Papa Leo XIV:Hatuwezi kukaa kimya mbele ya mateso ya wasio na ulinzi!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Dominika ya Tano ya Kwaresima, tarehe 22 Machi 2026, mara tu baada ya Tafakari na sala ya Malaika wa Bwana, amerudia kutoa wito mzito katika muktadha wa vita vinavyoendelea ulimwenguni kote. Akianza alisema: "Kaka na dada wapendwa, ninaendelea kufuatilia kwa masikitiko hali ilivyo Mashariki ya Kati, kama ilivyo katika maeneo mengine ya dunia yaliyoharibiwa na vita na vurugu. Hatuwezi kukaa kimya mbele ya mateso ya watu wengi, wahanga wasiojiweza wa migogoro hii. Chochote kinachowaumiza, kinawaumiza wanadamu wote."
Kifo na maumivu ya wasio na hatia
Papa Leo XIV aliendelea kueleza kuwa, “Kifo na maumivu yanayosababishwa na vita hivi ni kashfa kwa familia nzima ya wanadamu na kilio kwa Mungu! Ninarudia wito wangu kwa nguvu kuendelea katika sala, ili uadui ukome na njia za amani, zilizojengwa juu ya mazungumzo ya dhati na heshima kwa utu wa kila mwanadamu, hatimaye ziweze kufunguka.”
"Marathon ni ishara ya matumaini"
Papa akigeukia washiriki wa mbio za Marthon kutoka Ulimwenguni kote, zaidi ya watu 60,000, alisema, "leo hii Roma, Marathon kubwa inafanyika, ikiwa na wanariadha wengi kutoka ulimwenguni. Hii ni ishara ya matumaini! Michezo na iwashe njia za amani, ujumuishaji wa kijamii, na kiroho."
Salamu
Papa aliendelea na salamu zake za dhati kwa wote kuanzia na "Warumi na mahujaji kutoka nchi mbalimbali, hasa wale kutoka Jimbo la Córdoba nchini Hispania." Papa alisema " Ninawakaribisha kwa furaha waamini kutoka Belluno na Pordenone, kutoka Crotone, na kutoka Parokia ya Mtakatifu Maria wa Neema, Roma. Ninawasalimu vijana wa Nave, Jimbo la Brescia, kundi la wanakipaimara kutoka Jimbo la Firenze, na wawakilishi wa Chama cha Wasimamizi wa Hoteli." Alihitimishwa kwa kuwatakia wote Dominika Njema.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku bonyeza hapa: Just click here.
