2025.01.22 Papa ameeleza alivyowaita Parokia ya Gaza na kusisitiza kuomba amani. 2025.01.22 Papa ameeleza alivyowaita Parokia ya Gaza na kusisitiza kuomba amani.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa Francisko alipigia simu Parokia ya Gaza,wana furaha na tuombee amani!

Mwishoni mwa Katekesi Papa alisimulia alivyopiga simu kwa Jumuiya ya Familia Takatifu,huko Gaza na kwamba walimweleza walivyokula dengu na kuku,jambo ambalo hawakuzoea kulifanya nyakati hizi.Papa alitoa wito mpya dhidi ya vita ambayo siku zote ni kushindwa.Wazo kwa wazee wa Ukraine ambao wanakabiliwa na janga la vita na kwa wakazi wa Los Angeles wanaosumbuliwa na moto.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Mara baada ya  Katekesi yake, Jumatano tarehe 22 Januari 2025, Baba Mtakatifu Francisko katika salamu zake kwa mahujaji na waamini waliokusanyika katika Ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican alisema: "Ninawakaribisha kwa moyo mkunjufu mahujaji wanaozungumza Kiitaliano. Kwa namna ya pekee, ninawasalimu Mabinti wa Maria Immaculate wanaoadhimisha Mkutano mkuu huku nikiwahimiza wajitoe wenyewe kwa uaminifu kwa mapenzi ya Mungu ambaye ni mwaminifu kwetu daima." Na kisha ninawasalimia parokia, vyama na shule, hasa shule ya Sekondari ya Einstein ya huko Teramo.

Papa Francisko na mahujaji
Papa Francisko na mahujaji   (Vatican Media)

Kisha Papa alisema:  “Na ninataka mjue kwamba moyo wangu unawaendea watu wa Los Angeles, ambao wameteseka sana kutokana na moto ambao umeharibu vitongoji na jumuiya nzima. Na hawajamaliza…  Mama Yetu wa Guadalupe awaombee wakazi wote ili wawe mashahidi wa matumaini kwa nguvu ya utofauti na ubunifu ambayo kwayo wanajulikana duniani kote. Papa akiendelea alisema: “Na tusisahau kuteswa kwa Ukraine. Tusisahau Palestina, Israel na Myanmar. Tuombe amani. Vita daima ni kushindwa!"

Papa Francisko akisalimiana na mahujaji
Papa Francisko akisalimiana na mahujaji   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa pia alisema kwamba "Jana niliita, ninafanya kila siku, Parokia ya Gaza: walikuwa na furaha! Kuna watu 600 mle ndani, kati ya parokia na chuo. Na wakaniambia: "Leo tumekula dengu na kuku." Kitu ambacho hawakuzoea kufanya siku hizi: kwani walikuwa wanakula mboga mboga tu, na hivyo walifurahi! Lakini tuombe amani kwa ajili ya Gaza na sehemu nyingine nyingi za dunia. Vita daima ni kushindwa! Msisahau: vita ni kushindwa. Na ni nani anayefaidika na vita? Watengenezaji wa silaha. Tafadhali, tuombe amani. Hatimaye, mawazo yangu yanawaendea vijana, wagonjwa, wazee na waliofunga ndoa hivi karibuni.

Papa Francisko akisalimiana na wenye ndoa wapya
Papa Francisko akisalimiana na wenye ndoa wapya   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa Francisko vile vile ameeleza juu ya Juma la Kuombea Umoja wa Kikristo lililoanza tangu tarehe 18 Januari na litahitimishwa tarehe 25 Januari ikiwa Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Uongofu wa Mtakatifu Paulo Mtume wa Watu: “Katika siku hizi za maombi kwa ajili ya umoja wa Kikristo, ninawasihi tumwombe Mungu, Mmoja na Utatu, kwa ajili ya ushirika kamili wa wanafunzi wote wa Kristo!” Hatimaye ametoa Baraka zake kwa wote.

Baada ya Katekesi
22 Januari 2025, 12:22