Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana: Ufunuo wa Haki, Huruma, Upendo na Wokovu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kristo Yesu aliyaanza maisha yake ya hadhara kwa kukubali kubatizwa na Yohane Mbatizaji mtoni Yordani. Huu ni ubatizo wa toba iletayo ondoleo la dhambi. Anakubali kushikamana na mwanadamu katika hali halisi ya maisha yake na yote anayoyapitia ili aongozane naye polepole kuiinua hali yake duni aifikishe katika hadhi ya kimungu. Hii ni Sikukuu ya Epifania, yaani tokeo la Kristo Yesu kama: Masiha na Mwana wa Mungu aliye hai, tayari kuanza utume wake kama mtumishi anayeteseka. Anakubali ahesabike miongoni mwa wenye dhambi kwani Kristo Yesu ndiye Mwana kondoo wa Mungu anayechukua dhambi ya ulimwengu anatanguliza Ubatizo wa kifo cha kumwaga damu, ili kutimiza haki zote, kwa utii mkamilifu na kutekeleza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni. Anapokea kwa mapendo ubatizo wa kifo kwa ajili ya maondoleo ya dhambi. Rej. KKK 535-537; 1217-1239, Ubatizo wa Bwana ni Sikukuu inayowakumbusha waamini ubatizo wao, yaani mwanzo wa safari ya ukombozi kwa njia ya imani katika Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Sakramenti ya Ubatizo inamwingiza mwamini katika taifa jipya la Mungu ili kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka, baada ya kutakaswa kwa Maji ya Ubatizo yanayoponya na kuwapatia uzima wa milele. Kwa Maji ya Ubatizo, Kristo Yesu analitakasa na kulisafisha Kanisa lake kwa maji na katika Neno apate kuliletea Kanisa lake utukufu na utakatifu.
Ubatizo ni Sakramenti ya Pasaka na wokovu katika Fumbo la kufa na kufufuka kwake Kristo Yesu na hivyo kuwafanya kuwa ni watoto wa Mungu, kwa kuzaliwa kwa: Maji na Roho Mtakatifu na hivyo waamini wanaingizwa na kuwa ni sehemu ya jamaa ya watu wa Mungu, changamoto ni kujitahidi kuishi kama wana wa Mungu kwa kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka na kwa sababu hiyo Wakristo wanaunganishwa na Kristo Yesu na kuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Yesu, yaani, Kanisa na hivyo kushiriki: Ukuhani, Ufalme na Unabii wa Kristo Yesu. Ubatizo ni Sakramenti ya Imani. Kumbe, Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana Mtoni Yordani imesheheni utajiri na amana kubwa, kwani, Sikukuu hii inafunga sherehe za Noeli na kuanza kutembea katika Mwaka A wa Kanisa. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, Dominika tarehe 8 Januari 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amekazia kuhusu: Ubatizo wa Bwana unaofunua haki ya Mungu inayokita mizizi yake katika huruma, upendo na wokovu wa watu wote. Kwa njia ya Ubatizo, Kristo Yesu anafunua utume wake unaowahamasisha watu wa Mungu kuwa ni vyombo vya huruma, upendo na haki. Mwinjili Mathayo 3: 1-17 anaelezea Ubatizo uletea toba na maondoleo ya dhambi.
Ni katika hali hii, Kristo Yesu naye akamwendea Yohane Mbatizaji katika hali ya unyenyekevu na moyo safi, ili aweze kubatizwa pia. Tendo hili lilimshangaza sana Yohane Mbatizaji na alitakiwa kufanya hivyo ili kutimiza haki yote. Ubatizo wa Kristo Yesu mtoni Yordani ukafunua haki ya Mungu inayosimikwa katika huruma na upendo, tayari kumwinua tena binadamu mdhambi anayeelemewa na udhaifu wake wa kibinadamu. Hii ni haki ipatikanayo kwa kumwamini Kristo Yesu, kwa sababu haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii, ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Kristo Yesu kwa wote wanao mwamini. Rej. Rum 3: 22-31. Kwa njia ya Ubatizo Mtoni Yordani, Kristo Yesu amewafunulia watu wa Mataifa maana ya utume wake hapa ulimwenguni, wokovu wa wadhambi, kwa kubeba dhambi zao mabegani mwake kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake uletao wokovu na maisha ya uzima wa milele. Haki ya Mungu ni huruma na upendo wake unaoponya na kuokoa; upendo unaoonesha ushuhuda wa mshikamano na binadamu mdhambi, ili kumwondoa katika giza la dhambi. Kwa njia ya Kristo Yesu, Mwenyezi Mungu anasema Hayati Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anataka kumwokoa kila mtu, ili hatimaye, aweze kuuona mwanga. Huu ni mwaliko kwa Wakristo kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki ya Mungu kwa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa haki na amani; upendo na mshikamano wa dhati, kwa kusaidiana na kuchukuliana mizigo. Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, ndiye aliyemzaa Kristo Yesu, Nuru ya Mataifa, akazama katika udhaifu wa binadamu, ili kumwokoa na kumkirimia maisha mapya.