Jubilei ya miaka 800 ya Kifo cha Mt.Francis:Rehema Kamili!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika fursa ya miaka 800 ya kifo cha Mtakatifu Francis wa Assisi, Mwaka maalum wa Jubilei pamoja na msamaha kamili au Rehema Kamili (Undulgenzia Plenaria) ulitangazwa. Katika tangazo kutoka Idara ya Toba ya Kitume iliyotolewa kulingana na matakwa ya Baba Mtakatifu Leo XIV, ilichapishwa tarehe 10 Januari 2026. Katika tangazo hilo linabaisha kwamba, “Kwa mapenzi ya Baba Mtakatifu (rej. Barua ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwa Wakuu wa Mashirika ya Familia ya Wafranciskani katika tukio la ufunguzi wa Miaka mia nane ya Kifo cha Mtakatifu Francis wa Assisi, Januari), tarehe 10 Januari 2026, hadi tarehe 10 Januari 2027, Mwaka Mtakatifu wa Mtakatifu Francis utaadhimishwa, ambapo ni "wakati wa neema inayotolewa kwa Kanisa zima ili kuiishi mitazamo yetu na mioyo yetu kwa mwanga wa mfano unaong'aa wa Poverello wa Assisi, yaani Maskini wa Assisi.
Kwa hiyo katika Barua ambayo Baba Mtakatifu Leo XIV alituma kwa Wakuu wa Mashirika ya Kifransiskani Papa anabainisha kuwa, “inaanza safari hii ya Jubilei, ambayo inakumbusha kwa nguvu thamani ya ulimwengu wa ushuhuda wa Mtakatifu Francis, mtu wa amani, mwanafunzi mkali wa Injili, na mtangazaji asiyechoka wa amani inayotoka kwa Kristo.” Papa anasema kuwa “katika wakati uliojaa migogoro, mgawanyiko, na majeraha ya ndani na kijamii, Mtakatifu wa Assisi ni kama mwongozo wa uhakika wa kugundua upya chanzo halisi cha amani: upatanisho na Mungu, na kaka na dada zetu, na viumbe vyote. Mwaka huu wa Jubilei, katika mwendelezo kamili wa Jubilei ya Kawaida ya 2025, kwa hivyo unajionesha kama fursa ya maongozi ya uongofu, upya wa kiroho, na ushuhuda wa kiinjili, ili, katika nyayo za Mtakatifu Francis, kila mwamini aweze kuwa ishara hai ya matumaini, maelewano, na upendo hai duniani.
Hafla ya Uzinduzi wa Jubilei ya miaka 800
Hafla ya Uzinduzi wa Jibilei hiyo ilifunguliwa tarehe 10 Januari 2026 asubuhi saa 4:00 kwa salamu kutoka kwa Ndugu Mdogo Massimo Travascio, Msimamizi Mkuu wa Basilika ya Mtakatifu Maria wa Malaika huko Porziuncola, na kuendelea na maandamano yaliyoongozwa na Ndugu Francesco Piloni, Mkuu wa Wafransikani wa Provinsi ya Umbria na Sardegna pamoja na Wakuu sita wa Mashrika ya Kifransiskani: Ndugu Mdogo Massimo Fusarelli (OMF), Ndugu Carlos Alberto Trovarelli (OFM Conventual), Ndugu Roberto Genuin (OFM Capuchin), Tibor Kauser(Wafransiskani wa Kisekula OFS), Ndugu Amando Trujillo Cano (Shirika la Wafransiakani wa Tatu), na Sista Daisy Kalamparamban, Mwenyekiti wa Mashirika ya Kimataifa ya Wafransiakani wa Ndugu na Dada wa Shirika la Tatu la Mtakatifu Francis wa Assisi.
Ishara ya haraka na yenye maana
Askofu Mkuu-Askofu wa Assisi-Nocera Umbra-Gualdo Tadino na Foligno, Domenico Sorrentino, na Meya wa Assisi, Valter Stoppini, walitembea kuelekea Kanisa la alipofia Mtakatifu Francis wakiwa wameshika mshumaa usiowashwa mikononi mwao. Kisha waliwasha kupitia Mshumaa wa Pasaka, ishara ya Kristo aliyefufuka. Kutoka hapo, mwanga ulipelekwa kwenye vituo sita vya kando vya Basilika, kila kimoja kikiwa kimekabidhiwa kwa moja ya matawi sita wa familia ya Wafransiskani.
Msafara huo ulikumbuka upatanisho kati ya Askofu Guido II na meya wa Assisi, Carsedonio, ulioadhimishwa na Francis kama unabii wa amani. Kwa njia hiyo katika barua iliyotumwa kwao, Baba Mtakatifu aliwahakikishia wale watakaoshiriki katika matukio ya ukumbusho na kisha akatoa sala iliyotolewa kwa ajili ya Maskini Mtakatifu Francis. Sala ya Papa aliyotuma:
"Mtakatifu Francis, kaka yetu, wewe ambaye miaka mia nane iliyopita ulikwenda kukutana na Dada Kifo kama mtu mwenye amani, utuombee kwa Bwana. Katika Msalaba wa Mtakatifu Damiano ulitambua amani ya kweli. Tufundishe kumtafuta Yeye chanzo cha upatanisho wote unaobomoa kila ukuta. Wewe ambaye, bila silaha, ulivuka mipaka ya vita na kutokuelewana, utupe ujasiri wa kujenga madaraja ambapo ulimwengu hujenga mipaka. Katika wakati huu unaokumbwa na migogoro na mgawanyiko, utuombee ili tuweze kuwa wapatanishi: bila silaha na mashahidi wa amani inayotoka kwa Kristo. Amina."
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.