Tafuta

Papa Leo XIV: Katekesi Kuhusu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Usomaji wa Nyaraka Zake

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema baada ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, kuanzia Jumatano tarehe 7 Januari 2026 anaanzisha mzunguko mpya wa Katekesi unaojikita katika Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Usomaji Mpya wa Nyaraka zake, ili kugundua tena uzuri na umuhimu wa tukio hili la Kikanisa, Kipindi cha neema ambacho Mama Kanisa amekifaidi sana katika Karne ya ishirini: Kanisa, Liturujia na Ushuhuda wa imani tendaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI anasema, Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ilikuwa ni Pentekoste mpya kwa Kanisa Katoliki, kwa kutaka kusoma alama za nyakati, kusahihisha mapungufu yake, ili hatimaye, kuliwezesha Kanisa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kumletea mwanadamu maendeleo endelevu ya: kiroho na kimwili. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, lilikuwa ni tukio la matumaini ndani ya Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, wakatambua dhamana, wajibu na changamoto iliyokuwa mbele yao, wakaamua kujadili vipengele mbalimbali na hatimaye, kuvipigia kura. Ni Mtaguso uliowakusanya viongozi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kujadili maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, chini ya uongozi na usimamizi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, wakati huo akiwa ni Mtakatifu Yohane XXIII; Ukatafsiriwa kwa vitendo na Mtakatifu Paulo VI pamoja na Mtakatifu Yohane Paulo II. Baba Mtakatifu Benedikto XVI akapyaisha mafundisho yake kwa Katekesi makini kuhusu: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha Adili na Sala. Hayati Baba Mtakatifu Francisko akaendelea kujipambanua kwa kutaka ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu ili kuchangia katika maisha na utume wa Kanisa la Kristo Yesu, kila mmoja kadiri ya karama, wito na dhamana yake ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Miaka 60 tangu kuzinduliwa kwa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican tarehe 11 Oktoba 1962, katika mahubiri yake, alikazia kuhusu: Upendo ambao Kristo Yesu ameonesha kwa Kanisa lake, licha ya dhambi, udhaifu na mapungufu ya kibinadamu na hata wakati mwingine, kumezwa na malimwengu, changamoto na mwaliko kwa Kanisa kurejea tena katika chemchemi ya upendo ule wa awali ulioneshwa na Kristo Yesu kwa Kanisa lake: Moja, takatifu, katoliki na la mitume. Hili ni Kanisa linalotumwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili inayomwilishwa katika imani tendaji. Kanisa katika upendo, unyenyekevu na sadaka, linakabidhiwa utume wa kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Kristo na wa Mungu; kutangaza Habari Njema ya Wokovu sanjari na utamadunisho, ili kushiriki: furaha na matumaini; uchungu na fadhaa ya walimwengu.

Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni tukio muhimu kwa Kanisa
Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni tukio muhimu kwa Kanisa   (Archivio Fotografico Vatican Media)

Mkazo ni ushiriki mkamilifu wa ukuhani wa waamini wote unaowawezesha kushiriki sadaka ya Ekaristi Takatifu, kwa kupokea Sakramenti za Kanisa, kwa kusali na kwa njia ya ushuhuda wa maisha matakatifu, toba, wongofu wa ndani, kwa kujikana na kwa upendo wenye utendaji; Umoja wa watu wa Mungu ukipewa kipaumbele cha kwanza. Kanisa litambue kwamba, maskini wanao upendeleo wa pekee mbele ya Mwenyezi Mungu. Kwa hakika Kanisa ni Sakramenti ya umoja inayowaunganisha watu kiundani na Mwenyezi Mungu na hivyo kuleta umoja kati ya wanadamu wote. Ni jukumu la Mama Kanisa kuendelea kujikita katika Mapokeo, sera na mikakati ya shughuli za kiuchungaji. Mwaliko wa kuendeleza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Huu pia ni ni mwaliko wa kujenga na kudumisha ushirika wa Kanisa, ili wote wawe na umoja kama Kristo Yesu alivyojisadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema baada ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, kuanzia Jumatano tarehe 7 Januari 2026 anaanzisha mzunguko mpya wa Katekesi unaojikita katika Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Usomaji Mpya wa Nyaraka zake, ili kugundua tena uzuri na umuhimu wa tukio hili la Kikanisa, Kipindi cha neema ambacho kwa hakika, Mama Kanisa amekifaidi sana katika Karne ya ishirini. Kumbe, hiki ni kipindi cha Kanisa kujikita zaidi katika Nyaraka Kuu 4 za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yaani: “Dei verbum” yaani “Ufunuo wa Kimungu”, “Sacrosanctum concilium” yaani “Juu ya Liturujia”; “Lumen gentium” yaani “Fumbo la Kanisa” pamoja na “Gaudium et spes” yaani “Kanisa katika ulimwengu mamboleo.” Katekesi hii imenogeshwa na sehemu ya Maandiko Matakatifu: “Wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia Neno la Mungu; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao. Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele. Msichukuliwe na mafundisho ya namna nyingine nyingine, na ya kigeni.” Ebr 13: 7-9.

Wadau wengi walioshiriki katika Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican hawapo tena
Wadau wengi walioshiriki katika Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican hawapo tena   (Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema kwamba, ni ukweli usioweza kufumbiwa macho kwamba, wadau wengi wa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yaani: Maaskofu, wanataalimungu na waamini walei, hawapo tena kwani wametangulia mbele za haki, wakiwa na imani na matumaini ya maisha na uzima wa milele. Huu ni mwaliko kwa Mama Kanisa kupyaisha tena Mamlaka Fundishi ya Kanisa, au "Magisterium," yanayokita mizizi yake katika: Kufafanua na Kulinda Maandiko Matakatifu; Mafundisho na Mapokeo ya Kitume, ili kuwaongoza waamini katika imani na maadili; kwa kuendelea kufafanua Neno la Mungu na hivyo kuhakikisha kwamba, Kanisa linabaki katika ukweli wa Kristo Yesu, huku, Maaskofu wakiwa wameungana pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kama alivyowahi kusema Baba Mtakatifu Benedikto XVI kwamba yanaendana na uhalisia wa watu wa nyakati hizi za utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Mtakatifu Yohane XXIII wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican tarehe 11 Oktoba 1962 alisema kwamba, Maadhimisho haya yalikuwa ni mapambazuko ya siku mpya ya Kanisa na mwanga mpya kwa Kanisa zima.

Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni tukio muhimu sana la Kikanisa
Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni tukio muhimu sana la Kikanisa   (@VATICAN MEDIA)

Ni Maadhimisho ambayo yameliwezesha Kanisa kugundua tena: Uso wa huruma na upendo wa Mungu; Mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni watoto wa Mungu; Limeuona mwanga wa Kristo Yesu, Kanisa na waamini, kama fumbo la ushirika na Sakramenti ya umoja kati ya Mungu na watu wake. Kanisa limefanya mabadiliko makubwa katika Liturujia, ili kuwawezesha waamini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Mungu. Kanisa likaweza kusoma alama za nyakati, kwa kukubali mabadiliko na changamoto zake; kwa kujikita katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kwani Kanisa linawajibika kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili; kwa kusimama kidete katika wongofu wa kitamaduni unaothamini tamaduni, mila na desturi njema za watu mahalia, matumaini na fadhaa za watu wa Mungu ili kujenga jamii inayosimikwa katika haki na udugu wa kibinadamu. Ni katika muktadha huu, Kanisa limegeuka kuwa ni: Neno, Ujumbe na chemchemi ya majadiliano kwa kujikita katika mchakato wa kutafuta na kudumisha ukweli mintarafu majadiliano ya kiekumene, kidini na kitamaduni pamoja na watu wote wenye mapenzi mema. Ni mwaliko wa kuwa na sera na mikakati makini ya shughuli za kichungaji, kuendeleza upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa kwa kusoma alama za nyakati; kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; haki na amani na kwamba, matunda ya juhudi hizi yataonekana kwa wakati wake. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican anasema Baba Mtakatifu Francisko ulitoa kipaumbele cha kwanza kwa uwapo wa Mungu, Kanisa linaloonesha upendo kwa Kristo Yesu na kwa watu wote wanaopendwa na Mungu.

Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican umekuza majadiliano, kidini na kiekumene
Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican umekuza majadiliano, kidini na kiekumene   (@Vatican Media)

Huu ni wakati wa Mama Kanisa kuwaendea walimwengu, ili kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu inayokita mizizi yake katika: Umoja kati ya Kristo Yesu na Kanisa lake; Mapokeo hai, Historia ya Mitaguso, Mababa na Walimu wa Kanisa; Watakatifu na Mashuhuda wa Imani. Hii ni changamoto ya kuwaendea walimwengu katika ulimwengu mamboleo unaogubikwa na majanga yake, uchungu na fadhaa pamoja na dhambi zake, bila kusahau: mafanikio yake makubwa, tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu, ili kuwawezesha waamini na watu wenye mapenzi mema kujikita zaidi katika ujenzi wa misingi ya haki na amani, jambo ambalo Mama Kanisa analitamani kutoka kwa walimwengu. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuziendelea Nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ili kugundua tena Unabii na Umuhimu wake; Kukumbatia Mapokeo mengi ya maisha na utume wa Kanisa; kwa kuendelea kusoma alama za nyakati, ili kupyaisha ile furaha ya kukimbia kukutana na Ulimwengu; ili kutangaza na kujenga Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika upendo, haki na amani. Askofu Stephano Lameck Musomba, OSA wa Jimbo Katoliki Bagamoyo, Tanzania anasema kuna haja kwa Mama Kanisa kuendelea kujikita katika malezi ya dhamiri nyofu; wazazi wawe karibu na watoto wao katika malezi na makuzi, ili waweze kuwarithisha mila na tamaduni njema za Kiafrika na kwamba, wazee ni amana na utajiri wa Kanisa.

Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican
07 Januari 2026, 16:23

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >