Tafuta

Miaka 800 ya kifo cha Mtakatifu Francis wa Assis(1226-2026). Miaka 800 ya kifo cha Mtakatifu Francis wa Assis(1226-2026). 

Papa Leo XIV,OFM:Amani ni jumla ya baraka zote za Mungu kutoka Juu

Katika Barua ya Papa Leo XIV aliyotumwa kwa wakuu wa Shirika la Familia ya Ndugu wadogo Wafransiskani(OFM)katika fursa ya ufunguzi wa sherehe za miaka 800 tangu kifo cha Mtakatifu Francis anabainisha:"Amani ni jumla ya mema yote ya Mungu,zawadi inayoshuka kutoka Juu.Ingekuwa udanganyifu ulioje kufikiria kuijenga kwa juhudi za kibinadamu pekee."Papa anawahakikishia kuungana nao watakaoshiriki katika matukio ya ukumbusho na kuchapisha sala kuomba Mtakatifu huyo.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV, aliandika barua kwa Wakuu wa Familia ya Shirika la Wafransiskani(OFM) huko Assisi, katika fursa ya  ufunguzi rasmi, Jumamosi tarehe 10 Januari 2026, sherehe za miaka 800 tangu  kifo cha Mtakatifu Francis kilichotokea kunako mwaka 1226.  Katika barua hiyo Papa alianza kuandika kuwa:"Dada yetu kifo," alishangaa Mtakatifu Francis mnamo tarehe 3 Oktoba  1226, huko Porziuncola,(Kikanisa kidogo sana) alipomkaribia kama mtu ambaye hatimaye alikuwa na amani. Karne nane zimepita tangu kifo cha Poverello wa Assisi, ambaye aliandika neno la wokovu la Kristo kwa makini katika mioyo ya watu wa wakati wake. Katika kuadhimisha kumbukumbu muhimu ya miaka mia nane ya kifo chake, ninatamani kuungana kiroho na Familia nzima ya Wafransiskani na pamoja na wote watakaoshiriki katika matukio ya ukumbusho, nikitumaini kwamba ujumbe wa amani unaweza kupata mwangwi mkubwa katika Kanisa na jamii leo.

Mwanzoni mwa wito wa Mtakatifu Francis

Mwanzoni mwa maisha yake ya kiinjili, alisikia wito: "Bwana alinifunulia kwamba tunapaswa kusema salamu hii: 'Bwana na awape amani.'" Kwa maneno haya muhimu, anawafahamisha watawa wake na kila mwamini mshangao wa ndani ambao Injili ilimletea maishani mwake: Amani ni jumla ya baraka zote za Mungu, zawadi inayoshuka kutoka juu. Ingekuwa udanganyifu ulioje kufikiria kuijenga kwa nguvu za kibinadamu pekee! Na bado ni zawadi inayofanya kazi, ya kukaribishwa na kuishi kila siku. Ni salamu ile ile ambayo Bwana aliyefufuka aliwasalimia wanafunzi wake, wakiwa na hofu na kufungiwa katika Chumba cha Karamu Kuu huku juu  jioni ya Pasaka: "Amani iwe nanyi." Sio mtindo wa heshima, bali ni tangazo la uhakika la ushindi wa Kristo dhidi ya kifo.

Francis anatambua kila kiumbe mwonekano wa uzuri wa kimungu

Kama sauti ya malaika usiku wa  Noeli, "Utukufu kwa Mungu juu, na amani duniani miongoni mwa watu aliopendezwa nao" hivyo amani ambayo Baba wa Seraphic anatangaza ni amani ambayo Kristo mwenyewe aliifanya ivume kati ya mbingu na dunia. Katika enzi hii, iliyo na vita vingi vinavyoonekana kutokuwa na mwisho, na mgawanyiko wa ndani na kijamii unaosababisha kutoaminiana na hofu, anaendelea kusema. Si kwa sababu anatoa suluhisho za kiufundi, bali kwa sababu maisha yake yanaelekeza kwenye chanzo halisi cha amani. Maono ya Wafransiskani ya amani hayazuiliwi na uhusiano kati ya wanadamu, bali yanakumbatia viumbe vyote. Francis, anayeliita jua "kaka" na mwezi "dada," na anayetambua katika kila kiumbe mwonekano wa uzuri wa kimungu, anatukumbusha kwamba amani lazima ienee kwa familia nzima ya Uumbaji.

"Nyumba yetu inatishiwa na kuugua kwa unyonyaji"

Ufahamu huu unaonekana kwa uharaka wa pekee katika wakati wetu, wakati nyumba yetu ya pamoja inatishiwa na kuugua chini ya unyonyaji. Amani na Mungu, amani kati ya watu na Uumbaji ni vipimo visivyoweza kutenganishwa vya wito mmoja wa upatanisho wa ulimwengu wote. Baba Mtakatifu anendelea kukazia kwa ndugu hao wapendwa kwamba,kwa mfano na urithi wa kiroho wa Mtakatifu huyu, mwenye imani thabiti, imara katika tumaini, na mwenye bidii katika upendo hai kwa wengine, na awapatie msukumo katika umuhimu wote wa kumtumaini Bwana, wa kujitolea kwa maisha minifu kwa Injili, wa kukubali na kuwaangazia kwa imani na sala kila hali na tendo la maisha.

Sala ya Papa Leo: "Wewe bila silaha ulivuka mipaka ya vita"

Katika Mwaka huu wa neema,  Papa Leo XIV  alipenda kuwaombea kwamba Mtakatifu Francis wa Assisi aendelee kututia sote furaha na maelewano kamili:

"Mtakatifu Francis, kaka yetu, wewe ambaye miaka mia nane iliyopita ulikwenda kukutana na Dada Kifo kama mtu mwenye amani, utuombee kwa Bwana. Katika Msalaba wa Mtakatifu Damiano ulitambua amani ya kweli. Tufundishe kumtafuta Yeye chanzo cha upatanisho wote unaobomoa kila ukuta. Wewe ambaye, bila silaha, ulivuka mipaka ya vita na kutokuelewana, utupe ujasiri wa kujenga madaraja ambapo ulimwengu hujenga mipaka. Katika wakati huu unaokumbwa na migogoro na mgawanyiko, utuombeeni ili tuweze kuwa wapatanishi:bila silaha na mashahidi wa amani inayotoka kwa Kristo. Amina."

Kwa hisia hizo Papa alihitimisha kwa kuelezea matashi ya dhati ya wema hasa kwa :“nyinyi nyote mnaofuata karama ya Poverello wa Assisi na kwa wale watakaokumbuka dies natalis yake kwa njia mbalimbali, huku nikitoa kwa uchangamfu Baraka ya Kitume inayotakiwa.” Barua hiyo ilitiwa saini mjini Vatican tarehe 7 Januari 2026.

Papa kwa Wafransiskani

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.

10 Januari 2026, 13:59