu ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kati ya watu walioombewa na Stefano alikuwepo pia kijana Sauli aliyeona na kushuhudia vyema kuuawa kwake. Lakini baadaye kwa njia ya neema ya Mungu, Sauli akatubu na kumwongokea Mungu, akageuka kuwa ni Mtume na Mwalimu wa Mataifa; mmisionari aliyejisadaka bila ya kujibakiza kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sehemu mbalimbali za dunia. Mtakatifu Paulo amezaliwa upya kwa neema ya Mungu na kwa njia ya ushuhuda wa msamaha wa Mtakatifu Stefano Shemasi na Shahidi, kiasi kwamba, amekuwa ni mbegu ya toba na wongofu wake.
Huu ni ushuhuda kwamba, matendo ya huruma na mapendo, ni cheche zinazoweza kuleta mageuzi makubwa katika historia ya maisha ya mwanadamu. Haya ni mambo ambayo yamefichika katika uhalisia wa maisha ya kawaida. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Mwenyezi Mungu anaongoza historia ya ulimwengu kwa njia ya ujasiri wenye unyenyekevu wa watu wanaosali, wanaopenda na kusamahe. Hawa ndio watakatifu ambao ni majirani wa kila siku, wanaoshuhudia wema na huruma ya Mungu kwa njia ya matendo yao yanayogeuza historia ya ulimwengu. Baba Mtakatifu Leo XIV amehitimisha tafakari yake kuhusu Mtakatifu Stefano Shahidi kwa kutoa mwaliko kwa waamini kumwomba Bikira Maria, anayetafakari, mwanamke aliyebarikiwa kuliko wanawake wote wanaohudumia maisha, wanaopinga kiburi na kukita maisha yao juu ya imani dhidi ya hali ya kutoaminiana. Bikira Maria awaongoze waamini katika furaha yake mwenyewe, furaha ambayo huondoa kila hofu na tishio la maisha, kama theluji inavyoyeyuka kwenye jua.