Papa Francisko: Gereza Katika Maisha na Utume wa Yohane Mbatizaji: Huruma ya Mungu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa katika maisha na utume wake kwa wafungwa magerezani anakazia hasa: Umuhimu wa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wafungwa magerezani, kwa kutambua kwamba, wafungwa na askari magereza ni vyombo na mashuhuda wa Injili. Askari magereza wawe na ujasiri wanapotekeleza dhamana na utume wao miongoni mwa wafungwa. Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza askari magereza kila wakati wanapotekeleza dhamana na utume wao kwa ajili ya ulinzi na usalama kwa maskini na wanyonge zaidi katika jamii, yaani wafungwa, ili kuhakikisha kwamba, haki, amani, ulinzi na usalama vinatawala ndani ya jamii. Hii ni dhamana inayowataka siku kwa siku kuwa ni wajenzi wa haki na wajumbe wa amani kwa kuwakumbuka wafungwa hao waliofungwa kana kwamba, wamefungwa pamoja nao na kama wanadhulumiwa, basi hata wao wahisi haya madhulumu mwilini wao. Maisha ya gerezani ni magumu na mara nyingine yanaweza kukatisha tamaa, kwa mfungwa kuelemewa na upweke hasi, hali ya kukata tamaa na hatimaye kushindwa kuona hatima ya maisha yake. Gereza ni mahali pa mahangaiko ya binadamu. Askari magereza wanatumia muda mrefu kuwa magerezani, ili kulinda na kudumisha ulinzi na usalama, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinalindwa barabara.
Askari magereza wawe ni walinzi wa ndugu zao wafungwa, wawe ni madaraja kati ya magereza na jamii katika ujumla wake kwa kuonesha upendo unaowawajibisha, ili kuondoa wasiwasi na kashfa ya kutowajali wengine. Baba Mtakatifu anawataka askari magereza kutambua uzito wa kazi na wajibu wao kwa wafungwa pamoja na familia zao wenyewe. Kumbe, inawapasa kusaidiana na kushikamana ili kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa zinazopatikana kutokana na kazi na utume wao. Tarehe 11 Desemba 2022 Mama Kanisa anaadhimisha “Domenica Gaudete” maana yake “Dominika ya furaha” kwani wokovu wa mwanadamu umekaribia. Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amegusia kuhusu: Sifa kuu za Masiha na Mkombozi anajaye; Maana ya Gereza katika maisha na utume wa Yohane Mbatizaji; Gereza na utupu wa maisha ya ndani, mwaliko kwa waamini katika kipindi hiki cha Majilio kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu, ili aendelee kuwashangaza kwa huruma, ili hatimaye, wao pia wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya Tatu ya Kipindi cha Majilio Mwaka A wa Kanisa, inawatafakarisha kuhusu swali la Yohane Mbatizaji na ushuhuda uliotolewa na Kristo Yesu, kwa kuonesha sifa kuu za Masiha wanayemngoja. Yohane Mbatizaji alidhani kwamba, Masiha anayekuja atakuwa mkali na wakutisha, angetekeleza haki kwa mkono wenye nguvu, akiwashikisha adabu wadhambi, lakini mambo yakaenda kinyume kabisa cha matarajio yake. Kiini cha ujumbe wa Kristo Yesu kama Masiha ni huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani kwa wote, watu wakasikia na kuona kwamba “vipofu wanapata kuona, viwete wanakwenda, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema.” Mt 11:5. Ni vyema kutambua kwamba, wakati huu Yohane Mbatizaji alikuwa amefungwa gerezani. Gereza kama eneo na gereza kama hali ya maisha ya undani wa mtu anayetembea katika giza na utupu wa maisha ya ndani, kiasi hata cha kushindwa kutambua ukweli.
Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Yohane Mbatizaji, akiwa gerezani alishindwa kumtambua Kristo Yesu, Masiha waliyekuwa wanamngojea, kiasi cha kutumbukia katika giza na kushindwa kuutambua ukweli, kiasi cha kuthubutu kuwatuma wanafunzi wake wakamuulize. Lakini, hili ni jambo la kushangaza sana kwani Yohane Mbatizaji ni Nabii aliyefunga Agano la Kale, akawa daraja ya Agano Jipya, aliyemwandalia njia na hatimaye, wakati ulipowadia akamtambulisha Kristo Yesu kuwa ni Masiha, Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu. Rej Yn 1:29. Baada ya Kristo Yesu kubatizwa mtoni Yordani, Roho Mtakatifu akamshukia Kristo Yesu na mara sauti kutoka mbinguni ikasikika ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa wangu msikieni yeye”, alama ambayo Yohane Mbatizaji alikuwa akiisubiria na kwamba, Kristo Yesu ni Masiha wa Bwana. Yohane Mbatizaji ndiye aliyemtambulisha kuwa Kristo Yesu ndiye Mwana kondoo wa Mungu na wale wanafunzi wa kwanza wa Yohane Mbatizaji wakawa ni wafuasi wa kwanza wa Yesu! Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Mwenyezi Mungu anaendelea kujifunua kwa waja wake taratibu na ndiyo maana Yohane Mbatizaji aliendelea kukua na kukomaa katika maisha yake ya ndani, mwaliko wa toba na wongofu wa ndani ili hatimaye, kutambua Uso wa kweli wa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo.
Kristo Yesu mwenyewe anakiri kwa kusema “Amini, nawaambieni: Hajaondokea mtu katika wazao wa wanawake aliye mkuu kuliko Yohane Mbatizaji; walakini aliye mdogo katika Ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko yeye.” Mt 11: 11. Huu ni mwaliko wa kuendelea kumwongokea Mungu ili kumfahamu zaidi badala ya kumfungia katika mipango ya kibinadamu. Baba Mtakatifu Francisko amegusia pia kuhusu gereza na utupu wa maisha ya kiroho, kiasi cha kushindwa kuona upya wa maisha unaotangazwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu, kwa kudhani kwamba, tayari watu wanafahamu yote kumhusu Kristo Yesu. Wakati mwingine, waamini wanapicha tenge kumhusu Mungu na kusahau kwamba, Mwenyezi Mungu amejifunua kuwa ni mwingi wa huruma, mapendo na msamaha; anaheshimu na kuthamini uhuru wa watoto wake; mwaliko na changamoto kwa waamini kujifunika fadhila ya unyenyekevu katika maisha. Kipindi cha Majilio, iwe ni fursa ya kumwachia Mwenyezi Mungu aendelee kuwashangaza waja wake, kwa kuwafunulia ukuu na utukufu wake, unaofumbatwa katika unyenyekevu. Waamini wamtambue Mwenyezi Mungu anayekuja kukaa kwao. Maadhimisho ya Noeli, iwe ni fursa kwa waamini kuwa ni vyombo vya huruma na faraja kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kama alivyofanya Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, awashike na kuwasindikiza watoto wake katika kipindi hiki cha maandalizi ya Sherehe ya Noeli, ili waweze kutambua ukuu na utukufu wa Mungu anayekuja kuwakomboa watu wake kwa njia ya Mtoto Yesu.