Tafuta

Miaka 400 Tangu Apofariki Dunia Mt. Francisko wa Sales: Noeli

Mwaliko kwa waamini kufuata njia ya upendo kwa Mungu na jirani, kwa kutafakari kuhusu Maadhimisho ya Sherehe ya Noeli yanayofumbatwa katika umaskini, unyenyekevu, upole; Ukuu na utukufu wa Mungu. Mtoto Yesu alizaliwa katika hali ya umaskini na hatimaye, kuyamimina maisha yake juu ya Msalaba katika hali umaskini na upweke wa kutisha na hatimaye kuzikwa kaburini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika Waraka wa Kitume, “Totum Amoris Est” yaani “Yote ni Kuhusu Upendo”: Miaka 400 Tangu Alipofariki Dunia Mtakatifu Francisko wa Sales” Baba Mtakatifu Francisko anapembua utume wa Mtakatifu Francisko wa Sale uliosimikwa katika ushuhuda wa upendo na kwamba, kigezo kikuu kilikuwa ni upendo. Malezi ya awali ilikuwa ni safari ya kujitambua binafsi mbele ya Mwenyezi Mungu; Kuvumbua Ulimwengu mpya na kwamba, upendo hufanya yote kwa ajili ya watoto wake; mahitaji ya mabadiliko ya nguvu katika kuhubiri, kiasi cha kuhitaji upepo na mbawa. Baba Mtakatifu afafanua kuhusu Ibada ya kweli inayopata chimbuko lake katika upendo kwa Mungu, chemchemi ya utakatifu wote na kilele cha furaha ya maisha. Utume na maisha ya Mtakatifu Francisko wa Sales yalisimikwa katika ushuhuda wa upendo uliomwilishwa katika huduma ya majadiliano ya kina na watu mbalimbali; kwa kuungamisha, kutoa mahubiri na mihadhara pamoja na kuwasiliana na jirani zake, ili kuwashirikisha uwepo wa Mungu kutoka katika sakafu ya moyo wake na kwamba, mahali muafaka pa kukutana na Mwenyezi Mungu ni katika nyoyo za waamini wake; Mwenyezi Mungu ambaye daima yuko katika kila hali ya maisha. Huu ni mwaliko kwa waamini kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao.

Miaka 400 tangu alipofariki dunia Mt. Francisko wa Sales: Noeli ya Bwana
Miaka 400 tangu alipofariki dunia Mt. Francisko wa Sales: Noeli ya Bwana

Baba Mtakatifu Franciko wakati wa Katekesi yake amewaambia waamini kwamba, Waraka wa Kitume, “Totum Amoris Est” yaani “Yote ni Kuhusu Upendo”: Miaka 400 Tangu Alipofariki Dunia Mtakatifu Francisko wa Sales” umezinduliwa rasmi tarehe 28 Desemba 2022, mwaliko kwa waamini kufuata njia ya upendo kwa Mungu na jirani, kwa kutafakari kwa kina kuhusu Maadhimisho ya Sherehe ya Noeli yanayofumbatwa katika umaskini, unyenyekevu, upole; Ukuu na utukufu wa Mungu. Mtoto Yesu alizaliwa katika hali ya umaskini na hatimaye, kuyamimina maisha yake juu ya Msalaba katika hali umaskini na upweke wa kutisha na hatimaye kuzikwa kaburini. Mwinjili Luka anakazia sana dhana ya Hori ya kulia ng’ombe. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Admirabile signum” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli” anafafanua kwa kina kuhusu: Pango la Noeli, Asili yake, Mchango wa Mtakatifu Francisko wa Assisi kuhusu Pango kama ishara ya uinjilishaji pamoja na alama za Pango la Noeli. Pango la Noeli ni mchakato unaojikita katika kueneza na kurithisha imani katika hatua mbalimbali za maisha na utume wa Kristo Yesu. Huu ni mwaliko wa kutafakari na kuhisi na kuonja uwepo wa Mungu kwa binadamu; kuhisi na kuonja uwepo angavu wa Mungu kati pamoja na waja wake.

Pango la Noeli lina amana na utajiri mkubwa katika maisha na utume Kanisa
Pango la Noeli lina amana na utajiri mkubwa katika maisha na utume Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Pango la Noeli ni mahali ambapo panaonesha alipozaliwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, alama hai ya Injili, mwaliko wa kutafakari Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipofanyika mwanadamu, ili kukutana na watu wote, ili kuwaonjesha upendo wake na hatimaye, waweze kuunganika pamoja naye. Kiini cha Pango la Noeli ni Mtoto Yesu, anayetangazwa na Malaika. Hori ya kulia ng’ombe, ndicho kitanda cha Mfalme wa amani, kielelezo cha ukaribu wa Mungu, huruma na upendo na msamaha ambao umetundikwa juu ya Msalaba. Mwenyezi Mungu katika mtindo wake wa maisha, anapenda kuonesha ukaribu, upendo wa kibinadamu unaowajibisha na huruma. Kristo Yesu yuko tayari kuwaonjesha watu wake huruma, upendo na msamaha wa dhati, mwaliko kwa waamini kutupilia mbali tabia ya majivuno na hali ya kutaka kujimwambafai na daima waamini wakumbuke kwamba, Kiti cha enzi cha Kristo Yesu ni Hori ya kulia wanyama na Ukuu, Utukufu na Utakatifu wake umetundikwa juu ya Msalaba.

Pango la Noeli: Ukaribu wa Mungu, Ufukara na Uhalisia wa maisha
Pango la Noeli: Ukaribu wa Mungu, Ufukara na Uhalisia wa maisha

Maadhimisho ya Sherehe ya Noeli ni mwaliko kwa waamini kurejea katika uhalisia wa maana ya Sherehe hii kamwe wasimezwe na malimwengu kwa kuigeuza Noeli ya Bwana, kuwa ni wakati wa biashara, kula na kunywa! Upendo wa Mungu ulemalala kwenye hori ya kulia ng’ombe. Mtakatifu Francisko wa Sales anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwangalia na kumtafakari Kristo Yesu aliyelazwa kwenye Hori ya kulia wanyama, mwaliko wa kukubali na kupokea yote ambayo Mwenyezi Mungu anapenda kuwakirimia waja wake, kwani daima anawatakia mema! Yote haya ni kuhusu upendo ambao umelazwa Pangoni, Huruma na Msamaha uliotundikwa Msalabani, mwaliko kwa waamini kumtafuta na kufuata nyayo za Kristo Yesu katika njia ya Msalaba.

Katekesi Noeli
28 December 2022, 15:58

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >