Papa Leo XIV:Sitisheni mapigano,mamlaka zifanye kazi kwa ajili ya amani kupitia mazungumzo
Vatican News
Baba Mtakatifu Leo XIV, akijibu kundi la waandishi wa habari waliokuwa wakimsubiri nje ya Villa Barberini, makazi yake huko Castel Gandolfo, ambapo ametumia muda kati ya Machi 23 hadi jioni machi 24, ambayo imekuwa ni siku yake ya kawaida ya kupumzika na kufanya kazi alirudia kutoa wito wake katika muktadha wa vita kwamba: "Sitisheni mapigano" na "kufanya kazi kwa ajili ya amani, lakini si kwa silaha," badala yake "kupitia mazungumzo, kwa kutafuta suluhisho la kweli kwa kila mtu."
Kuhusu hali ya kimataifa, Papa Leo XIV alisema, "chuki inaongezeka, vurugu zinazidi kuwa mbaya, zaidi ya watu milioni moja "wametengwa," na "vifo vingi" vinarekodiwa. "Tunataka kuombea amani, lakini ninawasihi mamlaka zote kufanya kazi kwa bidii kupitia mazungumzo ili kutatua matatizo," Papa alisema.
Hata hivyo akiwa katika dirisha la Jumba la Kitume, mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 22 Machi 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV, akiwageukia waamini na mahujaji waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro alikuwa ameelezea: "kusikitishwa" kwake na hali katika Mashariki ya Kati na katika maeneo mengine ya dunia "yaliyogawanywa na vita na vurugu." "Hatuwezi kukaa kimya mbele ya mateso ya watu wengi wasio na ulinzi ambao ni waathiriwa wa migogoro hii," Papa alisema. "Kinachowaumiza kinawaumiza wanadamu wote. Kifo na maumivu yanayosababishwa na vita hivi ni kashfa kwa familia nzima ya wanadamu na kilio kinachomfikia Mungu!" Papa Leo aliendelea, "Ninarudia wito wangu wa kudumu katika maombi, ili uadui ukome na njia za amani hatimaye zifunguke, kwa kuzingatia mazungumzo ya dhati na heshima kwa utu wa kila mwanadamu."
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.
