Tafuta

2026.01.15 Kard Parolin huko Kuwait - alihutubia mapadre na watawa. 2026.01.15 Kard Parolin huko Kuwait - alihutubia mapadre na watawa. 

Kard.Paolin,Kuwait:Kanisa ni kama nuru ambayo Mungu anawaangazia watu wa mataifa yote!

Katikati ya changamoto za dunia,Yesu ni kimbilio la amani kwa wanadamu.Haya yalisemwa na Katibu Mkuu wa Vatican,Kardinali Parolin wakati wa Misa katika Kanisa Kuu la Familia Takatifu akisisitiza jinsi eneo lililogawanywa kati ya jangwa na bahari limeweza kuwakaribisha watu wa tamaduni mbalimbali wanaotafuta mustakabali bora.Akikutana na Mapadre na watawa wa eneo hilo,aliwaalika kuwa makuhani wa upendo.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Jangwa si nafasi ya upweke wa kimwili tu, pia ni mahali Mungu anawachagua watu wake. Ni maneno yaliyosikika ya Katibu Mkuu wa Vatican Kardinali Pietro Parolin akiwa katika nchi ya Peninsula ya Arabia wakati wa  Ziara rasmi kuanzia tarehe 14 Januari ambapo Alhamisi tarehe 15 Januari 2026 aliongoza ibada ya misa Takatifu kwa Mpadre na watawa katika Kanisa Kuu la Familia Takatifu katika fursa ya maadhimisho ya miaka 65 ya kuwekwa wakfu kwa Kanisa hili, akiwasilisha hata salamu za dhati na ukaribu wa kiroho wa Papa Leo XIV.  Awali ya yote Kardinali Parolin alisema: “Ninawaletea salamu za joto kutoka kwa Baba Mtakatifu Leo XIV, ambaye anataka kuelezea ukaribu wake wa kiroho nanyi nyote wakati wa kuinuliwa kwa Kanisa la Mama Yetu wa Arabia huko Ahmadi hadi hadhi ya Basilika Ndogo. Cheo hiki, kilichotolewa na Baba Mtakatifu tarehe 28 Juni 2025, ni utambuzi wa kujitolea kwa kina ambako Wakristo wanaoishi katika nchi hizi wanamjua  Bikira Maria, kuwa Mama wa Bwana.”

Kanisa lipo kati ya Bahari na Jangwa:eneo halisi la kukutana na mazungumzo

Katibu Mkuu wa Vatican aliendelea kueleza, “Pia ni heshima kubwa kwangu, katika ziara yangu ya kwanza Kuwait, kusherehekea Ekaristi Takatifu hii katika Kanisa Kuu la Familia Takatifu, kwani inaadhimisha miaka sitini na tano ya kuwekwa wakfu kwake. "Kwa miaka mingi, Kanisa hili, lililopo kati ya Bahari na Jangwa, limekuwa mahali halisi pa kukutania mazungumzo ya kiekumeni na kidini, bandari salama, na mahali pa amani na maelewano.” Kardinali alisisitiza kwamba Tangu 1961, Kanisa Kuu hilo  limelisha maisha ya kiroho ya waamini wengi ambao wamefika kuishi na kufanya kazi Kuwait kutoka ulimwenguni kote. Vizazi vya watu, wanaozungumza lugha tofauti na wanaotoka katika tamaduni mbalimbali, wamevutwa kwenye nchi hii kwa matumaini ya mustakabali bora, na wamepata katika kanisa hili kimbilio la amani na ukuaji wa kiroho katika kumjua Yesu Kristo, Bwana wetu," alisisitiza Kardinali.

Kardinali Parolin aliadhimisha Misa katika Kanisa Kuu la Kuwait katika fursa ya miaka 65  ya kutabarukiwa kwake
Kardinali Parolin aliadhimisha Misa katika Kanisa Kuu la Kuwait katika fursa ya miaka 65 ya kutabarukiwa kwake

Katibu Mkuu alisisitiza jinsi ambavyo Tunavyojua kwamba Kristo alichagua kuishi katika nyumba ya Yosefu  na Maria, akiunda Familia Takatifu ya Nazareti, ambayo chini ya uangalizi wake Kanisa Kuu hili limetengwa. Hili linaakisi umuhimu wa familia na jumuiya kama nafasi za upendeleo ambapo Mungu anachagua kujifunua. Katika Familia Takatifu ya Nazareti, tunapewa mfano wa maisha ya Kikristo yenye mizizi katika ushirika, imani, tumaini, na upendo. Zaidi ya hayo, katika mazingira haya ya kipekee ya kijiografia, kati ya bahari na jangwa, inafaa kutafakari uwepo wa vipengele hivi viwili katika historia ya wokovu.

Jangwa ni mahali ambapo Mungu aliwaongoza watu na kuanzisha agano jipya

Jangwa si nafasi ya kimwili ya upweke tu. Ni mahali ambapo Mungu alichagua kuwaongoza watu wake ili kuanzisha agano na kuonyesha ukaribu wake kwa kuwaunga mkono njiani. Jangwa ni sehemu ya ufundishaji wa Mungu: mahali pa ukimya, kusikiliza, kutakasa, na kubadilika. Kutoka jangwani sauti ya Yohana Mbatizaji inasikika, ikituita tutayarishe mioyo yetu: “Sauti inasikika jangwani: Itengenezeni njia ya Bwana, nyoosheni mapito yake” (Mt 3:3). Sauti hiyo inaendelea kutualika kufungua mioyo yetu ili Yesu Kristo aingie hekaluni mwa maisha yetu, akituweka huru kutokana na yote yanayotuzuia kumwabudu Bwana katika roho na kweli (taz. Yh 4:23). Bahari, kwa upande mwingine, ina maana kubwa kwa jamii zinazoishi karibu na maji ya Ghuba ya Arabia. Mara nyingi huelezewa kama “kioo cha jangwa.” Kama vile mababu zetu walivyojifunza kusoma nyota ili wasiangamie katika mchanga mkubwa, pia walijifunza kwamba bahari ni “jangwa la bluu,” wakidai heshima, ujasiri, na zaidi ya yoteutegemezi sawa kwa Muumba.

Bahari inakuwa mahali pa utakaso na kukutana

Kwa maana hiyo, bahari inakuwa mahali pa maongozi, utakaso, na kukutana. Tunakumbuka jinsi Kristo alivyowaita wanafunzi wake wa kwanza kando ya pwani ya bahari (taz. Mt. 4:18), jinsi alivyofunua nguvu zake za kimungu katika uvuvi wa ajabu wa samaki (taz. Lk. 5:1), na jinsi, akitembea juu ya maji yenye dhoruba, alivyowahakikishia wanafunzi wake kwa maneno haya: “Msiogope” (taz. Mt. 14:27). Kama ishara ya utakaso, bahari pia inawakilisha nafasi ya mwanzo mpya, ikikumbuka Roho wa Mungu akielea juu ya maji mwanzoni mwa uumbaji (taz. Mwa. 1:2). Imewekwa kimkakati mahali ambapo ukubwa wa mchanga wa jangwa unakutana na upeo usio na kikomo wa Ghuba, Kanisa Kuu hilo la Familia Takatifu, aliendelea ,  linasimama kama sehemu ya kukutana kati ya jangwa na bahari: kama lulu ya thamani inayotoka katika utakaso, kama nyota ya kiroho inayoongoza hatua za wale wanaoishi jangwani mbali na nyumbani na wale wanaosafiri katika "jangwa la bluu" wakiwa na tumaini la uzima wa milele.

KARDINALI PAROLIN
KARDINALI PAROLIN   (AFP or licensors)

Kardinali Parolin aliendelea  kufikiria Kanisa hilo la Kanisa Kuu kama nuru ambayo Mungu anawaangazia watu wa mataifa yote, akiwakumbusha kwamba katikati ya changamoto za ulimwengu kuna kimbilio la amani, ambapo imani hufanya kazi kama dira na Yesu Kristo ndiye bandari salama kwa wanadamu wote. Hata hivyo maana halisi ya hekalu hili haipatikani katika kuta zake za mawe, bali katika mawe yake yaliyo hai, waamini wanaokusanyika hapa. Hao ndio hekalu la kweli la Mungu. Mtakatifu Paulo anatukumbusha hili anapothibitisha kwamba kila mmoja wetu ni hekalu la Roho Mtakatifu (taz. 1 Kor. 6:19). Wakati huo huo, hekalu hili ambalo mara nyingi hujeruhiwa na kuchafuliwa na dhambi linaweza kuwa hatarini, kama Bwana anavyoonya, “pango la wezi” (Mt 21:13).

Kristo hutakasa hekalu

Karidnali Paroli aliendelea kusema kuwa, "Hii ndiyo sababu Kristo alikuja kulisafisha na kulijenga upya kupitia kifo na ufufuko Wake, akitangaza kuwa: “Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha” (Yh 2:19). Kristo hutakasa hekalu ndani ya kila mmoja wetu na anatuita kuwa sehemu ya hekalu kubwa na lililo hai: Kanisa. Kanisa ni moja, lakini tajiri katika utofauti wa viungo vyake; mwili mmoja wenye viungo vingi, ambavyo Kristo ndiye Kichwa chake. Ukweli huu unaonyeshwa vizuri na jumuiya za Kikristo zinazokusanyika kila siku katika Kanisa Kuu hili. Zaidi ya miaka sitini na mitano, jumuiya tajiri na tofauti ya kikanisa imechukua umbo hapa, waaminifu wa ibada tofauti, kutoka Mashariki na Magharibi, wakionesha ukatoliki wa Kanisa: umoja katika Kristo.

Kama Papa Francisko alivyosema, Roho Mtakatifu anafundisha Kanisa “kupanuka katika ulimwengu wote na kuungana katika umoja. Ulimwengu na Mmoja: hii ndiyo siri ya Kanisa” (Katekesi tarehe 9 Oktoba 2024). "Tunaposherehekea Jubilei ya Kanisa Kuu hili na kuinuliwa kwwa kwa Kanisa la Mama Yetu wa Arabia hadi  hadi ya Basilika Ndogo, tunaboresha ahadi yetu ya kuwa mawe hai ya hekalu hili la kiroho, linalokumbatia jangwa na bahari.  Jumuiya hii ya kikanisa, yenye utajiri wa ibada na tamaduni, iendelee kung'aa kama lulu ya imani na mazungumzo katika nchi hii nzuri ya Kuwait." Tunapoondoka kwenye kuta hizi, Kardinali Parolin aidha alisema "hebu tubebe ndani mwetu utume wa kuwa mahekalu ya Roho Mtakatifu, tukijenga Kanisa ambalo, katika ulimwengu wake na umoja wake, linaonyesha upendo wa Mungu chini ya ulinzi wa Mama Yetu wa Arabia. Familia Takatifu ya Nazareti ituongoze kila wakati, ikifanya imani yetu kuwa dira yetu na Yesu Kristo kuwa bandari salama ya maisha yetu.

Salamu kwa viongozi wa makanisa mengine

Mwishoni mwa Misa (kabla ya baraka ya mwisho, Kardinali Parolin alikuwa na ya kusema kwamba:  “Kaka na dada wapendwa, Kabla ya baraka ya mwisho, ningependa kutoa salamu zangu za dhati kwa viongozi wa Makanisa mbalimbali na madhehebu ya Kikristo ya Ghuba Katoliki, Kiorthodox, Kiinjili, Kianglikani, na Kiprotestanti, ambao watakusanyika katika siku zijazo kwa mkutano wa kiekumeni hapa Kuwait, unaoambatana na Juma la Maombi kwa Umoja wa Kikristo. Roho Mtakatifu awape msukumo wa kutafuta njia mpya kuelekea umoja uliosubiriwa kwa muda mrefu, na jinsi mnavyoishi pamoja kwa kukaribishana na kuheshimiana viwe mfano na mfano kwa wote."

Kardinali Parolin huko Kuwait: Misa katika Kanisa Kuu

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here

 

16 Januari 2026, 09:30