Baba Mtakatifu Leo XIV: Kwa Mungu Kila Mtu Anayo Nafasi ya Pekee
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Katika maadhimisho ya Kipindi cha Pasaka ya Bwana, kama Kanisa la Mwanzo, waamini wanafanya rejea ya kufafanua maana ya maneno ya Kristo Yesu katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, kifo na ufufuko uletao wokovu. Mambo yale yaliyokuwa yamefichika katika maisha ya wafuasi wa Kristo Yesu yanaibuka tena katika kumbukumbu, yanachangamsha na kuwapatia wafuasi matumaini mapya! Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya Tano ya Kipindi cha Pasaka Mwaka A wa Kanisa inaleta mbele ya waamini majadiliano kati ya Kristo Yesu na Wafuasi wake, wakati wa Karamu ya mwisho. Rej Yn 14:1-12. Kristo Yesu anawaambia wafuasi wake kwamba, anakwenda kuwaandalia makao, atakuja tena kuwachukua, ili mahali alipo wawepo pia wafuasi wake. Ni katika muktadha huu wa ahadi kutoka kwa Kristo Yesu, Mitume wanagundua kwamba, ndani ya Mwenyezi Mungu kila mtu anayo nafasi!
Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, Dominika tarehe 3 Mei 2026 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Anasema, haya ni mang’amuzi ambayo wanafunzi wake wawili walikuwa wameyapitia tangu siku ile ya kwanza walipokutana na kuzungumza na Kristo Yesu baada ya kutambulishwa kwao na Yohane Mbatizaji na kwamba, kati yao alikuwa ni Andrea ndugu yake Simon Petro waliomsikia Yohane na kumfuata Kristo Yesu. Rej. Yn 1:39. Kristo Yesu anapokikabili kifo, anaendelea kuzungumzia kuhusu nyumba, lakini kubwa zaidi kwani hii ni nyumba ya Baba yake wa milele ambayo ina nafasi kwa kila mtu. Kristo Yesu anajieleza kwamba Yeye ni mtumishi anayeandaa nafasi kwa kila mtu, ili wale wote watakapofika wajikute wakiwa tayari na hivyo kuhisi kwamba, walikuwa wakingojewa na sasa wamefika!
Baba Mtakatifu Leo XIV anaendelea kusema, mambo yanayoleta mvuto wa pekee katika Ulimwengu wa zamani, ni maeneo maarufu, tajiriba na mang’amuzi ya watu wachache na kwamba, huu ni upendeleo wa watu wachache wanaoweza kuingia ndani mwake! Lakini, Kristo Mfufuka katika Ulimwengu mpya anawavuta watu wote kwake na hivyo anakuwa ni chemchemi ya furaha; sadaka na majitoleo na hapo ushindani usiokuwa na tija wala mvuto unakoma; Ukarimu unafuta mwelekeo wa ubaguzi na kwamba, wingi wa neema na baraka unafutilia mbali tabia ya kukosekana kwa usawa. Hakuna kuchanganyiwa wala kupotea na kutokomea mahali kusikojulikana. Kifo kinatishia kufutilia mbali jina na kumbukumbu hai, lakini Mwenyezi Mungu anajidhihirisha kuwa ni mwenyewe. Kwa hakika, hapa ndipo mahali ambapo watu wote wanapatafuta, wakati mwingine hapa ni mahali ambapo baadhi ya watu wanataka kuangaliwa kwa jicho la pekee na hatimaye, kutambuliwa!
Kristo Yesu ndiye njia, ukweli na uzima anawataka wanafunzi wake kamwe wasifadhaike mioyoni mwao bali wamwini Mungu sanjari na kumwaini Kristo Yesu. Rej Yn 14:1 na mioyo yao itawekwa huru kutokana na wasi wasi unao wasonga katika maisha yao, udanganyifu na kutamani cheo cha juu au kupata thamani ya kitu fulani. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kila mtu katika siri na mbele ya Mwenyezi Mungu anayo thamani isiyokuwa na kikomo, huu ni ukweli wa kiwango cha juu na kwamba, waamini wanapaswa kupendana wao kwa wao kama Kristo Yesu alivyowapenda. Huu ndiyo msingi wa Amri mpya, kumbe wanadamu wanatazamia mbingu na dunia mpya itakayowafunulia kwamba udugu na amani ndiyo hatima yao ya maisha. Katika mchakato wa kumwilisha Injili ya upendo, kila mtu anagundua kwamba, yeye ni wapekee sana mbele ya Mungu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV katika tafakari yake, amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Bikira Maria, Mama wa Kanisa, ili kila Jumuiya ya Kikristo iwe ni nyumba iliyo wazi na makini kwa watu wote.