UNICEF:Watoto milioni 7.5 huko Sahel ya Kati wanahitaji msaada wa kibinadamu
Na Angella Rwezaula–Vatican.
Shirika la Umoja wa Mataifa limerekodi zaidi ya ukiukwaji mkubwa 1,500, ikiwa ni pamoja na mauaji, utekaji nyara, kuajiri, na matumizi ya watoto na vikundi vyenye silaha, huku zaidi ya shule 8,400 zikizuiwa kufikiwa mwaka 2025 pekee katika Ukanda wa Sahel. Baada ya misheni ya siku 14 katika Sahel ya Kati yote “niliona eneo lenye uwezo mkubwa, lakini likiendelea kukabiliwa na ukosefu wa usalama, mishtuko ya tabianchi, na misukosuko ya kijamii na kiuchumi.” Haya yalisemwa katika taarifa ya Ted Chaiban, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Nchini Niger, Burkina Faso na Mali.
Watoto milioni 7.5 wanahitaji msaada
Ripoti za vurugu nchini Mali katika siku za hivi karibuni “ni ushuhuda zaidi wa jinsi misukosuko kama hiyo katika eneo hilo inavyosababisha hali hatarishi sana kwa watoto, ambao kwa bahati mbaya pia husababisha vifo vyao. Katika Sahel ya Kati yote, karibu watoto milioni 7.5 wanahitaji msaada wa dharura wa kibinadamu: dharura ambayo bado iko mbali sana na umakini wa jumuiya ya kimataifa.” Kwa njia hiyo “Maafisa wa serikali, viongozi wa jamii, na watu waliohamishwa nchini Niger, Burkina Faso, na Mali, ambapo vurugu na kulazimishwa kuhama zimevuruga maisha ya zaidi ya watu milioni 3.6, wanaendelea kutoa matumaini, licha ya kila kitu.”
Sera za kuwaka kizazi kijacho katikati ya sera za kitaifa
Katika maeneo mengi ya vijijini, masoko yanafunguliwa tena, jamii zinaendelea kusaidiana, na watoto wanacheza, huku familia na vijana wakitarajia kupata tena heshima yao na uhuru wao wa kiuchumi. Kwa mujibu wa Taarifa yake Ted Chaiban, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Nchini Niger, alibainisha kuwa, “Nilikutana na wadau muhimu katika nchi hizo tatu, na mamlaka zilikubaliana kuhusu umuhimu wa kuwekeza katika rasilimali watu na kuimarisha mshikamano wa kijamii, nguzo muhimu kwa utulivu na maendeleo. Tamaa dhahiri inajitokeza kila mahali: kuweka kizazi kijacho katikati ya sera za kitaifa. Nilitiwa moyo na dhamira kubwa ya serikali hizo tatu katika kukuza na kulinda haki za kila mtoto.”
Nchini Niger
Katika taarifa hiyo aidha alifafanua kuwa “Kwa mfano, nchini Niger, mageuzi yanayofadhiliwa na serikali yameboresha mfumo wa usajili wa raia katika zaidi ya nusu ya manispaa za nchi hiyo, na kuongeza viwango vya usajili wa kuzaliwa kutoka 62% mwaka wa 2023 hadi 79% mwaka wa 2025 na kuanzisha usajili wa raia kidijitali kama kichocheo muhimu cha ugatuzi wa madaraka na utoaji jumuishi wa huduma za ndani. Nchini Burkina Faso, ahadi hii inaonyeshwa katika mgao wa takriban 25% ya bajeti ya taifa kwa elimu na karibu 12% kwa afya, ikionyesha juhudi kubwa ya kuimarisha huduma muhimu za kijamii.”
Nchini Mali
Vile vile kuwa “Nchini Mali, chanjo ya kitaifa ilifikia 82% mwaka wa 2024, ikileta nchi karibu na lengo la kumlinda kila mtoto kwa chanjo zinazookoa maisha. Sera na ahadi hizi si mifano mizuri tu; zinachukua maana yake kamili tunaposhuhudia mabadiliko chanya ya maisha ya kila siku ya watoto, na kuwawezesha kusonga mbele licha ya matatizo wanayokabiliana nayo. Mzunguko wa vurugu unabaki kuwa dhahiri kwa hatari, na hali kwa watoto ni ya kutisha sana.”
Ikiukaji mkubwa
“Ukosefu wa elimu na huduma muhimu huwaweka katika hatari ya magonjwa na dhiki ya kisaikolojia na kuhatarisha fursa zao za maendeleo kamili na yenye afya. Kulea watoto katika vurugu si chaguo endelevu kwa maendeleo ya kijamii na ukuaji wa uchumi wa muda mrefu.” “Kila mtu niliyekutana naye wakati wa ziara yangu alishiriki wasiwasi uleule” aliongeza wa: “kutoa ulinzi bora kwa watoto na familia, kurejesha amani, kuwezesha upatikanaji wa huduma za afya na elimu, na kuhakikisha kurudi nyumbani salama.” Kadhalika alisema: “pia nilitiwa moyo kuona timu za UNICEF zikifanya kazi kila siku kulinda haki za kila mtoto, haswa walio hatarini zaidi, katika eneo lote la Sahel.
Duni haipaswi kufumbia macho suala la watoto huko Sahel
Timu hizo zinasaidia serikali kuunga mkono mifumo ya utoaji wa afya, maji, elimu, na ulinzi wa kijamii, kuimarisha uwezo wa ndani, na kusaidia nchi kupata suluhisho bunifu kwa matatizo yanayoonekana kuwa magumu.” Mwakilishi huyo wa Unicef hakuhishia hapo bali anabainisha kuwa “Niliona kwamba mwitikio wetu unafaa zaidi wakati unajenga ustahimilivu kwa kuimarisha mifumo ya ndani, kuwawezesha jamii, na kukuza utawala jumuishi, kila wakati kuhakikisha kwamba sauti za watoto zinasikika na kuzingatiwa. Dunia haipaswi kufumbia macho ustahimilivu wa watoto huko Sahel; Bado kuna mamilioni ya watoto wenye mahitaji ya dharura ya kibinadamu ambao wanahitaji uingiliaji kati wa haraka. Ustahimilivu wao haimaanishi kuwa wako vizuri, wala haupaswi kutumika kama kisingizio cha kutochukua hatua.”
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here