Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko asema maadhimisho ya Fumbo la Pasaka ni kiini cha Liturujia inayoadhimishwa na Mama Kanisa katika kipindi cha mwaka mzima wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko asema maadhimisho ya Fumbo la Pasaka ni kiini cha Liturujia inayoadhimishwa na Mama Kanisa katika kipindi cha mwaka mzima wa Kanisa. 

Juma Kuu: Fumbo la Pasaka Kiini Cha Mwaka wa Liturujia ya Kanisa

Maadhimisho ya Alhamisi kuu: Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu ya Upadre na ushuhuda wa upendo. Ijumaa Kuu: Mateso na kifo cha Kristo Msalabani; Siku ya sala, kufunga na toba. Jumamosi kuu ni siku ya ukimya, kesha la Pasaka na hatimaye, shangwe la Fumbo la Ufufuko wa Yesu. Mama Kanisa anaadhimisha Fumbo la Pasaka, huku bado kukiwa na maambukizi makubwa ya UVIKO-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Juma kuu ni kiini cha maadhimisho ya Mwaka wa Liturujia wa Kanisa, ambamo waamini wanaadhimisha Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Waamini wanaliishi Fumbo hili kila wakati wanapoadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ibada ya Misa Takatifu inapyaisha Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Hii ni Njia ya Msalaba kuelekea Mlimani Kalvari. Hii ni sehemu ya Katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 31 Machi 2021 kutoka kwenye Maktaba yake binafsi mjini Vatican. Katika katekesi hii, Baba Mtakatifu amejielekeza zaidi katika maadhimisho ya Alhamisi kuu: Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu ya Upadre na ushuhuda wa upendo. Ijumaa Kuu: Mateso na kifo cha Kristo Msalabani; Siku ya sala, kufunga na toba. Jumamosi kuu ni siku ya kimya kikuu, kesha la Pasaka na hatimaye, shangwe la Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu. Lakini, Mama Kanisa anaadhimisha Fumbo la Pasaka, huku bado kukiwa na maambukizi makubwa ya Virusi vya Ugonjwa wa Korona, UVIKO, 19. 

Alhamisi Kuu, Mama Kanisa anaadhimisha kumbukumbu endelevu ya siku ile Kristo Yesu alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, kielelezo makini cha ushuhuda wa upendo wake, unaobubujika kutoka katika Ekaristi Takatifu. Hii ni kumbukumbu ya uwepo wake kati pamoja na waja wake. Kristo Yesu ndiye Mwanakondoo wa Mungu anayeichukua dhambi ya walimwengu. Kwa Mwili na Damu yake Azizi amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kristo Yesu aliteswa na kufa Msalabani kwa sababu ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu na sadaka yake Msalabani imekuwa ni chombo cha ukombozi wa binadamu wote!

Ijumaa Kuu ni siku ya toba, kufunga, kusali na kutafakari Maandiko Matakatifu, ili kushiriki Njia ya Msalaba na hatimaye, kusimama chini Msalaba ili kuadhimisha: mateso na kifo cha Kristo Msalabani kinacholeta wokovu kwa binadamu. Ni siku ya kumwabudu Kristo aliyeteswa na hatimaye kulazwa Msalabani kwa ajili ya wokovu wa binadamu. Ni siku ya kuonesha mshikamano wa udugu wa upendo kwa: wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa na kutelekezwa pembezoni mwa jamii. Ni siku ya kuwakumbuka wahanga wa vita, ghasia na watoto waliotolewa mimba. Mbele ya Msalaba wa Kristo Yesu, waamini wanahimizwa kuwakumbuka na kuwaombea, wale wote wanaoelemewa ni Misalaba ya maisha, ili waweze kuonja huruma na faraja kutoka kwa Kristo Yesu.

Mateso, Madonda Matakatifu na kifo cha Kristo Yesu ni chemchemi ya huruma ya upendo wa Mungu unaomwagilia na kulainisha “majangwa ya nyoyo za binadamu”. Ni mwanga unaofukuzia mbali giza katika maisha ya waamini. Hili ni giza la vita inayoendelea sehemu mbalimbali za dunia. Ni giza la watoto wanaoteseka na kufariki dunia kwa baa la njaa na utapiamlo; kwa kukosa fursa za elimu na tiba. Ni giza la watu wanaoteseka kutokana na mashambulizi pamoja na vitendo vya kigaidi; watu wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo, inayokumbatia utamaduni wa kifo! Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, amekuwa ni chemchemi ya toba, msamaha wa dhambi na mwanzo wa maisha mapya kwa kutambua kwamba, binadamu anapendwa na kuthaminiwa na Mungu. “Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa”. 1 Pet 2:24. Kwa njia ya Fumbo la Msalaba, asiwepo tena mtu anayetembea katika giza la mauti na kifo. Huu ni mwaliko kwa waamini kumwachia nafasi katika nyoyo zao, ili aweze kuwaongoza.

Jumamosi Kuu, ni siku ya kimya kikuu na majonzi! Mitume waliokuwa wameweka matumaini yao kwa Kristo Yesu, walipoona jinsi alivyoteswa, akasulubiwa na kufa Msalabani, walivunjika moyo na kutawanyika. Wakajisikia kuwa ni watoto yatima na kuona kana kwamba, hata Mwenyezi Mungu “amewageuzia kisogo”. Jumamosi kuu ni Siku ya kuomboleza na Bikira Maria, lakini mwingi wa upendo na ujasiri, kiasi cha kuthubutu kufuata Njia ya Msalaba hadi kusimama chini ya Msalaba na hatimaye, kupokea maiti ya Mwanaye Mpendwa, Kristo Yesu. Hapa dunia inaonekana kusimama na kifo kushika mkondo wake! Lakini, Bikira Maria aliendelea kukesha kwa imani, matumaini na mapendo makuuu. Bikira Maria aliyegubikwa kwa giza nene la kifo cha Mwanaye, akageuka kuwa ni Mama wa waamini na Mama wa Kanisa, alama ya matumaini. Ushuhuda wake ni nguzo thabiti, pale waamini wanapoelemewa na Msalaba wa maisha.

Mkesha wa Pasaka ni Mama wa mikesha yote inayoadhimishwa na Kanisa. Huu ni Usiku ambamo wimbo wa Aleluiya Kuu unasikika, kielelezo cha imani ya waamini wanaokutana na Kristo Mfufuka. Waamini wataendelea kumshangilia Kristo Mfufuka kwa muda wa Siku 50, hadi Sherehe ya Pentekoste. Kristo Mfufuka anapenda kuwahakikishia waja wake kwamba, uzuri utashinda ubaya; maisha “yatapeta” dhidi ya utamaduni wa kifo! Kristo Yesu ni chemchemi ya huruma, upendo na msamaha wa Mungu. Mtakatifu Maria Magdalena alikuwa ni mfuasi wa kwanza wa Yesu kuona na kushuhudia kwamba, amefufuka kwa wafu. Baba Mtakatifu Francisko hapa anauliza swali na “kizushi kidogo”, Je, wale askari waliokuwa wameambiwa kulinda kaburi, kweli hawakumwona Kristo Mfufuka? Lakini, wakaamua kukaa kimya, kwa sababu walikula rushwa, wakafumbwa midomo na fedha kiasi cha kubadili ukweli wa mambo. Hata leo hii, rushwa inaendelea ili kunyamazisha ukweli, lakini iko siku ukweli huu utajulikana tu!

Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini kwamba, maadhimisho ya Sherehe za Pasaka kwa Mwaka 2021 bado yamegubikwa kwa maambukizi makubwa yanayosababishwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Waathirika wakubwa ni familia, watu wanaoteseka kwa umaskini, majanga asilia pamoja na vita. Msalaba wa Kristo ni mwanga angavu, unaowaangazia katika kipindi hiki cha mpito na mahangaiko makubwa. Msalaba wa Kristo unapaswa kuwa ni alama ya matumaini yasiyo danganya kamwe, kwani mateso na mahangaiko yao yote ni sehemu ya mpango wa wokovu wa Mungu kwa mwanadamu. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba, Mwenyezi Mungu ili awakirimie neema na baraka za kumtumikia kwa ari na moyo mkuu; kumtambua bila kumsahau kwa gharama kubwa aliyotoa kwa ajili ya ukombozi wao!

Papa Juma Kuu 2021
31 March 2021, 14:31

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >