Papa Leo XIV: Mapokeo Na Maandiko Matakatifu Ni Mahali Muafaka Pa Mungu Kuzungumza

Papa Leo XIV anasema, Mapokeo na Maandiko Matakatifu ni mahali ambako Mwenyezi Mungu anaendelea kuzungumza na watu ili kwa kumsikiliza, waweze kumfahamu na kumpenda. Neno la Mungu limeandikwa kwa kutumia maneno ya binadamu, ili kumwezesha Mwenyezi Mungu kuingia katika majadiliano na binadamu; kufahamu upendo wake usiokuwa na kikomo. Hivi ndivyo ilivyo mpendeza Mwenyezi Mungu kujifunua kwa kutumia maneno na lugha ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni tukio lililowakusanya viongozi wa Kanisa kutoka sehemu mbalimbali za dunia, ili kujadili maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, chini ya uongozi na usimamizi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, wakati huo akiwa katika nafsi ya Mtakatifu Yohane XXIII; Ukatafsiriwa kwa vitendo na Mtakatifu Paulo VI pamoja na Mtakatifu Yohane Paulo II. Baba Mtakatifu Benedikto XVI akapyaisha mafundisho yake kwa Katekesi makini kuhusu: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha Adili na Sala. Hayati Baba Mtakatifu Francisko akaendelea kujipambanua kwa kutaka ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu ili kuchangia katika maisha na utume wa Kanisa la Kristo Yesu, kila mmoja kadiri ya karama, wito na dhamana yake ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Miaka 60 tangu kuzinduliwa kwa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican tarehe 11 Oktoba 1962, katika mahubiri yake, alikazia kuhusu: Upendo ambao Kristo Yesu ameonesha kwa Kanisa lake, licha ya dhambi, udhaifu na mapungufu ya kibinadamu na hata wakati mwingine, kumezwa na malimwengu, changamoto na mwaliko kwa Kanisa kurejea tena katika chemchemi ya upendo ule wa awali ulioneshwa na Kristo Yesu kwa Kanisa lake: Moja, takatifu, katoliki na la mitume. Hili ni Kanisa linalotumwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili inayomwilishwa katika imani tendaji. Kanisa katika upendo, unyenyekevu na sadaka, linakabidhiwa utume wa kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Kristo na wa Mungu; kutangaza Habari Njema ya Wokovu sanjari na utamadunisho, ili kushiriki: furaha na matumaini; uchungu na fadhaa ya walimwengu.

Katekesi Kuhusu Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican
Katekesi Kuhusu Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican   (@Vatican Media)

Mkazo ni ushiriki mkamilifu wa ukuhani wa waamini wote unaowawezesha kushiriki sadaka ya Ekaristi Takatifu, kwa kupokea Sakramenti za Kanisa, kwa kusali na kwa njia ya ushuhuda wa maisha matakatifu, toba, wongofu wa ndani, kwa kujikana na kwa upendo wenye utendaji; Umoja wa watu wa Mungu ukipewa kipaumbele cha kwanza. Kanisa litambue kwamba, maskini wanao upendeleo wa pekee mbele ya Mwenyezi Mungu. Kwa hakika Kanisa ni Sakramenti ya umoja inayowaunganisha watu kiundani na Mwenyezi Mungu na hivyo kuleta umoja kati ya wanadamu wote. Ni jukumu la Mama Kanisa kuendelea kujikita katika Mapokeo, sera na mikakati ya shughuli za kiuchungaji. Mwaliko wa kuendeleza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Huu pia ni ni mwaliko wa kujenga na kudumisha ushirika wa Kanisa, ili wote wawe na umoja kama Kristo Yesu alivyojisadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema baada ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, kuanzia Jumatano tarehe 7 Januari 2026 anaanzisha mzunguko mpya wa Katekesi unaojikita katika Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Usomaji Mpya wa Nyaraka zake, ili kugundua tena uzuri na umuhimu wa tukio hili la Kikanisa, Kipindi cha neema ambacho kwa hakika, Mama Kanisa amekifaidi sana katika Karne ya ishirini. Kumbe, hiki ni kipindi cha Kanisa kujikita zaidi katika Nyaraka Kuu 4 za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yaani: “Dei verbum” yaani “Ufunuo wa Kimungu”, “Sacrosanctum concilium” yaani “Juu ya Liturujia”; “Lumen gentium” yaani “Fumbo la Kanisa” pamoja na “Gaudium et spes” yaani “Kanisa katika ulimwengu mamboleo.”

Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni Tukio la Kikanisa: Upyaisho wa Utume
Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni Tukio la Kikanisa: Upyaisho wa Utume   (@Vatican Media)

Hati ya Kusikiliza kwa Uchaji Ufunuo wa Neno la Mungu “Dei verbum” inagusia kwa undani kuhusu: Ufunuo wenyewe; Urithishaji wa Ufunuo wa Kimungu; Uvuvio wa Kimungu na Ufafanuzi wa Maandiko Matakatifu; Agano la Kale, Agano Jipya; pamoja na Maandiko Matakatifu Katika Maisha ya Kanisa. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu, Ufunuo wa Baba wa milele, anazungumza na wanadamu kama mtu anavyo zungumza na rafiki yake. Huu ni mwaliko kwa waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao pamoja na kujikita katika maisha ya sala!Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, “kwa njia ya ufunuo huo, ukweli kamili juu ya Mungu na juu ya wokovu wa wanadamu unang’ara kwetu katika Kristo Yesu, ambaye Yeye mwenyewe ndiye mshenga na utimilifu wa ufunuo wote.” DV 2. Kristo Yesu ametumwa na Baba na kwa njia yake, wanadamu wanaweza kushiriki katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ili kuweza kulifahamu fika kuna haja ya kujenga mahusiano na Kristo Yesu pamoja na Roho Mtakatifu kama anavyosimulia Mwinjili Luka kuona furaha ya Kristo Yesu kwa jinsi amnavyo Injili hufunuliwa kwa watoto wachanga katika Baba na Mwana. “Saa ile ile alishangilia katika Roho Mtakatifu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza. Akasema, Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu, wala hakuna amjuaye Mwana ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia.” Lk 10:21-22.

Kristo Yesu ni Ufunuo wa Baba wa Milele
Kristo Yesu ni Ufunuo wa Baba wa Milele   (@VATICAN MEDIA)

Kristo Yesu anakamilisha ufunuo wa Baba yake wa milele. Maana alimtuma Mwanawe, yaani Neno wa Milele, anayewaangazia watu wote, ili akae kati ya wanadamu na kuwafunulia siri za Mungu. Rej. DV, 4. Na Baba yako aonaye sirini atakujazi na kwamba, Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba. Rej Mt 6; 4.6.8; 62; 32. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema kwa njia ya Kristo Yesu, mwamini anaweza kuufahamu ukweli kuhusu Mungu Baba na wao wenyewe kujifahamu kuwa waana katika Mwana. Mwenyezi Mungu amejifunua kwa njia ya Kristo Yesu kwa kutumia mwili wake. Kwa kumwona Kristo Yesu, watu wanamwona pia Baba aliyemtuma. Rej Yn 14:9. Kwa uwepo na ushuhuda wake; kwa maneno na kazi zake, kwa alama na miujiza aliyotenda lakini zaidi ni kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake mtukufu kutoka kwa wafu na hatimaye, kwa kumtuma Roho wa kweli. Rej DV, 4. Ili kuweza kumfahamu Mungu katika Kristo Yesu, kuna haja kwa waamini kuupokea ubinadamu wake katika ukamilifu wote kwani “Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua.” Yn 1:18. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufuata kikamilifu njia ya Kristo Yesu, watu wanaweza kugundua kwamba, hakuna kitu chochote kinachoweza kuwatenga na upendo wa Mungu kama anavyosema Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa katika utenzi wake kuhusu upendo wa Mungu; “Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye? Rum 8:31-32. Ni kwa njia ya Kristo Yesu, Mkristo anamfahamu Mungu Baba Mwenyezi na hivyo kujiachilia mikononi mwake kwa imani.

Familia zijenge utamaduni wa kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu
Familia zijenge utamaduni wa kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu   (@Vatican Media)

Mababa wa Kanisa wanasema, kile ambacho Kristo Yesu aliwakabidhi Mitume, wao walikiendeleza kwa mahubiri au kwa maandishi, kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu, kwa vizazi vyote mpaka Kristo Yesu atakaporudi katika utukufu. “Mapokeo Matakatifu na Maandiko Matakatifu yanaunda amana moja tu takatifu ya Neno la Mungu.” DV, 10; ambamo kama kioo, Kanisa lililoko safarini lamtafakari Mwenyezi Mungu, aliye chanzo na utajiri wake wote. Katika mafundisho, maisha na ibada, Kanisa linadumisha na kuendeleza kwa vizazi vyote, yale yote yanayolifanya liwe lilivyo na yale yote linaloyasadiki. Rej. DV 8&1. Taifa lote la Mungu, kwa nguvu ya hali yake ya imani ya Kimungu haliachi kupokesa paji la Ufunuo wa Mungu, haliachi kupenya daima ndani zaidi na kuishi kwa ukamilifu zaidi. Kazi ya kufafanua kwa uthabiti Neno la Mungu imekabidhiwa tu kwa Mamlaka rasmi ya ufundishaji katika Kanisa, yaani kwa Baba Mtakatifu na Maaskofu wakiwa katika umoja naye. Rej. KKK 96-100. Baba Mtakatifu Leo XIV katika Katekesi yake, Jumatano tarehe 4 Februari 2026 ambayo imenogeshwa na sehemu ya Neno la Mungu lisemalo: “Bali wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao; na ya kuwa tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu. Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki.” 2Tim 3:14-17.

Mapokeo Matakatifu Na Maandiko Matakatifu ni Mahali pa Mazungumzo
Mapokeo Matakatifu Na Maandiko Matakatifu ni Mahali pa Mazungumzo   (@VATICAN MEDIA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mapokeo Matakatifu na Maandiko Matakatifu ni mahali muafaka ambako Mwenyezi Mungu anaendelea kuzungumza na watu wa nyakati hizi, ili kwa kumsikiliza, waweze kumfahamu na kumpenda. Neno la Mungu limeandikwa kwa kutumia maneno ya binadamu, ili kumwezesha Mwenyezi Mungu kuingia katika majadiliano na binadamu; kufahamu upendo wake usiokuwa na kikomo. Hivi ndivyo ilivyo mpendeza Mwenyezi Mungu kujifunua kwa binadamu kwa kutumia maneno na lugha ya binadamu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema: “Maana, maneno ya Mungu yaliyotamkwa kwa lugha za binadamu yameingia katika maneno ya mwanadamu, kama vile Neno wa Baba wa Milele alivyojifanya mtu, akichukua udhaifu wa maumbile ya kibinadamu” DV, 13. Hapa maudhui na lugha iliyotumika, inaonesha kwamba katika Maandiko Matakatifu, ukweli na utakatifu wa Mungu ukiwa imara daima, hisani “Condescensio” ya ajabu ya Hekima ya milele inadhihirishwa, ili kuifunua huruma ya Mungu kwa binadamu pamoja na nia yake ya kutaka kuwa karibu na binadamu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema kweli zilizofunuliwa na Mwenyezi Mungu zilizomo na zinazoelezwa katika matini ya Maandiko Mtakatifu, zimeandikwa chini ya uvuvio wa Roho Mtakatifu. Mungu mwenyewe ndiye mtunzi na Maandiko Matakatifu yamekabidhiwa kwa Kanisa na kwamba, linafundisha kwa nguvu na uaminifu bila hitilafu ukweli ambao Mwenyezi Mungu alitaka ukabidhiwe kwa Maandiko Matakatifu kwa ajili ya wokovu wa watu wa Mungu. Rej. DV, 11.

Kanisa ni Sakramenti ya Umoja
Kanisa ni Sakramenti ya Umoja   (@Vatican Media)

Kumbe, tafsiri sahihi ya Maandiko Matakatifu lazima izingatie: mazingira ya kihistoria, maneno ya binadamu yaliyotumika na kwamba, Maandiko Matakatifu lazima yamwilishwe katika hali halisi, tayari kumwilishwa katika historia ya mwanadamu, ili hatimaye, Maandiko Matakatifu yaweze kupenya na kugusa nyoyo za watu, daima kwa kuendelea kusoma alama za nyakati kwa kuzingatia mtindo wa kujieleza ili kuweza kuupyaisha Ulimwengu mamboleo. Maandiko Matakatifu yanapaswa kupewa uzito wake unaostahili na kamwe yasiangaliwe kama ni “Waraka uliopitwa na wakati.Maandiko Matakatifu yanapotangazwa mintarafu maadhimisho ya Liturujia Takatifu, lengo ni kuliwezesha Neno la Mungu kuweza kuzungumza na waamini, kugusa maisha yao, fursa, changamoto na matatizo yao, ili kuwaangazia njia na maamuzi ya kufanya. Maandiko Matakatifu yanapaswa kusomwa na kufafanuliwa kwa msaada wa Roho Mtakatifu, kwa kujali umoja wake, Mapokeo hai ya Kanisa na ulinganifu wa imani. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Maandiko Matakatifu yanapaswa kuwasaidia waamini kukoleza Injili ya upendo kwa Mungu na jirani; tayari kuitolea ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kama chemchemi ya utimilifu wa maisha na uzima ambao Mwenyezi Mungu amewapatia wanadamu kwa njia ya Kristo Yesu. Mwenyezi Mungu katika wema na ukarimu wake wa daima, ataendelea kuwalisha waja wake kwa Neno lake, mwaliko kwa waamini kusali kwa kutumia maneno yao, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, ili waonje upendo na huruma ya Mungu kama inavyosimuliwa katika Maandiko Matakatifu.

Papa Leo XIV Mapokeo ya Kanisa
04 Februari 2026, 15:20

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >