Papa Leo XIV:Diplomasia ya Kipapa ni kukuza na kulinda heshima ya wote
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatatu tarehe 27 Aprili 2026 alitembelea Chuo cha Kipapa cha Kanisa jijini Roma, ambapo katika hotuba yake alifafanua juu ya wito maalum kwa Padre wa kidiplomasia ya kipapa ambaye anaitwa kujikita na Diplomasia ya huduma ya amani, ukweli na haki. Mkutano huo ulifanyika ndani ya muktadha wa maadhimisho ya miaka 325 ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo, ambayo Papa alikuwa tayari ameitembelea kabla ya kuchaguliwa kuwa Kharifa wa Mtume Petro, alipokuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maaskofu.
Kujenga umoja kati ya tofauti
Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake alionesha shukrani kubwa kwa historia ya kujitolea na huduma iliyoadhimishwa na maadhimisho haya ya furaha. Ni historia muhimu, iliyowezeshwa na mapadre kutoka ulimwenguni kote ambao wamechangia kwa juhudi zao za unyenyekevu za kujenga umoja huo katika Kristo ambao, kati ya utofauti wa asili, hufanya ushirika kuwa sifa inayofafanua Kikosi cha Kidiplomasia ya Vatican.
Mageuzi ya kufufua muundo wa mafunzo
Papa Leo XIV kadhalika alitafakari kuhusu mageuzi ambayo yameipatia taasisi hiyo uhuru unaohitajika ili kufufua muundo wa mafunzo ya sheria, historia, sayansi ya siasa na uchumi, pamoja na utafiti wa lugha zinazotumika katika mahusiano ya kimataifa. Hata hivyo kuna mageuzi muhimu zaidi, alisisitiza kwamba ni ya zoezi la uongofu la mara kwa mara, linalolenga kukuza ukaribu, kusikiliza kwa makini, ushuhuda, mbinu ya kidugu na mazungumzo, pamoja na unyenyekevu na upole, fadhila zote ambazo lazima zienee katika huduma yao yote ya ukuhani, Papa alisisitiza.
Amani iwe nanyi:utume unakuwa madaraja na njia
Akiwakumbuka watakatifu, wenyeheri na Mapapa ambao wameunda historia ya Chuo hicho, Baba Mtakatifu aliakisi jukumu la kipekee la Padre wa kidiplomasia wa kipapa kwamba ni mjumbe wa tangazo la Pasaka lile la, “Amani iwe nanyi!” Hata wakati matumaini ya mazungumzo na upatanisho yanaonekana kufifia, bado ni muhimu kupeleka maneno yote ya Kristo Mfufuka asemaye: "Ninawaachieni amani, nawapeni amani yangu," Papa alisisitiza. Kwa kusisitiza zaidi, Papa alisema “Utume wenu unawataka kuwa madaraja na njia ili neema itokayo mbinguni iweze kuingia katika historia.
Diplomasia ya Papa ni kupeleka ukweli
Katika kudadavua aidha Baba Mtakatifu alibainisha kuwa Kazi nyingine ya mwanadiplomasia wa kipapa ni kupeleka Ukweli ambao ni Kristo, katika mkutano wa mataifa, kuwa ishara ya upendo Wake kwa sehemu hiyo ya ubinadamu iliyokabidhiwa kwa uangalizi, awali kama mchungaji, na kisha tu kama mwanadiplomasia. Kwa njia hiyo Papa Leo XIV alirudia, kama alivyofanya katika hotuba yake ya Kikundi cha Kidiplomasia kilichoidhinishwa na Vatican , mwanzoni mwa mwaka 2026, kwamba maneno yale yana uzito na lazima tena "yaeleze ukweli waziwazi na bila utata, ili kukuza mazungumzo halisi bila kutoelewana, kwa kushuhudia kile ambacho kimekuwa mwili."
Huduma ya mwanadiplomasia si kwa jumuiya ya wakatoliki
Kwa kupanua mtazamo wake lazima kukumbatia familia nzima ya wanadamu, “kwani huduma ya mwanadiplomasia huyo haishii na Jumuiya ya Wakatoliki tu. Kwa hiyo Papa alisema inawataka kuwa watetezi wa kila aina ya haki inayosaidia kutambua, kurejesha na kulinda taswira ya Mungu iliyochorwa ndani ya kila mtu. Katika ulimwengu uliojaa mvutano, ambao unaonekana kufanya migogoro kuwa njia pekee ya kushughulikia mahitaji, juhudi zetu za kujitolea kwa mazungumzo, kusikiliza na upatanisho zinaweza kuonekana kuwa hazitoshi, wakati mwingine hata hazina maana, Papa alisema."
Wakati huo huo katika salamu zake, Askofu Mkuu Salvatore Pennacchio, Rais wa Chuo cha Kipapa cha Kanisa, alisisitiza kwamba ziara ya Papa ni chanzo cha kutia moyo katika njia ya maandalizi ya huduma katika diplomasia ya Vatican. Pia alitoa matashi mema yake kwa Kardinali Pietro Parolin katika maadhimisho ya miaka 46 ya kuwekwa wakfu kwake kwa ukuhani, ambayo ilifanyika tarehe 27 Aprili 1980.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here
