Tafuta

2025.10.23 Mfalme Charles III akiwa na Papa Leo XIV na Malkia Camilla wakati wa ziara yao mjini Vatican  Oktoba 2025 . 2025.10.23 Mfalme Charles III akiwa na Papa Leo XIV na Malkia Camilla wakati wa ziara yao mjini Vatican Oktoba 2025 .  (@Vatican Media)

Mfalme Charles ampongeza Papa Leo XIV kutimiza mwaka I tangu kuchaguliwa kwake!

Mfalme Charles III wa Uingereza amempongeza Papa Leo XIV kwa ajili ya maadhimisho ya kwanza ya kuchaguliwa kwake kunako Mei 8,2025,akithibitisha tena kujitolea kwa Uingereza kuimarisha uhusiano na Vatican na kushirikiana katika changamoto za kimataifa ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi na ujenzi wa amani.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Mfalme Charles alikumbuka mkutano wake na Papa Leo XIV wakati wa Ziara ya Kiserikali ya wanandoa wa kifalme katika Kiti Kitakatifu mnamo 23 Oktoba 2025, akielezea kama "wakati wa umuhimu mkubwa" kibinafsi na kwa uhusiano kati ya mataifa na imani hizo mbili. Alikumbusha hayo katika fursa ya kumtakia matashi mema ya kutimiza mwaka mmoja tangu achaguliwe kuwa Kharifa wa Mtume Petro, kunako tarehe 8 Mei 2025, katika ujumbe uliochapishwa na Ubalozi wa Uingereza unaowakilisha Nchi yake mjini Vatican.

Papa alipokutana na wafalme wa Uingereza na ujumbe wao Oktoba 2025
Papa alipokutana na wafalme wa Uingereza na ujumbe wao Oktoba 2025   (@Vatican Media)

Katika ujumbe huo Mfalme wa Uingereza anaandika kuwa: "Siku hii ni fursa muhimu ya kutafakari urafiki wa kudumu kati ya mataifa yetu.  Mimi na mke wangu tunakumbuka, kwa upendo mkubwa, mkutano na Baba Mtakatifu wakati wa Ziara yetu ya Kiserikali katika Kiti Kitakatifu mnamo Oktoba 2025; wakati wa umuhimu mkubwa kwetu binafsi na kwa uhusiano kati ya mataifa na imani zetu husika."

Utetezi wa masuala ya Tabianchi

Mfalme wa Uingereza pia alisifu utetezi wa Papa Leo XIV kuhusu masuala ya hali ya Tabianchi akibainisha kuwa ubinadamu una jukumu la pamoja la kulinda sayari kwa vizazi vijavyo. “Tunapokabiliana na changamoto za pamoja za wakati wetu, hasa zile zinazohusu hali ya tabianchi na uhifadhi wa ulimwengu wetu wa asili, nina matumaini katika utetezi wako unaoendelea wa kushughulikia mabadiliko ya hali ya tabianchi kama suala la kimaadili na kiroho.” Mkuu huyo wa Uingereza aidha alibainisha “Sote ni walinzi wa sayari yetu ya thamani tukiwa na wajibu kwa vizazi vijavyo, kwa mujibu wa uumbaji wa Mungu.”

Ushirikiano Endelevu kati ya Uingereza na Vatican

Kwa njia hiyo, Mfalme Charles alionesha matumaini zaidi kwamba dini na sayansi zitaendelea kuhamasisha “hatua zenye mwanga na mabadiliko” katika kutafuta amani. Aliongeza kuwa Uingereza inaendelea kuwa na matumaini ya ushirikiano endelevu na Kiti Kitakatifu kuelekea kufikia “suluhisho zenye maana na za kudumu” kwa changamoto za kimataifa. Kwa kuhitimisha Mfalme Charles alibainisha kuwa “Mimi na mke wangu tunakuhakikishia Baba Mtakatifu  maombi yetu ya amani, ustawi na ustawi katika mwaka ujao.”

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

08 Mei 2026, 13:00