Tafuta

Mgogoro mkubwa huko Sudan. Mgogoro mkubwa huko Sudan. 

Hakuna usalama wa kuchota maji:Wanawake Sudan wakimbia droni mchana na ubakaji usiku

Kwa wanawake na wasichana katika mji wa El Obeid nchini Sudan,hata kitendo cha kwenda kuchota maji sasa kimegeuka kuwa safari ya kuamua kati ya uhai na kifo kwa sababu ya ngeze zisizo n arubani,wakati usiku,wanabakwa.

Umoja wa Mataifa (UN).

Katika hali halisi ya mgogoro unaondelea katika maeneo mengi nchini Sudan, Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake, UN Women, linasema mashambulizi ya droni yanayolenga maeneo ya kuchota maji mchana yamewalazimu wanawake wengi kusubiri hadi usiku ili kuchota maji, wakiamini giza litawalinda dhidi ya mashambulizi ya angani. Japokuwa tena usiku huo huo hukumbana na unyanyasaji, ubakaji na aina nyingine za ukatili wa kingono. Kutokana na hilo UN Women inaonya kuwa hali hiyo inafanana na matukio yaliyoshuhudiwa mwaka 2025  kwenye mjini wa El Fasher, huku ikisema, “Hakuna tena muda salama kwa wanawake na wasichana wa  kupata maji.”

Visa vya kipindupindu mwanzoni mwa Julai

Wakati wananchi wa nchi hiyo wakiendelea kukumbana na hayo ya vita, msimu wa mvua unaotarajiwa kufikia kilele mwezi ujao wa Agosti  hali hiyo  inaongeza hofu ya kuenea kwa magonjwa yanayosababishwa na maji machafu. Shirika la Umoja wa Mataifa Afya Duniani (WHO) limesharekodi visa 1,330 vya kipindupindu mwanzoni mwa Julai, huku utapiamlo na ukosefu wa huduma za afya vikiongeza hatari ya wanawake na wasichana kuugua na kufariki.

Ukatili wa kikogono unaendelea kutumika kama silaha katika vita

Kwa mujibu wa UN Women, ukatili wa kingono umeendelea kutumika kama silaha katika vita vya Sudan vilivyodumu kwa miaka mitatu. Idadi ya wanawake na wasichana wanaohitaji huduma za kukabiliana na ukatili wa kijinsia imeongezeka mara nne tangu vita kuanza na sasa inakadiriwa kufikia milioni 12.7 mwaka 2026. Hata hivyo, mashirika ya wanawake yaliyo mstari wa mbele kuwasaidia waathirika yanaendelea kudhoofishwa na upungufu wa fedha. Takribani theluthi mbili ya mashirika hayo yanasema vituo salama na huduma za waathirika zimefungwa au kupunguzwa kwa kiasi kikubwa, huku nusu yakihofia kusitisha shughuli zake ndani ya mwaka mmoja bila msaada wa haraka wa kifedha.

Wito wa UN Womne ni Sitisheni mapigano ili kuhakikisha misaada inafika

UN Women imetoa wito wa “kusitishwa mara moja kwa mapigano”, kuhakikisha misaada ya kibinadamu inafika bila vikwazo, kulindwa kwa wanawake na wasichana, wahusika wa ukiukwaji kuwajibishwa, na manusura kupata haki pamoja na huduma zote muhimu za kuwasaidia. Pia imesisitiza kuwa wanawake wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika mazungumzo ya amani na juhudi za kuijenga upya Sudan.

Imesasishwa tarehe 28 Julai 2026 saa 10:17 jioni na Angella Rwezaula.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

 

 

28 Julai 2026, 16:17