Tafuta

Papa Leo XIV Katekesi Kuhusu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican: Kanisa Linalosafiri

Katekesi ya Papa Leo XIV imechota amana na utajiri wake kutoka katika ile Sura ya Saba Mwanga wa Mataifa: Tabia ya Kieskatolojia ya Kanisa linalosafiri na Umoja wa Kanisa lililo mbinguni, humu ndimo waamini wanapata utakatifu kwa neema ya Mungu na utimilifu wake katika Kristo Yesu. Hili ni Kanisa linalosafiri katika Sakramenti na taasisi zake zilizo za wakati huu, linachukua sura ya ulimwengu huu unaopita na linaishi kati ya viumbe ambavyo vinaugua na vina utungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipitisha Katiba ya Fumbo la Kanisa, “Lumen gentium” yaani “Mwanga wa Mataifa” tarehe 21 Novemba 1964. Hii ni Katiba inayozungumzia kuhusu: Fumbo la Kanisa na Kanisa kama Sakramenti katika Kristo Yesu, Kanisa kama Taifa la Mungu; Muundo wa Kihierarkia wa Kanisa na hasa Uaskofu; Waamini walei; Wito wa watu wote katika Kanisa kuwa watakatifu; Watawa; Tabia ya kieskatolojia ya Kanisa linalosafiri na umoja wa Kanisa lililo mbinguni; Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa katika Fumbo la Kristo Yesu na la Kanisa. Katekesi ya Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 6 Mei 2026 imenogeshwa na sehemu ya Maandiko Matakatifu inayolionesha Kanisa mithili ya wateuliwa: “Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-Kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao; wakilia kwa sauti kuu wakisema, Wokovu una Mungu wetu aketiye katika kiti cha enzi, na Mwana-Kondoo.” Ufu 7:9-10. Katekesi hii imechota amana na utajiri wake kutoka katika ile Sura ya Saba: Tabia ya Kieskatolojia ya Kanisa linalosafiri na Umoja wa Kanisa lililo mbinguni, humu ndimo waamini wanapata utakatifu kwa neema ya Mungu na utimilifu wake katika Kristo Yesu. Hili ni Kanisa linalosafiri katika Sakramenti na taasisi zake zilizo za wakati huu, linachukua sura ya ulimwengu huu unaopita na linaishi kati ya viumbe ambavyo vinaugua na vina utungu hata sasa na vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu. Rej. Rum 8:19-22. Kanisa ni watu wa Mungu wanaosafiri katika historia wanaotenda kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu na kwamba, linapata chanzo na asili yake kutoka kwa Kristo Yesu aliyetangaza kuhusu Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika kweli na uzima; ni ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Rej. LG 9, 5.

Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu
Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu   (@Vatican Media)

Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu kwa watu wote na linaishi katika historia kwa njia ya huduma ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu, kwa kuadhimisha Sakramenti za Kanisa, lakini kwa namna ya pekee sana Sakramenti ya Ekaristi Takatifu inayoimarisha uhusiano wa upendo na kwamba, wokovu ni zawadi ya Mungu inayotolewa na Roho Mtakatifu kwa watu wote hata nje ya mipaka yake inayoonekana kwa macho! Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, kwa mateso, kifo, ufufuko pamoja na kumtuma Roho wake Mtakatifu amelifanya Fumbo la Mwili wake, ulio Kanisa kuwa ni Sakramenti ya Wokovu kwa watu wote; alama na chombo cha utimilifu wa maisha na amani kama ahadi kutoka kwa Mungu na kwamba, utimilifu wake utafikiwa mwishoni mwa dunia. Wakristo wanaosafiri huku bondeni kwenye machozi, wanaendelea kukomaa katika kutenda mema, wakati mwingine kwa uwepo wa ukosefu wa haki pamoja na mahangaiko, bila kukata tamaa, bali kwa kuishi huku wakiwa na mwelekeo wa mbingu na dunia mpya ambamo haki yakaa ndani mwake. Kumbe, Kanisa linatekeleza utume wake kama mwanzo na utimilifu wa ahadi na ujenzi wa Ufalme wa Mungu katika Kristo Yesu. Mama Kanisa ni mlinzi wa tumaini linaloangazia njia, kwa kusimama kidete kukataa kitu kinacho hatarisha maisha na hivyo kukwazimisha maendeleo yake; kwa kuendelea kushikamana na maskini, wale wanaonyonywa, waathirika wa vurugu na vita, bila kuwasahau watu wanaoteseka kiroho na kimwili. Rej. Mkusanyiko wa Mafundisho Jamii Kuhusu Kanisa, 159.

Kanisa ni watu wanaosafiri katika historia na wakati
Kanisa ni watu wanaosafiri katika historia na wakati   (@Vatican Media)

Kanisa kama Ishara na Sakramenti ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu ni hujaji anayesoma na kufasiri mienendo ya historia kutoka katika mwanga wa Injili, akikemea maovu kwa namna zote na kutangaza, kwa maneno na matendo, wokovu ambao Kristo Yesu anataka kuleta kwa ajili ya wanadamu wote na hivyo kusimika Ufalme wake wa haki, upendo na amani. Kila kitu katika maisha na utume wa Kanisa kinapaswa kuelekezwa katika wokovu kwa njia ya Kristo. Kwa mtazamo huu, Kanisa linaitwa kukiri kwa unyenyekevu udhaifu wa kibinadamu na mpito wa taasisi zake, ambazo, wakati zikiutumikia ujenzi wa Ufalme wa Mungu, zinabeba sura ya muda ya ulimwengu huu. Rej. LG, 48. Kwa vile taasisi za Kikanisa zinaishi katika historia na wakati, zinaitwa na kuhimizwa kujikita mara kwa mara katika toba na wongofu wa ndani, kwa kuendelea kupyaisha miundo na mahusiano yao ili waweze kuendana kweli na utume wao. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, umoja wa wale wanaosafiri duniani na wa ndugu waliolala katika amani ya Kristo Yesu haukatiki hata kidogo, kinyume chake kadiri ya imani ya daima ya Kanisa, umoja huo huimarishwa kwa kubadilishana mema ya kiroho. Umoja huu na Kanisa la mbinguni hutimizwa kwa njia bora pale Mama Kanisa anapoadhimisha sifa ya Mungu Mwenyezi kwa shangwe moja, hasa katika Liturujia takatifu, ambamo uwezo wa Roho Mtakatifu hutenda kazi ndani ya waamini kwa ishara za Sakramenti.

Sakramenti ya Ekaristi Takatifu inaimarisha umoja na upendo
Sakramenti ya Ekaristi Takatifu inaimarisha umoja na upendo   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kwa kuwaombea wafu na kufuata nyayo zao wale ambao tayari wameishi wakiwa wanafunzi wa Kristo Yesu, waamini nao wanategemezwa katika safari ya ona hivyo kuimarisha Ibada yao kwa Mwenyezi Mungu. Waamini wakiwa wametiwa alama na Roho Mtakatifu na kuunganishwa katika Liturujia moja pamoja na wale waliotangulia katika imani, waamini wanasifu na kulitukuza Fumbo la Utatu Mtakatifu. Shukrani, ziwaendee Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kwa kuwakumbusha waamini juu ya haki hii muhimu na nzuri ya kuwa Wakristo, changamoto ni kuitafuta na kuikuza katika uhalisia wa maisha yao. Huu ni mwaliko kwa Wakristo kuwa ni mashuhuda wa haki, amani na upendo. Maombezi ya Watakatifu wa Mungu yanaimarisha na kudumisha umoja na tunu msingi za Kikristo na kwamba, Bikira Maria anang’aa duniani kama alama ya hakika ya matumaini na ya faraja kwa taifa la Mungu linalosafiri, mpaka siku ya Bwana itakapowadia. LG 68; 2Pet 3:10. Ushirika pamoja na wafu: Kanisa ndani ya washiriki wanaotembea duniani, limejengwa kwa ibada sana kumbukumbu za wafu, ili wafunguliwe dhambi na hivyo kuimarisha ushirika. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwakumbuka na kuwaombea ndugu, jamaa na marafiki zao waliotangulia mbele ya haki, wakiwa na imani juu ya Ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele.

Kanisa ni Fumbo la Mwili wa Kristo!
Kanisa ni Fumbo la Mwili wa Kristo!   (@VATICAN MEDIA)

Baba Mtakatifu Leo XIV amewakumbusha waamini na mahujaji kwamba, tarehe 6 Mei ya kila mwaka, Mama Kanisa anaadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Dominiko Savio (1842-1857) anayejulikana kama "matunda ya kwanza ya utakatifu" wa mfumo wa elimu wa Don Bosco. Kama mwanafunzi kipenzi na wa kwanza wa Oratorio ya Don Bosco huko Turin, alionesha kuwa utakatifu unawezekana katika umri mdogo sana kwa kuishi maisha ya kawaida kwa njia ya kipekee. Ni kijana aliyejiaminisha katika maongozi ya Roho Mtakatifu katika maisha yake yote, awe ni mfano na msaada wa kila mwamini katika kujibu matamanio ya wema kadiri ya Roho Mtakatifu.

Kanisa Linalo safiri

 

06 Mei 2026, 14:54

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >