Mzunguko wa Katekesi: Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 31 Agosti 2022 alianzisha Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Utambuzi kwa kusema kwamba, hili ni tendo muhimu sana linalomwathiri kila mtu, kwa sababu kupanga ni kuchagua mambo mbalimbali katika maisha; ambayo kimsingi yanapaswa kufanywa kwa uthabiti mkubwa kwa kutambua kwamba, kuna pia mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema kuna mambo yanayopaswa kupewa uzito wa juu mintarafu utambuzi unaofanywa katika maisha ya kila siku, kwani hili ni zoezi linalohusishwa na: akili, ustadi na utashi kwa kusoma alama za nyakati na hivyo kutenda kwa busara. Utambuzi unagusia mahusiano ili kupata furaha ya kweli na hatimaye, Siku ya Mwisho, binadamu watahukumiwa kutokana na utambuzi wao kwa Mwenyezi Mungu. Utambuzi ni zoezi gumu lakini la muhimu katika maisha. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alitumia picha za maisha halisi kufafanua utambuzi wake kuhusu maisha ya wavuvi na taaluma yao: walikusanya samaki wazuri na kuwatia chomboni na wale wabaya kuwatupa baharini au mfanya biashara aliyegundua lulu ya thamani, akauza alivyo navyo vyote, ili aweze kuipata. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Utambuzi.
Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume. Rej. Mt 9:9-13. Hii ndiyo tema ya Mzunguko Mpya wa Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko kuanzia Jumatano tarehe 11 Januari 2023. Hii ni tema ya dharura na madhubuti kwa maisha ya Kikristo. “Naye Yesu alipokuwa akipita kutoka huko aliona mtu ameketi forodhani, aitwaye Mathayo, akamwambia, Nifuate. Akaondoka, akamfuata. Ikawa alipoketi nyumbani ale chakula, tazama, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuja wakaketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake. Mafarisayo walipoona, waliwaambia wanafunzi wake, Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Naye aliposikia, aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi. Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.” Mt 9: 9-13. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume ni mambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa kwa sababu, jumuiya ya waamini inazaliwa kwa sababu ya utume na umisionari, huku ikisukumwa na Roho Mtakatifu, waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.
Huu ndio mwelekeo na dira ya maisha ya Kikristo, vinginevyo, Wakristo wanaweza kujikuta wakijitafuta wao wenyewe. Bila ya kuwa na shauku ya uinjilishaji, imani itadhohofu na hatimaye, kunyauka na utume ndicho kiini cha maisha ya mwamini. Kumbe, mzunguko mpya wa katekesi ni kutaka kupyaisha shauku ya uinjilishaji kwa kuzama zaidi katika Maandiko Matakatifu sanjari na Mafundisho Tanzu ya Mama Kanisa ili kuchota amana na utajiri wa ari, mwamko na bidii ya kitume. Katika mzunguko huu wa Katekesi, Baba Mtakatifu anasema, atajitahidi kuweka mbele ya waamini mifano hai na baadhi ya mashuhuda wa imani, walioamsha shauku ya Habari Njema ya Wokovu, ili wawasaidie waamini kuwasha tena ule moto wa Roho Mtakatifu, ili hatimaye, uweze kuzijaza nyoyo za waamini wote mapendo. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu amependa kuanza mzunguko huu kwa wito wa Mathayo mtoza Ushuru kama anavyosimulia yeye mwenyewe! Rej. Mt 9: 9-13. Mwinjili Mathayo anasimulia jinsi ambavyo Kristo Yesu alivyomwangalia kwa jicho la huruma, akampenda hata kama alikuwa ni Mtoza ushuru kwa ajili ya Warumi waliokuwa wanatawala eneo la Palestina kwa wakati ule. Watu wengi wakamwona kama “Chawa” wa Serikali ya kikoloni na msaliti wa wananchi wenzake.
Kwa hakika Mathayo mtoza hakuwa na sifa njema mbele ya wananchi wenzake na kwa kweli alidhararuliwa kama soli ya kiatu! Lakini Kristo Yesu alikuwa na jicho la huruma na mapendo, akaamua kuvunjilia mbali kuta za utengano na kumkaribia Mathayo Mtoza ushuru kwani kila mtu hata katika udhaifu wake ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; anapendwa na kuthaminiwa na Mwenyezi Mungu jinsi alivyo. Jicho la huruma na upendo ni mwanzo wa shauku ya uinjilishaji, jambo la msingi ambalo hata waamini katika ulimwengu mamboleo wanapaswa kujifunza kutoka kwa Kristo Yesu kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji na ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ni changamoto kwa waamini na watu wte wenye mapenzi mema kuwa na mwelekeo na mawazo chanya kwa jirani zao na kamwe wasitake kujenga kuta za utengano na dharau kwa watu wengine. Wawaangalie kwa jicho la huruma na upendeleo wa pekee, ili kujenga mahusiano na mafungamano ya ujirani mwema kama ilivyokuwa kwa Kikristo Yesu. Kristo Yesu anasema, Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi. Mt. 9:13.
Mathayo Mtoza ushuru alipoonja huruma na upendo wa Kristo Yesu akaacha yote, akaondoka na kumfuasa Kristo Yesu na kuacha nyuma yake madaraka aliyokuwa nayo. Jambo la kwanza ambalo Kristo Yesu alilifanya ni kumwondoa Mathayo madarakani na hivyo kumwelekeza zaidi katika mwelekeo wa huduma. Huu ni mwaliko na changamoto kwa Mama Kanisa na waamini katika ujumla wao, kutobweteka wala kuridhika, lazima Mama Kanisa asimame na kuanza kutembea ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hatima ya wito na maisha ya Mathayo mtoza ushuru, kwanza kabisa ni kushirikisha furaha yake pamoja na watoza ushuru wenzake, katika nyumba na mazingira alimozoea, huku akiwa amebadilika, kwa maneno mengine, anarejea nyumbani kwake, akiwa ametubu na kumwongokea Mungu baada ya kuonja huruma na upendo wa Kristo Yesu katika maisha yake. Huu ni mwaliko kwa Wakristo wote katika hali na mazingira yao, wajibidiishe kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Habari Njema na kamwe wasisubiri kutangazwa watakatifu ndipo waanze kuhubiri na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Baada ya hapo, Mathayo mtoza ushuru alianza kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu katika mazingira na watu aliowazoea.
Wakristo wajitahidi katika maisha yao ya kila siku kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Kristo unaoganga, kuponya na kuwaokoa watu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Habari Njema ya Wokovu inatangazwa na kushuhudiwa kwa njia ya matendo adili na matakatifu na wala si wongofu wa shuruti kama alivyokaza kusema, Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI. Huu ndio ushuhuda wa furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa, lengo na hatima ya jicho la huruma na upendo kutoka kwa Kristo Yesu, kazi ambayo inaendelezwa kwa sasa na Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!