Kardinali Koch:Miaka 40 ya ziara ya kwanza ya Papa Yohane Paulo II katika Sinagogi
Kardinali Kurt Koch
Ziara ya Mtakatifu Yohane Paulo II kwenye Sinagogi ya Roma mnamo tarehe 13 Aprili 1986, ilikuwa tukio la ajabu. Kwa mara ya kwanza katika historia, Askofu wa Roma aliingia kwenye sinagogi ili kutoa ushuhuda mbele ya ulimwengu kuhusu uthamini wake kwa dini ya Kiyahudi na watu wa Kiyahudi.
Papa alisisitiza kwamba Kanisa Katoliki lina uhusiano na Uyahudi tofauti na dini nyingine yoyote: "Dini ya Kiyahudi si ya 'nje' kwetu, lakini kwa maana fulani ni ya 'ndani' ya dini yetu wenyewe."
Aliwarejea Wayahudi kama "ndugu wapendwa sana na, kwa njia fulani, ndugu zetu wakubwa," hivyo akifupisha kwa ufanisi kile "kilichobainishwa na Mtaguso." Kupitia ziara hasa hii ya Sinagogi ya Roma miaka arobaini iliyopita na pia kupitia kauli zake nyingi muhimu kuhusu mazungumzo ya Kikatoliki na Kiyahudi, ishara mbalimbali za ufasaha, na urafiki wa kibinafsi aliodumisha na watu wa Kiyahudi, Papa Yohane Paulo II aliweka njia muhimu kwa ajili ya mustakabali wa maridhiano kati ya Kanisa Katoliki na Uyahudi.