Papa Francisko Ujumbe wa Urbi Et Orbi, Noeli 2022: Amani Duniani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Salam na Baraka kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” zilianza kutolewa kwa mara ya kwanza na Mtakatifu Paulo VI kunako mwaka 1974. Kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii, ujumbe huu unawafikia watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia kwa njia ya mfumo wa matangazo yanayorushwa kwa njia ya satellite saba. Baba Mtakatifu Francisko katika Salam na Baraka zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” wakati wa maadhimisho ya Sherehe za Noeli tarehe 25 Desemba 2022 alikuwa ameambatana na Kardinali James Michael Harvey, Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo Nje ya Kuta za Roma pamoja na Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu. Baba Mtakatifu Francisko katika Salam na Baraka zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, “Urbi et Orbi” amegusia kuhusu: Kristo Yesu, Nuru ya Mataifa, “kwa Kiebrania: עִמָּנוּאֵל, Immanuel, yaani, "Mungu pamoja nasi.” Ni Noeli ya Amani, lakini walimwengu wanaendelea kuishi katika janga la ukosefu wa amani, watu wanapekenyuliwa na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha kutokana na biashara haramu ya silaha duniani. Noeli ya Kristo Yesu iwe ni kielelezo cha upendo na mshikamano, ishara ya huruma, upendo na unyenyekevu wa Mungu katika historia ya maisha ya mwanadamu.
Baba Mtakatifu katika Salam zake amewatakia watu heri na baraka za Sherehe ya Noeli, Ili Kristo Yesu aliyezaliwa na Bikira Maria awakirimie watu wote upendo wa Mungu, chemchemi ya imani na matumaini. Mtoto Yesu awajalie amani kama ilivyotangazwa na Malaika “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia” Lk 2:14. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuinua macho yao mbinguni ili kumtaza Mtoto Yesu aliyezaliwa katika Hori ya kulishia wanyama, kwa sababu wazazi wake hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni. Katika hali ya unyenyekevu na kimya kikuu, Kristo Yesu Nuru halisi ya ulimwengu, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Huyu ndiye Emmanueli yaani Mungu pamoja nasi aliyethubutu kuzaliwa kati pamoja na maskini na anaendelea kubisha hodi katika nyoyo za waamini, ili apate kuingia na kupata joto la upendo na hifadhi. Kristo Yesu ndiye kiini cha Sherehe ya Noeli. Ni Mwana wa Mungu aliyezaliwa kwa ajili yetu! Kristo Yesu ni amani ya watu wake, inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kimsingi hii ni Noeli ya Bwana, Noeli ya Amani. “Natalis Domini, Natalisi est pacis”. Kristo Yesu ni njia pia ya amani.
Kristo Yesu, kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, mateso, kifo na ufufuko wake, amewafungulia walimwengu njia huru itakatowawezesha walimwengu kuishi katika udugu wa kibinadamu na katika amani njia ambayo watu wa Mungu wanapaswa kuifuata na wala si katika giza la uadui, vita na kinzani, changamoto ni kuuvua utu wa kale na kuanza kutembea kwa kufuata nyayo za Kristo. Ni mwaliko kwa kumkubali na kumpokea Mtoto Yesu kinyume cha Mfalme Herode na maafisa wake walioshindwa kumtambua na matokeo yake wakaendelea kumezwa na uchu wa mali na madaraka; kiburi na unafiki, mambo yaliyofunga nyoyo zao kiasi cha kushindwa kwenda Bethlehemu kumwona Mtoto Yesu aliyekuwa amezaliwa. Walimwengu wamepewa Mfalme wa amani, lakini bado upepo wa vita na kinzani unaendelea kuvuma sehemu mbalimbali za dunia. Sherehe ya kuzaliwa kwa Kristo Yesu ni Sherehe ya amani, mwaliko kwa waamini kumwangalia Mtoto Yesu, ili kuwa na ujasiri wa kutambua watoto kutoka sehemu mbalimbali za dunia wanaolilia amani. Iwe ni fursa ya kuangalia nyuso za watu wa Mungu kutoka Ukraine wanaosherehekea Noeli ya Bwana wakiwa wamezungukwa na mashambulizi ya vita, giza nene kutokana na ukosefu wa nishati ya umeme na uharibifu mkubwa. Waamini wawe mstari wa mbele kuonesha mshikamano wa udugu wa kibinadamu; wenye nguvu na mamlaka, wasaidie kuhakikisha kwamba, mtutu wa bunduki unazima. Lakini kwa bahati mbaya hakuna anayeweza kusikiliza kilio cha watoto.
Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, watu wanapekenyuliwa kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha kutokana na biashara haramu ya silaha duniani. Hii ndiyo hali halisi ilivyo nchini Siria na Nchi Takatifu ambako watu wanaendelea kupoteza maisha kutokana na mapambano ya silaha. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusali kwa ajili ya kuombea amani na majadiliano ya kweli kati ya Israeli na Palestina, ili watu wote wa Mungu katika nchi hizi mbili waweze kuishi kidugu, wakiheshimiana na kuthamiana hata katika tofauti zao msingi za Kiimani. Mtoto Yesu awasaidie watu wa Mungu nchini Lebanon ili kwa msaada wa Jumuiya ya Kimataifa, udugu wa kibinadamu na mshikamano wa upendo, waweze kupata suluhu ya matatizo na changamoto zinazowaandama kwa sasa. Nuru ya Kristo iwaangazie watu wa Mungu wanaoishi katika Ukanda wa Saheli, ambako kwa sasa ukanda huu umegeuka kuwa ni uwanja wa fujo, ili hatimaye, maridhiano kati ya watu wenye tamaduni na mapokeo mbalimbali waweze kuishi kwa amani na upendo. Yemen na Myanmar zijielekeze katika majadiliano na upatanisho wa kitaifa na Iran, isitishe umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia. Watu wa Amerika wajielekeze katika ujenzi wa haki, amani na maridhiano kwa kujikita katika sera na mikakati ya kisiasa inayokidhi mahitaji msingi ya watu mahalia. Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee, amewakumbuka na kuwaombea watu wa Mungu nchini Haiti wanaoendelea kuteseka sana kutokana na hali tete ya maisha nchini humo.
Kristo Yesu alizaliwa mjini Bethlehemu “Bethlehem (/ˈbɛθlɪhɛm/; Kiarabu: بيت لحم Bayt Laḥm; Kiebrania: בֵּית לֶחֶם Bet Leḥem” maana yake “Nyumba ya mkate.” Baba Mtakatifu Francisko ameyaelekeza mawazo yake kwa watu wanaosiginwa na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha sehemu mbalimbali za dunia, wakati kuna sehemu nyingine za dunia, watu wanakula na kusaza! Kwa namna ya pekee kabisa Baba Mtakatifu amezikumbuka nchi za Afghanstan na Nchi zilizoko kwenye Pwani ya Pembe ya Afrika, ambazo zimeathirika sana kutokana na ukame wa kutisha. Haya ni matokeo ya vita yanayopelekea kushuka kwa shughuli za kilimo na uzalishaji wa chakula. Watu wa Mataifa, lakini zaidi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa wajifunze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki na kwamba, chakula kisiwe ni silaha ya vita, bali chombo cha kukoleza amani. Katika furaha ya Sherehe ya Noeli, Baba Mtakatifu amezikumbuka familia zote ambazo zimeathirika kutokana na vita sehemu mbalimbali ya dunia, athari za myumbo wa uchumi Kitaifa na Kimataifa, kiasi cha kukosa fursa za ajira pamoja na mahitaji msingi. Kristo Yesu, Nuru ya Mataifa, awaangazie watu ili waondokane na ubinafsi, uchoyo pamoja na kutowajali wengine, hasa wakimbizi na wahamiaji, wanaotafuta hifadhi na mahitaji yao msingi. Kamwe maskini, wagonjwa, watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, wasisahaulike, watambulike kama watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, licha ya kasoro na matatizo yanayowasonga kila kukicha!
Bethlehemu ni kielelezo cha ukuu, unyenyekevu na utakatifu wa Mungu ambao ulifichwa kwa wenye hekima na akili, bali ukafunuliwa kwa watoto wachanga. Rej. Mt 11: 25. Huu ni mwaliko hata kwa waamini kwenda kwa haraka kama ilivyokuwa kwa wale wachungaji walioishi makondeni, ili kushangaa tukio la Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu kufanyika mwili kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Mwana wa Mungu ambaye ni chemchemi ya wema na utakatifu wote, amejifanya kuwa maskini, kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu, Yeye ni upendo wa Mungu, mwaliko kwa waamini kufuata nyayo zake, ili kuweza kushiriki kikamilifu katika utukufu wake.