Papa Francisko alipigia simu Parokia ya Gaza,wana furaha na tuombee amani!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mara baada ya Katekesi yake, Jumatano tarehe 22 Januari 2025, Baba Mtakatifu Francisko katika salamu zake kwa mahujaji na waamini waliokusanyika katika Ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican alisema: "Ninawakaribisha kwa moyo mkunjufu mahujaji wanaozungumza Kiitaliano. Kwa namna ya pekee, ninawasalimu Mabinti wa Maria Immaculate wanaoadhimisha Mkutano mkuu huku nikiwahimiza wajitoe wenyewe kwa uaminifu kwa mapenzi ya Mungu ambaye ni mwaminifu kwetu daima." Na kisha ninawasalimia parokia, vyama na shule, hasa shule ya Sekondari ya Einstein ya huko Teramo.
Kisha Papa alisema: “Na ninataka mjue kwamba moyo wangu unawaendea watu wa Los Angeles, ambao wameteseka sana kutokana na moto ambao umeharibu vitongoji na jumuiya nzima. Na hawajamaliza… Mama Yetu wa Guadalupe awaombee wakazi wote ili wawe mashahidi wa matumaini kwa nguvu ya utofauti na ubunifu ambayo kwayo wanajulikana duniani kote. Papa akiendelea alisema: “Na tusisahau kuteswa kwa Ukraine. Tusisahau Palestina, Israel na Myanmar. Tuombe amani. Vita daima ni kushindwa!"
Papa pia alisema kwamba "Jana niliita, ninafanya kila siku, Parokia ya Gaza: walikuwa na furaha! Kuna watu 600 mle ndani, kati ya parokia na chuo. Na wakaniambia: "Leo tumekula dengu na kuku." Kitu ambacho hawakuzoea kufanya siku hizi: kwani walikuwa wanakula mboga mboga tu, na hivyo walifurahi! Lakini tuombe amani kwa ajili ya Gaza na sehemu nyingine nyingi za dunia. Vita daima ni kushindwa! Msisahau: vita ni kushindwa. Na ni nani anayefaidika na vita? Watengenezaji wa silaha. Tafadhali, tuombe amani. Hatimaye, mawazo yangu yanawaendea vijana, wagonjwa, wazee na waliofunga ndoa hivi karibuni.
Papa Francisko vile vile ameeleza juu ya Juma la Kuombea Umoja wa Kikristo lililoanza tangu tarehe 18 Januari na litahitimishwa tarehe 25 Januari ikiwa Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Uongofu wa Mtakatifu Paulo Mtume wa Watu: “Katika siku hizi za maombi kwa ajili ya umoja wa Kikristo, ninawasihi tumwombe Mungu, Mmoja na Utatu, kwa ajili ya ushirika kamili wa wanafunzi wote wa Kristo!” Hatimaye ametoa Baraka zake kwa wote.
