UN:mabadiliko ya tabianchi yaathiri watu milioni 13 barani Afrika 2025
Umoja wa Mataifa.
Shirika la Umoja wa Mataifa la utabiri wa Hali ya Hewa Duniani (WMO), limesema juu ya matukio mabaya ya hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi yaliyoathiri takriban watu milioni 13 barani Afrika kwa mwaka 2025 na kusababisha vifo zaidi ya watu 3,000 huku athari zake zikigusa sekta zote za uchumi na maisha ya jamii. Ripoti mpya ya shirika: “Hali ya Tabianchi Afrika 2025” iliyotolewa tarehe 18 Juni 2026 mjini Geneva Uswiss ilieleza kuwa mafuriko yalikuwa janga lililoripotiwa zaidi, huku yakisababisha hasara kubwa za kiuchumi na kibinadamu na yakichangia zaidi ya nusu ya matukio yote ya hali mbaya ya hewa yaliyorekodiwa barani humo.
Afrika bado ina pengo kubwa katika mifumo ya tahadhari za mapema
WMO ilisisitiza kuwa Afrika bado ina pengo kubwa katika mifumo ya tahadhari za mapema, ingawa maendeleo yanaendelea kufanyika. Nchini Nigeria, mafuriko makubwa mwezi Mei yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 200, huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, ikishuhudia zaidi ya watu 160 wakifariki kutokana na mafuriko mwezi Aprili.
Afrika inazidi kupashwa joto kwa kasi
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Afrika sasa inapashwa joto kwa kasi zaidi kuliko wastani wa dunia. Kiwango cha ongezeko la joto tangu mwaka 1991 ni kikubwa zaidi kuliko kipindi chochote cha miaka 30 kilichopita. WMO imeeleza kuwa mwaka 2025 ulikuwa miongoni mwa miaka yenye joto kali zaidi kuwahi kurekodiwa barani humo. Ukame uliathiri zaidi ya watu milioni 8.5 katika eneo la Afrika Mashariki, huku msimu wa vimbunga katika Bahari ya Hindi Kusini ukiwa miongoni mwa misimu yenye shughuli nyingi zaidi katika miaka ya hivi karibuni
Mlima Kilimanjaro wapoteza barafu zake
Ripoti hiyo pia imeonya kuwa barafu za Afrika zinaendelea kutoweka kwa kasi na kuwa barafu katika maeneo ya milima ya Afrika, ikiwemo Mlima Kilimanjaro, inaendelea kuyeyuka kwa kasi, wakati kina cha bahari katika baadhi ya maeneo ya pwani kikipanda kwa kiwango kikubwa kuliko wastani wa dunia. Tangu mwishoni mwa karne ya 19, bara hilo limepoteza zaidi ya asilimia 90 ya eneo lake la barafu. Katika Mlima Kilimanjaro nchini Tanzania, eneo la barafu limepungua kutoka kilomita za mraba 11.4 mwaka 1900 hadi chini ya kilomita moja ya mraba katika miaka ya karibuni. Wakati huo huo, kina cha bahari katika baadhi ya maeneo ya pwani za Afrika kinaongezeka kwa kasi zaidi kuliko wastani wa dunia, hali inayoongeza hatari kwa makazi, miundombinu na maisha ya watu wanaoishi katika maeneo ya mwambao.
Tahadhari za mapema bado ni changamoto
Licha ya hatari zinazoongezeka, ni asilimia 40 pekee ya nchi za Afrika zilizo na mifumo ya tahadhari za mapema kwa majanga mbalimbali, jambo ambalo WMO inasema linaweka maisha na riziki za mamilioni ya watu katika hatari. Hata hivyo, ripoti ilibainisha mafanikio yanayoonekana kupitia ushirikiano bora kati ya huduma za hali ya hewa, mamlaka za usimamizi wa majanga na serikali za mitaa, pamoja na matumizi ya huduma za tabianchi kama utabiri wa misimu. “Dalili za mabadiliko ya tabianchi zinaonekana wazi kote Afrika kuanzia ongezeko la joto, kupanda kwa kina cha bahari hadi mafuriko na ukame wenye madhara makubwa.
Ripoti hii inaonesha si tu ukubwa wa hatari hizi, bali pia umuhimu unaoongezeka wa mifumo ya tahadhari za mapema, huduma za tabianchi na hatua za pamoja za kulinda maisha na riziki za watu,” alisema Katibu Mkuu wa WMO, Celeste Saulo. WMO ilisisitiza kuwa uwekezaji zaidi katika mifumo ya tahadhari za mapema na huduma za hali ya hewa ni muhimu ili kusaidia Afrika kukabiliana na athari zinazoongezeka za mabadiliko ya tabianchi.
Imesasishwa saa 4.45 tarehe 19 Juni 2026 na Angella Rwezaula
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here