Papa Leo XIV kwa Waagostinian wa Katalonya:wape utajiri wenu wa kiroho kwa kila mtu
Tiziana Campisi na Angella Rwezaula Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV aliwapatia mwaliko kwa takriban wanashirika 25 wa familia ya Mtakatifu Agostino aliokutana nao alasiri ya tarehe 9 Juni 2026 katika makazi ya Askofu Mkuu huko Barcelona, "Msijifungie ndani ya jumuiya zenu, bali mpeleke utajiri wa maisha yenu ya kiroho kwa kila mtu katika mazingira ya kila siku." Yamejiri akiwa tayari katika kituo chake cha Pili cha hija yake ya 4 ya kitume nchini Hispania.
Papa Leo XIV, kulingana na chaneli ya Telegram ya Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Vatican, inabainisha kuwa, alitumia karibu nusu saa, "katika mazingira ya upendo na urafiki," pamoja na wenzake kutoka Katalonya na Wamisionari wa Kiagostinian, Watawa wa ndani wa Kiagostinian na Masisita wa Faraja wa Kiagostinian. Mwishoni mwa mazungumzo, Papa Leo XIV alitoa baraka zake na kuwasalimu watawa hao wa kike na kiume mmoja mmoja
Waagostinian wa Barcelona
Miongoni mwa Waagostinian waliokuwapo katika mkutano huo, ni watawa 4 wa Jumuiya ya Kimataifa wanaoishi katika Parokia ya Carme huko Barcelona, katika Wilaya ya Raval, wanajitolea kwa huduma ya kichungaji katika Parokia za Mtakatifu Roque, Mtakatifu Agostino, Mama asiye na Dhambi na Mtakatifu Lorenzo Ruiz. Padre Dennis Pineda, Padre Michael Go Maambong, Padre Faustin John Mlelwa, Padre Laurent Joseph Temanya, hawa ni kutoka Ufilippini na Tanzania na katikati ya jiji kuu la Kikatalani, wanajitolea kwa shughuli mbalimbali. Kwa kushirikiana na kushiriki majukumu, wanatekeleza kazi yao ya kichungaji katika mazingira ya kidugu, mfano wa karama yao ya Kiagostinian.
Shughuli za Kichungaji za Watawa
Katika Parokia ya Mtakatifu Roque, watawa, pamoja na kusimamia mipango na sherehe za uinjilishaji, wanahamasisha mipango mbalimbali ya kielimu, kijamii, na kiutamaduni inayolenga watoto, vijana, na watu wazima, hasa kwa kuzingatia makundi yaliyo hatarini. Kazi hii ya kijamii na kielimu inafanywa kwa ushirikiano na Mfuko wa Mtakatifu Roque ambao uko katika Parokia hiyo hiyo. Pia katikati ya Barcelona, katika Parokia ya Mtakatifu Agostino, ambapo Papa atakutana na mashirika ya upendo na usaidizi ya jimbo kuu tarehe 10 Juni 2026, watawa hawa wanawajibika kwa Katekesi na liturujia, kuongoza jumuiya za Kikristo kutoka nchi mbalimbali za Amerika Kusini ambazo husherehekea utamaduni na ibada zao hapo na kushirikiana na Mfuko wa Mano Amiga, ambao husaidia wahamiaji kwa kusambaza chakula na nguo.
Wahudumu wa Parokia, pamoja na kutoa mahitaji ya kiroho na kimwili ya wale wanaohudhuria Parokia, huwatunza watu wengi wa dini zingine. Hatimaye, katika Parokia ya Mama asiye na Dhambi na Mtakatifu Lorenzo Ruiz, Waagostinian wanaunga mkono Jumuiya ya Wafilipino wanaoishi katika jiji kuu la Kikatalani, wakiwapa huduma ya kichungaji waamini, wakiwasaidia katika mahitaji yao ya kiroho na kijamii. Parokia zote tatu pia zina dhamira ya kuwasindikiza wahamiaji. Waagostinian wamekuwepo Barcelona tangu karne ya 13. Konventi yao ya kwanza ilijengwa mwaka 1349 katika kitongoji cha Ribera. Leo hii, kwa kiasi kikubwa kuna kumbukumbu ya Picha ya jiji, Jumba la Makumbusho la Chokoleti, na Hoteli ya Mtakatifu Agostino. Katika karne ya 18 Waagostinian walihamia Wilaya ya Raval na hapo wanaendelea kutekeleza utume wao kwa "moyo mmoja na roho moja", wakifuata mwongozo wa Mtakatifu Agostino.
Zawadi za Watawa wa Kiagostinian
Familia ya Kiagostinian nchini Hispania imehamasishwa sana katika siku za hivi karibuni kwa ajili ya ziara ya kitume ya Papa Leo XIV. Zaidi ya watu 8,000, wakiwemo vijana, familia, na wanaume na wanawake watawa kutoka sehemu mbalimbali za nchi, walifika Madrid kati ya Jumamosi na Jumatatu ili kushiriki katika mikutano na Papa. Hata hivyo, wengi hawakuweza kusafiri hadi mji mkuu, na watawa wa ndani wa Kiagostinian wa Seville na Huelva, lakini walitengeneza Rozari kwa ajili yao. Ishara hii pia ilionesha mapendo yao kwa Papa Leo XIV na kuwafanya wale waliounganishwa na jumuiya zao za watawa na wale watakaowatembelea wakati wa kukaa kwa Papa Leo XIV nchini Hispania wajisikie karibu naye.
Wakati wa ziara ya Papa huko Madrid, watawa wa Kiagostinan wa Monasteri ya Mtakatifu Isabel waliandaa biskuti zinazoitwa "pastas de San Alonso," zilizopewa jina la mwanzilishi wa Jumuiya ya watawa, Mtakatifu Alonso de Orozco. Vitumbua hivyo vilipelekwa kwa Papa, pamoja na barua. Katika barua hiyo, watawa hao walimkumbusha Papa uwepo wao Roma tarehe 19 Mei 2002, siku ya kutangazwa kwa Mtakatifu Alonso kuwa mtakatifu, na mkutano wao katika Uwanja wa Mtakatifu Petro pamoja naye, ambaye wakati huo alikuwa Mkuu wa Shirika la Mtakatifu Agostino.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here
