Talitha Kum yapanua mtandao wake.Waathiriwa milioni 50 wa biashara haramu ya binadamu
Na Stefano Leszczynski – Vatican.
Biashara haramu ya binadamu inaendelea kuwa moja ya ukiukwaji mkubwa zaidi wa utu wa binadamu. Kulingana na makadirio ya Shirika la Kazi Duniani na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, inasadikika watu milioni 50 wanaishi katika hali ya utumwa mamboleo, huku biashara haramu ya binadamu na aina zinazohusiana za unyonyaji zikizalisha faida haramu ya dola bilioni 236 kila mwaka. Ni kutokana na hali hii kwamba, katika hafla ya Siku ya Dunia ya Kupinga Biashara Haramu ya Binadamu, (Julai 30)Talitha Kum iliwasilisha Ripoti yake ya Mwaka 2025, ambayo inaakisi dhamira inayoongezeka ya mtandao wa kimataifa unaoendelezwa na Umoja wa Kimataifa wa Mama Wakuu wa Watawa (UISG) kupambana na jambo hili linaloendelea kubadilika.
Mtandao wa kimataifa unaozidi kuenea
Katika mwaka mzima wa 2025, Talitha Kum ilifikia watu milioni 1.21, ongezeko la 29.6% zaidi ya mwaka uliopita, kupitia shughuli za kuzuia, usaidizi kwa manusura, upatikanaji wa haki, utetezi, na ushirikiano wa kimataifa. "Nyuma ya kila namba kuna mtu, familia, na jamii," ripoti inasema. "Takwimu hizi zinawakilisha maisha yaliyofikiwa, jamii zilizohamasishwa, na matumaini ya kurejeshwa." Mtandao huo kwa sasa unafanya kazi kupitia mitandao 68 ya kitaifa katika nchi 113 na unahusisha watawa na washirika 6,387, pamoja na mashirika ya kitawa ya wanawake 882 na mashirika ya kitawa 100 ya wanaume, ishara ya ushiriki mpana wa Kanisa katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu.
![]()
Uwakilishi wa Ripoti ya Mwaka ya Talitha Kum
Kinga inabaki kuwa dawa ya kwanza
Kinga inaendelea kuwa eneo kuu la uingiliaji kati, huku watu 928,972 wakifikiwa mwaka 2025, wakiwemo wanawake na wasichana zaidi ya 303,000 na watoto 262,000, kutokana na kampeni katika shule, parokia, vituo vya afya, vyombo vya habari vya kijadi, na mitandao ya kijamii. Wakati huo huo, manusura 27,329 walipokea ulinzi na usaidizi kupitia makazi, usaidizi wa kimatibabu na kisaikolojia, ushauri nasaha wa kisheria, na programu za mafunzo na ujumuishaji upya. Ripoti pia inaakisi ongezeko kubwa la hatua za kukuza upatikanaji wa haki, ambazo zilifikia watu 7,141, ongezeko la 72.4% ikilinganishwa na 2024.
![]()
Vijana Mabalozi wa Talitha Kum
Wanawake, watoto, na wahamiaji wanabaki kuwa waathiriwa wakuu
Takwimu kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) inathibitisha kiwango cha kimataifa cha tukio hili. Wanawake na wasichana wanaendelea kuwakilisha idadi kubwa ya waathiriwa waliotambuliwa, huku 60% ya wanawake vijana wakinyanyaswa kingono. Miongoni mwa watoto waliotambuliwa, 45% ni waathiriwa wa kazi za kulazimishwa, na karibu nusu wanahusika katika aina zingine za unyonyaji, kama vile kuombaomba au uhalifu wa kulazimishwa. Katika maeneo kadhaa ya dunia, kazi za kulazimishwa, ambazo sasa zinachangia 42% ya visa vilivyotambuliwa, zimezidi hata unyonyaji wa kingono kama lengo kuu la biashara haramu ya binadamu.
Mitego Mipya ya Uhalifu wa Kidijitali
Mageuko ya jambo hili yanahusiana kwa karibu na maendeleo ya teknolojia za kidijitali. Kulingana na UNODC, mashirika ya uhalifu yanatumia mitandao ya kijamii, majukwaa ya mtandaoni, na ofa za uongo za kazi ili kuwaajiri waathiriwa, ambao kisha wanalazimishwa kushiriki katika ulaghai wa kiteknolojia wa hali ya juu. Haya ni mabadiliko ambayo Sr Abby Avelino, mratibu wa kimataifa wa Talitha Kum, anaona kila siku. "Usafirishaji haramu wa binadamu unaongezeka kwa njia ngumu zaidi," alisema katika mahojiano na vyombo vya habari vya Vatican. "Waathirika wengi tunaokutana nao wamenaswa kupitia majukwaa ya kidijitali." Waathiriwa wanaelezea kushawishiwa na ahadi za ajira zinazopatikana mtandaoni; mara tu wanapofika mahali wanapokwenda, wanagundua kuwa hakuna kazi inayopatikana, hati zao zinachukuliwa, na uwezekano wowote wa kutoroka unazuiwa. "Huu ndio mwelekeo wa sasa: majukwaa ya kidijitali yanatumiwa na mashirika ya uhalifu kuvutia vijana, ambao wanatafuta mustakabali bora na kazi nzuri yenye hadhi"
![]()
Wata wa Afrika Kusini wa Mtandao wa Talitha Kum
Kuanzia Usaidizi hadi Kuzaliwa Upya
Ili kukabiliana na aina hizi mpya za unyonyaji, Talitha Kum inawekeza katika mafunzo ya vijana kupitia programu ya Mabalozi wa Vijana, ikihamasisha kampeni za uhamasishaji kwenye mitandao ya kijamii, radio, na televisheni. Lakini kiini cha mwitikio kinabaki kuwaunga mkono manusura. "Sio tu kuhusu kuwaokoa watu," alisisitiza Sr Abby. Lazima tuwape manusura nafasi ya kuelezea mahitaji yao, kuunda fursa, na kuhakikisha usaidizi unaoendelea na endelevu kweli." Mbinu hii inawatambua waathiriwa kama wahusika wakuu wa safari yao ya kuzaliwa upya na sehemu muhimu ya suluhisho.
Kushughulikia Sababu za Msingi za Unyonyaji
Kwa mratibu wa kimataifa wa mtandao huo, kupambana na biashara haramu ya binadamu pia kunahitaji mabadiliko ya kimuundo. "Watu huhama kwa sababu ya umaskini. Huhama kwa sababu ya ukosefu wa usawa. Wanahama kwa sababu ya migogoro. Hii ndiyo sababu lazima tuhapambane ili kujenga ulimwengu usio na biashara haramu ya binadamu," alisema. Vita, migogoro ya hali ya tabianch, kutokuwa na utulivu wa kisiasa, na uhamiaji wa kulazimishwa vinaendelea kuongeza udhaifu wa mamilioni ya watu, na kuwafanya kuwa mawindo rahisi kwa mitandao ya uhalifu, kama inavyothibitishwa na uchambuzi wa shirika maalum la Umoja wa Mataifa. Kwa sababu hiiyo Sr Abby Avelino alihitimisha, elimu inabaki kuwa mojawapo ya zana bora zaidi. "Hata watoto, kuanzia umri mdogo sana, lazima wajifunze jinsi biashara haramu ya binadamu inavyoenea," kwa sababu ni utamaduni imara wa kuzuia, pamoja na kujitolea kwa taasisi, asasi za kiraia, na jumuiya za Kanisa, ndiyo unaoweza kuvunja mzunguko wa unyonyaji.
Imesasishwa tarehe 30 Julai 2025 na Angella Rwezaula
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.