Papa Leo XIV: Katekesi Kuhusu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican: Liturujia: Ibada, Ishara na Alama
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV baada ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, anaendeleza Mzunguko wa Katekesi unaojikita katika Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Usomaji Mpya wa Nyaraka zake, ili kugundua tena uzuri na umuhimu wa tukio hili la Kikanisa, Kipindi cha neema ambacho kwa hakika, Mama Kanisa amekifaidi sana katika Karne ya ishirini. Kumbe, hiki ni kipindi cha Kanisa kujikita zaidi katika Nyaraka Kuu 4 za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yaani: “Dei verbum” yaani “Ufunuo wa Kimungu”, “Sacrosanctum concilium” yaani “Juu ya Liturujia”; “Lumen gentium” yaani “Fumbo la Kanisa” pamoja na “Gaudium et spes” yaani “Kanisa katika ulimwengu mamboleo.” Katiba ya “Sacrosanctum concilium” yaani “Juu ya Liturujia” inaelezea kanuni za jumla za marekebisho na ukuzaji wa Liturujia Takatifu; Fumbo Takatifu la Ekaristi, Sakramenti nyingine na visakramenti; Liturujia ya Vipindi; Mwaka wa Liturujia wa Kanisa, Muziki Mtakatifu; na hatimaye, ni Sanaa Takatifu na Vifaa vitakatifu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanafafanua nafasi ya Liturujia katika fumbo la Kanisa kwa kusema kwamba, maana kwa njia ya Liturujia, hasa Sadaka takatifu ya Ekaristi, “latimizwa tendo la ukombozi wetu.” Liturujia inasaidia kikamilifu waamini waoneshe katika maisha yao na kuwadhihirishia wengine fumbo la Kristo Yesu na pia maumbile halisi ya Kanisa la kweli. Kanisa kwa undani kabisa ni la kibinadamu na pia la kimungu, linaloonekana lakini lenye mambo yasiyoonekana ndani yake, lenye bidii kubwa katika matendo na uradhi katika kutafakari, lililopo ulimwenguni lakini kama mwenye kufanya hija. Hayo yote yamo ili yale ya kibinadamu ndani yake yaelekezwe kwa yale ya kimungu, yaonekanayo kwa yasiyoonekana, matendo kwenye kutafakari, yaliyopo yaelekee mji ujao tunakoelekea.
Hivyo Liturujia kila siku inawajenga wale waliomo katika Kanisa wawe hekalu takatifu la Bwana, makao ya Mungu katika Roho, mpaka kuufikia utimilifu wa Kristo. Wakati huohuo kwa namna ya ajabu Liturujia inaimarisha nguvu za waamini kumhubiri na kumshuhudia Kristo Yesu; na kwa njia hiyo inawaonesha wale walio nje [nalo,] Kanisa lililo ishara iliyoinuliwa juu kati ya Mataifa, ambayo chini yake watoto wa Mungu waliotawanyika wakusanyika katika umoja mpaka liwepo zizi moja chini ya mchungaji mmoja. Rej. SC, 2. Katekesi ya Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 3 Juni 2026 imenogeshwa na sehemu ya Injili ya Luka inayomwonesha Kristo Mfufuka akiwatokea wafuasi wa Emau: “Wakakikaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, naye alifanya kama anataka kuendelea mbele. Wakamshawishi wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukaa nao. Ikawa alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao.” Lk 24:28-31. Mababa wa Kanisa wanasema, Mama Kanisa anajibidisha kwa namna nyingi kusudi waamini waweze kushiriki ibada takatifu kwa akili, kwa moyo na kwa matendo ya kiliturujia, wakielewa vizuri fumbo hilo kwa njia ya matendo ya kiliturujia na sala. Waamini wanapaswa kuelimishwa kuhusu: Neno la Mungu, walishwe katika Karamu ya Bwana, wamtolee Mungu shukrani wakijiunga kikamilifu na Sadaka takatifu ya Misa, huku wao wenyewe wakijifunza kujisadaka bila ya kujibakiza, ili hatimaye, waweze kukamilishwa katika umoja na Mungu kati yao, ili hatimaye Mungu awe yote katika wote. Rej. SC, 48.
Hii ni Katekesi iliyosimikwa katika: Ibada, Ishara na Alama za kiliturujia na sala, ili kuwawezesha waamini kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa moyo wa ibada na uchaji wa Mungu, kwa kukazia mambo msingi katika maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, katika Maadhimisho ya Ibada waamini wanapata mantiki ya sadaka na ukarimu; wanapata muda wa kusimama na kutafakari; mambo yanayojenga na kupyaisha moyo, kwa kutambua kwamba, waamini wanatanguliwa na neema ya Kimungu na hivyo kujifunza kuishi kadiri ya mpango wa Roho Mtakatifu. Kristo Yesu yupo katika Liturujia ya Kanisa ambalo kwa njia yake Mungu hutukuzwa kikamilifu na wanadamu wanatakatifuzwa. Katika Liturujia kwa ishara zinazoonekana, huoneshwa na kutendeka kutakatifuzwa kwake binadamu, kila ishara ikiwa na maana yake ya pekee. “Adhimisho la Sakramenti limesukwa kwa ishara na alama. Kadiri ya malezi ya Mungu ya wokovu, maana yake ina mizizi katika kazi ya ukombozi na katika utamaduni wa watu. Huainishwa ndani ya matukio ya Agano la Kale na kufunuliwa kikamilifu katika nafsi na kazi ya Kristo.” KKK 1145. Alama ya Maji inapata chimbuko lake katika kazi ya uumbaji na mafuriko; alama ya watu wa Mungu kuvuka Bahari ya Shamu na hatimaye, ni Maji yanayobubujika kutoka ubavuni mwa Kristo Yesu, alama ya Sakramenti ya Ubatizo, kielelezo cha mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema ishara na alama hizi zinawaelekeza waamini katika maisha mapya kwa njia ya Ubatizo, yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na kwamba, alama na ishara hizi ni vielelezo vya Kisakramenti, mambo yanayowaunda waamini, kwa kugusa akili na nyoyo zao na hivyo kuibua uhusiano wa Kikanisa, mwaliko kwa waamini kujibidisha kufahamu maana ya ishara na alama, ili kuweza kushiriki vyema maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa. Kazi ya kwanza ya malezi na majiundo ya Kiliturujia ni kumwezesha mwanadamu kuwa na uwezo wa kusoma alama na ishara. Tajiriba ya liturujia hai inayosimikwa katika Ibada na uchaji wa Mungu inaambatana na Katekesi ya Mafumbo ya Kanisa ni nyenzo bora zaidi ya kupyaisha uwezo wa mwamini kukutana na Mwenyezi Mungu, ambao katika mantiki ya Fumbo la Umwilisho, unaweza kutokea tu kwa kumshirikisha mtu mzima: roho, nafsi na mwili. Rej. 1 The 5:23.
