Papa Leo XIV: Fumbo La Kanisa Linaloonekana Na Kanisa Lisiloonekana
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipitisha Katiba ya Fumbo la Kanisa, yaani “Mwanga wa Mataifa” “Lumen gentium” tarehe 21 Novemba 1964. Hii ni Katiba inayozungumzia kuhusu: Fumbo la Kanisa na Kanisa kama Sakramenti katika Kristo Yesu, Kanisa kama Taifa la Mungu; Muundo wa Kihierarkia wa Kanisa na hasa Uaskofu; Waamini walei; Wito wa watu wote katika Kanisa kuwa watakatifu; Watawa; Tabia ya kieskatolojia ya Kanisa linalosafiri na umoja wa Kanisa lililo mbinguni; Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa katika Fumbo la Kristo Yesu na la Kanisa. Katekesi ya Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 18 Februari 2026 ilikita ujumbe wake katika Katiba ya Fumbo la Kanisa, yaani “Mwanga wa Mataifa” “Lumen gentium”; hati inayojulikana kama “Mwanga wa Mataifa”: “Katika Kristo Kanisa ni kama Sakramenti au ishara na chombo cha kuwaunganisha watu kiundani na Mungu na kuleta umoja kati ya wanadamu wote.” LG, 1. Katekesi hii imenogeshwa na sehemu ya Neno la Mungu kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai: Kristo Yesu ni mfano wa Mungu asiyeonekana. “Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni.” Kol 1:19-20. Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa anasema, Kanisa ni Fumbo lililokuwa limefichika tangu zamani, lakini sasa limefunuliwa, kama sehemu ya mpango wa Mungu wa kuviunganisha na kuvipatanisha vitu vyote chini ya Kristo Yesu, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake uletao wokovu. Umoja huu unajionesha kwa namna ya pekee katika Maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa, mahali ambapo Mwenyezi Mungu anatukuzwa na mwanadamu anatakatifuzwa. Kristo Yesu ndiye amani ya waja wake, aliyewafanya kuwa wamoja, huku akibomoa kiambaza cha kati kilichokuwa kinawatenga. Rej. Efe 2:14.
Kwa Mtakatifu Paulo, Mtume, Fumbo hili linawahusu binadamu na hatimaye viumbe wote. Ni kwa njia ya Kristo Yesu na Roho Mtakatifu anayewezesha kuvunja nguvu ya utengano na hivyo kuwawezesha waamini kukutana ili kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa, kwa kuamini kuhusu Injili na Msalaba wa Kristo Yesu unaowavuta waamini, kushuhudia ufunuo wa Fumbo la Upendo wa Mungu kwa njia ya Kristo Yesu ndiyo maana Fumbo la Kanisa linaitwa: “Ekklesia” maana yake mkutano wa watu wanaojitambua kwamba, wameitwa kushiriki katika Fumbo la Kanisa ambalo limefunuliwa na Mwenyezi Mungu na linawashirikisha watu pamoja na viumbe vyote. Ndiyo maana Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakiri kwa kusema, “Katika Kristo Kanisa ni kama Sakramenti au ishara na chombo cha kuwaunganisha watu kiundani na Mungu na kuleta umoja kati ya wanadamu wote.” LG, 1. Mababa wa Kanisa, wakiongozwa na ufafanuzi wa Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa kanisa wanasema kwamba, Sakramenti ni "ishara zinazoonekana za neema isiyoonekana," zilizowekwa na Kristo Yesu ili kuleta utakatifu na hivyo kujenga uhusiano na Mwenyezi Mungu. Sakramenti hizi saba (Ubatizo, Kipaimara, Ekaristi, Upatanisho, Mpako Mtakatifu, Daraja, Ndoa) ni alama hai zinazotenda kile zinachomaanisha kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Kwa njia ya Kanisa kama Sakramenti ya Wokovu, Mwenyezi Mungu anawaunganisha watu wote pamoja naye na kati yao wao wenyewe.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Sura ya Saba wanafafanua kuhusu: Tabia ya Kieskatolojia ya Kanisa linalosafiri na Umoja wa Kanisa lililo mbinguni. Hili ni Kanisa linalosafiri, katika Sakramenti zake na taasisi zake na kwamba, Kristo Yesu alipoinuliwa juu aliwavuta wote kwake, akiisha kufufuka katika wafu akamtuma ndani ya wanafunzi wake Roho wake mleta uzima, na kwa njia yake akauweka Mwili wake ulio Kanisa kuwa ni Sakramenti ya wokovu kwa wote. Akikaa kuume kwa Baba, daima hutenda kazi Ulimwenguni ili awaongoze wote kwenye Kanisa na kwa njia yake awaunganishe naye zaidi, na kwa kuwalisha Mwili na Damu yake Azizi, aweze kuwashirikisha katika maisha ya utukufu wake. Rej. LG. 48. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, sehemu hii ya Mafundisho ya Mababa wa Kanisa inawasaidia waamini kuona husiano kati ya nguvu ya Roho Mtakatifu ya kuwaunganisha waamini katika Fumbo la Pasaka ya Kristo Yesu, ambayo kimsingi ni: Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu; utambulisho wa Kanisa. Waamini ni sehemu ya Fumbo la Kanisa, Mwili wa Kristo Uliofufuka na hivyo wao wanakuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo; Watu wa Mungu wanaosafiri katika historia, wanaoishi katika uwepo wa Kristo Yesu anayewatakatifuza na kuwaelekeza katika ujenzi wa umoja na upatanisho kati ya watu!
Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 4 Machi 2026 aliendelea na Katekesi yake kuhusu Katiba juu ya Fumbo la Kanisa, yaani “Mwanga wa Mataifa” “Lumen gentium” inayozungumzia: Fumbo la Kanisa na Kanisa kama Sakramenti katika Kristo Yesu, Kanisa kama Taifa la Mungu; Muundo wa Kihierarkia wa Kanisa na hasa Uaskofu; Waamini walei; Wito wa watu wote katika Kanisa kuwa watakatifu; Watawa; Tabia ya kieskatolojia ya Kanisa linalosafiri na umoja wa Kanisa lililo mbinguni; Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa katika Fumbo la Kristo Yesu na la Kanisa. Katekesi hii imenogeshwa na sehemu ya Neno la Mungu kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso isemayo: “Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo. Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo.” Efe 4: 14-16. Katekesi hii imenogeshwa na mada isemayo: Kanisa linaloonekana na lisiloonekana. Hii ni jumuiya ya imani, matumaini na mapendo, chemchemi ya neema: Linaunganisha ubinadamu na umungu na hivyo kuwa ni chombo cha wokovu chenye uhai, vivyo hivyo muundo wa kijamii wa Kanisa unamtumikia Roho wa Kristo anayeuhuisha, kwa ajili ya kuukuza mwili wake. Hii ni Jumuiya inayoshirikishana furaha na mateso, kwa kuwa ni Wakristo, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, alama ya Kristo Yesu inayowasindikiza katika safari ya maisha na kwamba, Kanisa, kimsingi kwa pamoja lina tabia ya kimungu na kibinadamu, linaonekana, lakini limejaa kweli zisizoonekana, lenye bidii katika utendaji na linalojishughulisha na kutafakari, lililomo ulimwenguni, lakini likiwa safarini kuelekea mbinguni. Rej. LG, 8; KKK 771.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema asili ya ubinadamu na umungu wa Kanisa unaliwezesha kuwakumbatia wakosefu ndani yake na wakati ule ule ni takatifu na kwamba, linahitaji kutakaswa, haliachi kamwe kutubu na kuendelea kujipyaisha, tayari kuwapeleka wakosefu kwa Mungu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema kwamba, wale wote waliobahatika kukutana na Kristo Yesu katika njia za Palestina, waliweza kuonja ubinadamu wake, wale walioamua na kuthubutu kumfuasa, waliweza kuonja huruma, upendo na ukarimu wake; wakapata baraka, wakawekwa huru na kuponywa magonjwa yao. Mitume waliomfuasa Kristo Yesu, walikuwa wanajifungulia njia ya kukutana na Mwenyezi Mungu, akawa kweli ni ufunuo hai wa Mungu anayeonekana. Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, Fumbo la Kanisa linaundwa na watu kamili, ambao wakati mwingine wanatangaza na kushuhudia uzuri wa Injili, wanaonesha uwepo wa Kristo Yesu na kazi yake ya ukombozi; kielelezo kamili cha utimilifu kati ya Injili na muundo wa Kanisa unaomwilisha Injili nyakati hizi kama alivyowahi kusema Baba Mtakatifu Benedikto XVI. Ikumbukwe kwamba, hakuna Kanisa linaloelea kwenye ombwe na katika ukamilifu; Kanisa ambalo linajitenga na dunia, bali kuna Kanisa moja la Kristo Yesu ambalo limemwilishwa katika historia. Ni katika muktadha huu, Utakatifu wa Kanisa unajionesha, kwani Kristo Yesu anaendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa njia ya udogo na udhaifu wa waja wake na kwamba, huu ndio “Mtindo wa Mungu” anayeendelea kujifunua na kutenda kwa njia ya udhaifu wa viumbe vyake.
Mama Kanisa ataendelea kuwafunda watoto wake sanaa ya kusindikiza inayowafundisha kuvua viatu mbele ya mahali patakatifu pa mtu mwingine. Rej Kut 3;5. Mwelekeo huu unawawezesha waamini hadi leo hii kushiriki katika ujenzi wa Kanisa linaloonekana sanjari na Kanisa katika ulimwengu wa kiroho kwa kukuza na kudumisha ushirika na upendo kati ya waamini. Fadhila ya upendo inaliwezesha Kanisa kumdhihirisha Kristo Mfufuka. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, upendo, kwa kweli, daima uonesha uwepo hai na angavu wa Yesu Kristo Mfufuka. Anasema Mtakatifu Augustino: "kwamba wote wanaweza kuzingatia tu upendo na kwamba upendo peke yake hushinda vitu vyote na bila upendo vitu vyote ni bure; popote unapopatikana, upendo huvuta vitu vyote kwake" (Mahubiri 354,6,6).
