Katekesi Kuhusu Utambuzi: Faraja ya Kweli Katika Maisha

Baba Mtakatifu Francisko amekazia: Faraja ya kweli kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya roho za waamini. Faraja inapaswa kujielekeza katika jambo jema kwa kumhakikishia mwamini amani na utulivu wa ndani. Jambo la msingi ni kufuata kanuni inayokuelekeza katika kutenda jambo jema, bila kupuuza dhamana na majukumu yao katika familia na jamii katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Utambuzi anasema hili ni zoezi linalofungamanishwa na: akili, ustadi na utashi kwa kusoma alama za nyakati, ili kutenda kwa busara na hekima. Utambuzi unagusia mahusiano ili kupata furaha ya kweli na kwamba hili ni zoezi gumu lakini la muhimu katika maisha, ikiwa kama linasaidiwa na hali halisi, ili kufanya upembuzi yakinifu. Baba Mtakatifu anasema, sala ni chombo muhimu sana kinachomwezesha mwamini kufanya utambuzi wa maisha ya kiroho na hivyo kumwezesha kumwendea Mungu kwa urahisi na katika hali ya kawaida ya maisha kama mtu anavyozungumza na rafiki yake mpendwa, kwa kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu na kutenda yale mambo yanayompendeza Mungu. Ukaribu na Mwenyezi Mungu unamwondolea mwamini hofu na woga na kwamba umuhimu wa sala na wa mwamini ni kujitambua jinsi walivyo, zoezi linalogusa na kukita mizizi yake katika milango ya ufahamu: kumbukumbu, akili, utashi, mahusiano na mafungamano na hivyo kumhakikishia mtu nafasi yake katika jamii inayomzunguka. Si rahisi sana kwa mtu kujitambua jinsi alivyo, kwani ni kawaida ya binadamu kutaka kuficha uhalisia wa maisha yake ya kiroho na kiutu. Katika mashaka ya maisha ya kiroho na kiwito, mara nyingi kunakosekana majadiliano ya kina kati ya maisha ya kiroho na mwelekeo wa kibinadamu; kati ya utambuzi na hisia.

Waamini wajitahidi kutafuta faraja ya kweli
Waamini wajitahidi kutafuta faraja ya kweli

Katika mchakato wa utambuzi, kuna matatizo na changamoto nyingi ambazo hazina budi kutambuliwa na kuchunguzwa. Hii si kwa sababu waamini hawamfahamu fika Mwenyezi Mungu, wala hawafahamu kusali vyema, bali ni kwa sababu hawajitambui vya kutosha, wala kujifahamu kikamilifu, mwanadamu katika hulka yake anapenda kujificha na kamwe hasijulikane si tu mbele ya wengine hata katika maisha yake binafsi. Kutokutambua uwepo angavu wa Mungu katika maisha ya mwanadamu ni kwa sababu ya ujinga na kutokutambua nafsi ya mtu na matamanio yake ya ndani. Kujitambua binafsi ni mchakato wa kuchimba undani wa mtu mwenyewe, ili hatimaye, kujitambua jinsi ulivyo, unavyotenda, mawazo yako na yale mambo msingi yanayokuongoza kufikiri na kutenda unayotenda. Walimu wa maisha ya kiroho wanasema “tamaa” ni ile hamu ya utimilifu na ishara ya uwepo wa Mungu ndani ya mwamini. “De-sidus” kwa lugha ya Kilatini maana yake ni “ukosefu wa nyota. Kumbe, “tamaa kimsingi ni ukosefu wa nyota na hatua ya kumbukumbu inayoongoza njia ya uzima; kwa kuibua mateso, na mapungufu katika hija ya maisha ya kiroho.

Faraja ya kweli ni kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha
Faraja ya kweli ni kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha

Tamaa ni dira na mwongozo katika safari ya maisha, inayomkirimia mwamini ujasiri wa kusonga mbele pasi na kukata tamaa. Tamaa ni kikolezo cha kujisadaka, ili kuweza kufikia lengo kamili pasi na kukata wala kujikatia tamaa. Kimsingi Baba Mtakatifu Francisko katika Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Utambuzi amekwisha kudadavua kwa kina na mapana kuhusu: Umuhimu wa sala, Utambuzi wa mtu binafsi na tamaa ya kutaka kupata utimilifu wa uwepo angavu wa Mungu katika maisha ya mwamini. Kila mwamini anapaswa kuzama katika mchakato wa kuandika historia ya kitabu cha maisha yake, kama kigezo msingi cha kufanya utambuzi. Lakini kwa bahati mbaya, watu wengi kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Augostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa wanaiandika na kuisoma historia ya maisha yao kwa kuchelewa sana kutambua uwepo angavu wa Mungu katika maisha ndani mwao. Baba Mtakatifu Francisko katika Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Utambuzi, amezungumzia pia kuhusu: Ukiwa, huzuni na majonzi moyoni. Amekazia umuhimu wa waamini kujifunza kusoma alama ya: Ukiwa, huzuni na majonzi moyoni. Ukiwa ni kikwazo katika kutenda mema na kamwe usithubutu kufanya mabadiliko katika maisha wakati ukiwa mkiwa, mwenye huzuni na majonzi moyoni.

Faraja ijielekeze katika kutenda mema
Faraja ijielekeze katika kutenda mema

Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mwendelezo wa Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Utambuzi, ameendelea kujielekeza zaidi kuhusu hali ya upweke, huzuni na majonzi. Umuhimu wa kutenda kwa kushirikiana na wengine, bila ya kusukumwa sana na hisia, ili kujenga ukomavu katika mahusiano na watu. Waamini wajifunze kumtafuta na hatimaye, kukaa na Kristo Yesu, ili kujenga mahusiano na mafungamano ya nguvu na ya dhati kabisa. Baba Mtakatifu anasema, upweke hasi, huzuni na majonzi moyoni, bila ya mtu kupata kishawishi cha kukimbia uhalisia wa maisha, inaweza kuwa ni fursa kwa mwamini kukua na kukomaa katika undani wa maisha yake. Hali kama hii inahitaji mwamini awe makini na aendelee kujikita katika hali ya unyenyekevu; mambo msingi hata katika maisha ya kiroho. Kinyume cha maelezo haya, mwamini anaweza kujikuta anapoteza utu na heshima yake kama binadamu. Upweke chanya kwa watakatifu wengi, imekuwa ni fursa ya toba na wongofu wa ndani, uliowasaidia kupata mwelekeo mpya wa maisha.

Nyenzo inayotumika ikusaidie kutenda mema
Nyenzo inayotumika ikusaidie kutenda mema

Baba Mtakatifu baada ya kupembua kwa kina na mapana kuhusu giza la maisha ya kiroho amesema, faraja ni nuru ya roho. Ni uzoefu wa furaha ya ndani, ambayo inaruhusu mtu kuona uwepo wa Mungu katika mambo yote; inaimarisha imani na matumaini, pamoja na uwezo wa kutenda mema. Mtu anayepata faraja hakati tamaa kwa urahisi anapokabiliana na matatizo pamoja na changamoto za maisha kwa sababu anapata amani yenye nguvu kuliko majaribu. Kwa hiyo faraja ni zawadi kubwa kwa maisha ya kiroho na maisha katika ujumla. Huu ni mwaliko kwa waamini kuitafuta na kuiambata ile faraja na furaha ya ndani. Baba Mtakatifu Francisko katika Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Utambuzi, Jumatano 30 Novemba 2022 amekazia kuhusu faraja ya kweli kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya roho za waamini. Faraja inapaswa kujielekeza zaidi katika jambo jema kwa kumhakikishia mwamini amani na utulivu wa ndani. Jambo la msingi ni kufuata kanuni inayokuelekeza katika kutenda jambo jema, bila kupuuza dhamana na majukumu yao katika familia na jamii katika ujumla wake. Pili nyenzo inayotumiwa na mwamini, imsaidie kutenda jambo jema na wala si kujitafuta mwenyewe kwa kuwadharau na kuwabeza wengine kama ilivyokuwa kwenye mfano wa Mfarisayo na Mtoza ushuru. Rej. Lk. 18:9-14.

Mang'amuzi ya maisha: Kanuni, Nyenzo na Hatima yake
Mang'amuzi ya maisha: Kanuni, Nyenzo na Hatima yake

Nyenzo inayotumiwa na mwamini haina budi kujikita katika fadhila ya unyenyekevu. Tatu ni hatima ya tendo linalotekelezwa na mwamini kwa kumwezesha kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Mwamini anapaswa kuchunguza vyema dhamiri yake, ili kuangalia kanuni inayomwongoza, nyenzo anazotumia na hatima ya matendo yake, ikiwa kama yanamsaidia kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu. Waamini watambue kwamba, wasipokuwa makini wanaweza kuambulia faraja ya Shetani, Ibilisi na hatimaye, kuwaondoa kabisa katika ile nia ya kutenda mema. Kumbe, kuna haja ya kujikita katika ukweli wa mawazo yako, ndilo “Neno la Siri” au “Password” ya kuingia katika undani wa maisha yako. Ili kuweza kupata mafanikio katika safari ya maisha ya kiroho, kuna haja ya kuchunguza dhamiri kila siku ili kutambua neema ya Mungu inayotenda kazi ndani mwako kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Faraja ya kweli ni kielelezo cha mwamini kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake, kwa kutafuta kile kilicho chema. Mwamini awe makini kuchunguza mizizi ya mambo yanayokwamisha ukuaji wake wa maisha ya kiroho na mafungamano na jirani zake, kwa msaada wa Roho Mtakatifu.

Faraja ya Kweli
30 November 2022, 17:17

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >