Rais Samia Suluhu Hassan Akutana na Kuzungumza na Maaskofu Katoliki Tanzania
Na Ikulu, Chamwino, - Dodoma, Tanzania.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Chamwino, Dodoma inasema kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan, Jumatatu tarehe 10 Agosti 2026 amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, “Tanzania Episcopal Conference, TEC,” Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma.
Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na kujadili masuala mbalimbali ya kitaifa yanayogusia jamii, yakiwemo ya kisiasa, imani na maendeleo, pamoja na kuimarisha amani, mshikamano na kujenga mustakabali mwema wa Taifa.
Aidha mazungumzo hayo yaligusia umuhimu wa nafasi ya madhehebu na viongozi wa dini katika kulea jamii yenye maadili mema, uwajibikaji na mshikamano, ikiwa ni sehemu ya mchango wao katika ustawi na maendeleo endelevu ya Taifa. Mheshimiwa Rais aliwashukuru Maaskofu hao kwa kuona umuhimu wa kukutana na kujadiliana naye masuala yenye tija kwa Taifa na kuwahakikishia dhamira yake ya kuendeleza utamaduni wa kushauriana na kushirikiana na viongozi wa dini na makundi mbalimbali katika jamii kuhusu masuala muhimu ya kitaifa kila inapohitajika.