Kard.Parolin,Ahmadi-Kuwait:Kuinuliwa kwa Basilika Ndogo ya Mama Yetu wa Arabia
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Bwana anatukusanya leo katika nyumba hii ya maombi, na anatuita tufurahi na kushangilia siku ya kihistoria, sio tu kwa Kanisa huko Kuwait, bali kwa Kanisa katika Ghuba nzima ya Arabia. Ndivyo alivyoanza mahubiri yake Kardinali Pietro Parolin, Katibu Mkuu wa Vatican, Ijumaa tarehe 16 Januari 2026 kutoa umuhimu wa Kanisa la Mama Yetu wa Arabia, wakati wa kuongoza misa Takatifu ya kuinuliwa kwa mahali pa ibada huko Ahmadiyya kuwa Basilika ndogo. Katika sherehe hiyo, ambayo imekuwa kilele cha ziara yake nchini Kuwait tangu tarehe 14 Januari 2025, Kardinali aliongeza kusema kuwa Baba Mtakatifu Leo XIV, anayewatumia salamu zake za dhati na ukaribu wa kiroho, ameinua Kanisa hilo la Ahmadi hadi hadhi ya Basilika Ndogo.
Kardinali Parolin alianza kuelezea historia ya Kanisa kwamba ilikuwa mwaka 1948 ambapo kikundi kidogo cha wafanyakazi wa kigeni, waliokuwa wamekuja katika nchi hizi kufanya kazi katika tasnia ya mafuta iliyoibuka wakati huo, walifungua Kanisa la kawaida. Lilibarikiwa tarehe 8 Desemba mwaka huo huo, na kuwekwa wakfu kwa Mama Yetu wa Arabia. Kutoka mwanzo huo mnyenyekevu, ibada kwa jina hili la Maria iliongezeka kwa kasi. Miaka michache baadaye, kwa baraka ya Papa Pio XII juu ya sanamu ya Mama Yetu wa Arabia, iliyochongwa kwa mwerezi wa Lebanon, Kanisa hilo lilijengwa, na kuwa Kanisa la kwanza Katoliki katika nchi ya Kuwait.
Hivyo ndivyo safari ndefu ya imani ilianza, ambapo Wakristo wengi wamempata Maria vazi la ulinzi: yeye ambaye ni Lango la Mbinguni na anayetupatia Mwanawe, Yesu Kristo. Likiwa limejengwa juu ya mchanga wa jangwa, Kanisa hili la Basilika linatukumbusha kwamba Maria mwenyewe aliwahi kupata kimbilio katika nchi zile zile za jangwa, ambapo alimtunza, alimlea, na kumlinda Mpatanishi mmoja kati ya Mungu na familia ya wanadamu, Yesu Kristo. Alijua nyakati za furaha na nyakati za majaribu, nyakati za kuondoka na kukimbia, pamoja na nyakati za kurudi—akitafakari mambo haya yote moyoni mwake.
Katibu Mkuu wa Vatican aliendelea kusema kuwa “mawazo yetu kwa kawaida huwageukia watu wengi kote ulimwenguni ambao, kwa sababu ya vita, umaskini, majanga ya asili, au magumu mengine, wanalazimika kutafuta mahali pa usalama. Ni Maria, aliyejaa neema, anayetufundisha kumlinda katika vilindi vya mioyo yetu Mtoto Yesu, ili kutetea imani kwake, hali yoyote ile ambayo maisha yanaweza kuleta. Kwa kutazama Injili iliyosomwa, Kardinali Parolin alisema “ katika Injili ya leo tunasikia swali la msingi ambalo Yesu anawauliza wanafunzi wake: “Watu husema Mwana wa Adamu ni nani?” Hatuwezi kumkaribisha Mtoto Yesu nyumbani kwetu na mikononi mwetu—ambaye kuzaliwa kwake na kumbusu kwake tumesherehekea hivi karibuni, isipokuwa tutambue utambulisho wake wa kweli na yote yanayomaanisha. Kama Kristo angekuwa nabii mmoja tu miongoni mwa wengine, au mtu mwema na mfano mzuri wa maadili, hangeweza kubadilisha maisha yetu katika kiwango chao cha ndani kabisa.
Petro, wa kwanza kati ya Mitume, akiongozwa na Roho Mtakatifu, alitangaza ukweli ambao ndio msingi wa imani yetu: “Wewe ndiwe Masiha, Mwana wa Mungu aliye hai.” Ni mtu aliyezaliwa kutoka juu tu anayeweza kukiri hivyo. Sisi Wakristo, kama Petro, tunaitwa kutambua na kushuhudia kwamba Yesu Kristo ni Mungu wa kweli na mwanadamu wa kweli. Ni Roho Mtakatifu, aliyepewa sisi, anayetuwezesha kuamini kwa moyo na kukiri kwa midomo yetu kwamba Yesu ni Bwana na kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu (taz. Warumi 10:9). Ingawa tumetungwa mimba katika dhambi, kama Zaburi inavyotukumbusha, tunazaliwa upya katika maji ya Ubatizo na kuwa viumbe vipya, washiriki wa Kanisa na raia wa mbinguni, wenye uwezo wa kutangaza kwa imani na uhakika kwamba Kristo ndiye Mwokozi wetu.
Siku hizi, tunashuhudia kwa huzuni jinsi wengi katika ulimwengu wetu hawamjui Kristo au hawakanushi utambulisho wake. Hata mchakato wa kutawaliwa na ulimwengu unaonekana kuendelea bila kupungua. Lakini Maandiko yanatuhakikishia kwamba kwa wale wanaompokea, anawapa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu, “waliozaliwa si kwa damu wala si kwa mapenzi ya mwili wala si kwa mapenzi ya mwanadamu, bali kwa Mungu” (Yh 1:13). Kardinali, aliomba kwa moyo wake wote kwamba Kanisa hili ambalo sasa limeinuliwa hadi hadhi ya Basilika Ndogo “liimarishe imani, tumaini, na upendo wa wote wanaokusanyika hapa. Na muwe hekalu la Mungu, mawe yaliyo hai yanayong'aa kuliko nyota, na mazuri zaidi kuliko jengo lolote la mawe. Kwa maana uzuri wa kweli haupatikani katika mwonekano wa nje, bali katika uzuri wa roho.”
Basilika hii iendelee kuwa mahali pa hija, ikiwavutia zaidi wale wanaomtafuta Maria, waliovikwa taji ya nyota kumi na mbili, kupumzika kutokana na kazi zao. Mchagueni Mwanawe. Mwamini. Mkaribieni moyoni Mwake, jiwe lililo hai ambalo, hata katika jangwa kavu, mto wa maji yaliyo hai hutiririka. Leo, Bwana anatuita tena kumtambua na kumfuata, kuwa mawe yaliyo hai katika ujenzi wa Kanisa Lake, nyumba ya kiroho, taifa teule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa Mungu. Katibu Mkuu wa Vatican alisisitiza kwamba "Kaka na dada, tangu asili yake hasa ikihusishwa na Maria, Mungu sasa anataka Basilika hii iendelee kuunganishwa kwa karibu na Roma, kwa Petro na warithi wake. Kanisa ni Petro; Kanisa ni Maria.
Kadhalika alisisitiza kuwa "Kanisa ni mwamba na ngome; Kanisa ni mama na rehema, kimbilio la wenye dhambi. Jipeni moyo! Msiogope kutoa ushuhuda wa imani yenu, kumtambua Yesu Kristo katikati ya kizazi hiki, "kati yao mnang'aa kama mianga duniani." Hebu tushikamane na Bwana, tuanguke mbele zake katika ibada, na tumwombe alifanye Kanisa hili kuwa "nyumba ya sala kwa watu wote" ya kweli. Mama yetu wa Arabia, Mlinzi wa Rasi nzima yenye jina lake, atuongoze daima kwa Mwanawe, yeye ambaye ni Lango la Mbinguni, Nyota ya Bahari, na Malkia wa Amani." Kwake Yeye Kardinali Parolin alipenda kumkabidhi ulinzi wa Nchi ya Kuwait, raia wake, na Wakristo wote."
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here