Tafuta

2026.07.29 Sr Abby Avellino katikati na Watawa wengine wa Mtandao wa Talitha Kum Kimatiaifa: 2026.07.29 Sr Abby Avellino katikati na Watawa wengine wa Mtandao wa Talitha Kum Kimatiaifa:  (Talitha Kum International)

Nyuma ya ulaghai:Kurejesha hadhi ya binadamu na matumaini kwa manusura wa biashara haramu ya binadamu

Katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa Dhidi ya Biashara Haramu wa Binadamu 2026 kwa kaulimbiu:"Tumenaswa nyuma ya ulaghai,"Mratibu wa Kimataifa wa Talitha Kum,mtandao wa kimataifa wa Watawa Dhidi ya Biashara Haramu ya Binadamu,amenatuletea historia ya kawaida sana ya wakati wetu na mvuto wa kuunganisha mitandao ya matumaini,amani,uhuru na haki ili mtu yeyote asitendewe kama bidhaa.

Na Sr Abby Avellino,MM.

Biashara haramu ya binadamu inaendelea kujibadilisha katika aina mpya. Kadri teknolojia inavyoendelea, wafanyabiashara haramu pia hubadilika, kwa kutumia mitandao ya kijamii, majukwaa ya mtandaoni, na mikakati ya udanganyifu ya kuajiri ili kuwanyonya watu wanaotafuta fursa bora. Ofa ya kazi inayoahidi matumaini na mustakabali inaweza kuwa njia ya kuelekea hofu, unyanyasaji, na unyonyaji. Na mfano wa historia ya Ayu [1] ni kuhusu ukweli huu mchungu. Ayu aliondoka Indonesia baada ya kukubali kile alichoamini kuwa ofa halisi ya kazi kutoka kwa rafiki anayemwamini, na kisha akawa mwathirika wa biashara haramu ya binadamu nchini Ufilipino. Alisafirishwa hadi katika eneo la utapeli mtandaoni, ambapo alilazimika kufanya kazi chini ya woga wa kila mara, huku walinzi waliokuwa na silaha wakifanya ugumu wa uwezekano wa kutoroka.

Alishuhudia wengine wengi wakivumilia vitisho, vurugu, na unyanyasaji wa kihisia kabla ya kuokolewa kupitia ushirikiano wa mitandao ya Talitha Kum nchini Indonesia na Ufilipino, pamoja na Tume ya Kimataifa ya Haki (IJM), na kuanza safari yake ya uponyaji. Leo hii, yeye ni mtetezi aliyenusurika, akitumia sauti yake kuonesha  ukweli uliopo wa biashara haramu ya binadamu na kusaidia kuzuia wengine kutokana na unyonyaji huo. Uzoefu wake unaonesha ukweli mchungu uliofichwa nyuma ya ulimwengu wa kidijitali. Nyuma ya kila ujumbe wa ulaghai, mpango wa uongo wa uwekezaji, au ulaghai mtandaoni, kunaweza kuwa na mtu ambaye uhuru wake umechukuliwa, mwanamke au mwanamume aliyedanganywa na ahadi za uongo, aliyesafirishwa nje ya mipaka, na kulazimishwa na mitandao ya uhalifu kufanya shughuli haramu. Katika Siku hii ya Kimataifa  Dhidi ya Biashara Haramu ya Binadamu kwa  2026, kaulimbiu : "Wamenaswa Nyuma ya Ulaghai" inatualika kutazama zaidi ya skrini na kutambua wanadamu waliojificha nyuma ya uhalifu mtandaoni. Watu wengi walionaswa katika misombo ya ulaghai si wahalifu. Ni waathiriwa wa usafirishaji haramu ambao hadhi, uhuru, na ndoto zao zimeibwa.

Kama Talitha Kum, mtandao wa kimataifa wa Masista Wakatoliki waliojitolea kukomesha biashara haramu ya binadamu na aina zote za unyonyaji, tunasimama na manusura na kutembea nao kuelekea uponyaji, haki, na urejesho. Tunasikiliza historia zao, tunasindikizana nao katika safari zao, na kuthibitisha hadhi ambayo hakuna aina yoyote ya unyonyaji inayoweza kuondoa. Utume huu umeoneshwa na wito wa Papa Leo XIV katika Waraka wake wa Magnifica Humanitas, [2] kutukumbusha kwamba utu wa binadamu lazima ubaki katikati ya kila maendeleo ya kijamii, kiuchumi, na kiteknolojia. Kazi si njia tu ya kujipatia riziki; ni usemi wa utu wa binadamu, ushiriki katika kazi ya ubunifu ya Mungu, na mchango kwa manufaa ya wote. Leo hii, mabadiliko ya kidijitali na akili unde  hutoa fursa kubwa kwa binadamu. Hata hivyo, teknolojia lazima itumike kumtumikia binadamu kila wakati. Haipaswi kamwe kuwa chombo kinachowashusha watu hadi kuwa vyombo vya kuzalisha faida au unyonyaji. Ukweli wa uhalifu wa kulazimishwa katika shughuli za ulaghai ni ukiukwaji mkubwa wa hadhi ya kazi. Watu wanaosafirishwa kibiashara hunyimwa uhuru wao, uwezo wao unanyonywa, na ubinadamu wao unanyimwa. Wanatendewa kama bidhaa badala ya kuonekana kama watu walioumbwa kwa mfano na sura ya Mungu.


Katika Talitha Kum, tunaendelea kukemea biashara haramu ya binadamu kwa uhalifu wa kulazimishwa kama ukiukaji mkubwa wa utu wa binadamu. Mwitikio wetu unazidi uokoaji. Kupitia kinga, usindikizaji wa walionusurika, ushirikiano, na utetezi. Tunafanya kazi na jamii, serikali, mashirika ya kimataifa, asasi za kiraia, na vijana kushughulikia sababu kuu za biashara haramu ya binadamu na kuunda njia kuelekea uhuru na matumaini. Vijana wameunganishwa sana na ulimwengu wa kidijitali, ambao huunda fursa na hatari mpya za udanganyifu na unyonyaji. Kwa sababu hiyo, kinga na elimu ni muhimu. Hata hivyo vijana siyo   kwamba wako katika hatari tu; pia wao ni sehemu ya suluhisho. Kwa ubunifu wao, nguvu, na ushawishi miongoni mwa wenzao, wanaweza kuwa viongozi katika kukuza uelewa na kujenga utamaduni wa kuzuia. Kwa kutembea nao na kuwawezesha kwa maarifa, maadili, na uwajibikaji, tunatambua uwezo wao wa kujilinda na kuwalinda wengine ndani ya jamii zao. Tumehamasishwa na kujitolea kwa Mabalozi wa Vijana wa Talitha Kum, ambao huongeza uelewa miongoni mwa wenzao na kukuza utamaduni wa kidijitali uliojengwa juu ya ukweli, mshikamano, uwajibikaji, na heshima kwa utu wa binadamu.

Mwaka wa 2025, mtandao wa kimataifa wa Talitha Kum ulifikia zaidi ya watu milioni 1.2 kupitia kinga, ulinzi, utetezi, mitandao, na usindikizaji wa walionusurika. Nyuma ya kila namba kuna mtu: mwathirika anayepata uhuru tena, kijana anayeongoza mabadiliko, familia inayopata tumaini, au jamii inayochagua mshikamano. Matokeo haya yanawezeshwa na kujitolea kwa maelfu ya Masista Wakatoliki, mapadre, vijana viongozi, watetezi wa mwathirika, na washirika duniani kote ambao hubadilisha huruma kuwa hatua halisi. Hata hivyo, changamoto nyingi zinabaki, na kazi yetu ni ya haraka zaidi kuliko hapo awali. Waathirika wanaendelea kukabiliana na safari ngumu wanapojenga upya maisha yao na kutafuta fursa za mustakabali salama na imara zaidi. Kama mwathirika mmoja kijana kutoka Afrika alivyoshirikisha kuwa: "Kwa sasa, changamoto yangu kuu ni kwamba sina kazi au shughuli yoyote thabiti ya kujikimu. Ninajaribu niwezavyo kupata fursa na kujenga upya maisha yangu."

Maneno yake yanatukumbusha kwamba biashara haramu ya binadamu si kitendo cha jinai tu; pia ni ukiukwaji wa utu wa binadamu unaofichua ukosefu wa usawa wa kijamii na kiuchumi unaohitaji mwitikio wetu wa pamoja. Uhuru kutokana na unyonyaji ni mwanzo tu. Wanusurika wanahitaji fursa, usindikizaji, jamii zinazounga mkono, na wanatumaini kujenga upya maisha na utu wao kikamilifu. Katika Siku hii ya Kimataifa Dhidi ya Biashara Haramu ya Binadamu, na tujitolee kufichua kilichofichwa nyuma ya ulaghai, kusikiliza sauti za wanusurika, na kutetea utu wa kila mtu ambaye amenyonywa. Tuendelee kujenga ulimwengu ambapo teknolojia inahudumia ubinadamu, kazi inarejesha hadhi, na hakuna mtu anayetendewa kama bidhaa. Kwa pamoja, tuunganishe mitandao ya matumaini, amani, uhuru, na haki, ili kila mtu aweze kuishi kwa hadhi, ulinzi, upendo, na amani anayostahili.

* Sr. Abby Avelino, MM, Mratibu wa Kimataifa wa Mtanadao wa Talitha Kum

----------

[1] The survivor’s name has been changed to protect her identity.

[2] Pope Leo XIV, "Safeguarding Humanity at a Time of Transformation", Magnifica Humanitas (148-156).https://www.vatican.va/content/leo-xiv/en/encyclicals/documents/20260515-magnifica-humanitas.html

Ushuhuda wa Mratibu wa Talitha Kum

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.

30 Julai 2026, 16:40