Tafuta

Tangu mamlaka ya kweli ilipowazuia wasichana kupata elimu ya sekondari mnamo Septemba 2021,wasichana milioni 1 wamenyimwa haki yao ya kupata elimu. Tangu mamlaka ya kweli ilipowazuia wasichana kupata elimu ya sekondari mnamo Septemba 2021,wasichana milioni 1 wamenyimwa haki yao ya kupata elimu.  (ANSA)

Afghanistan:wasichana milioni 1 wanyimwa haki yao ya kupata elimu tangu 2021

Zaidi ya wasichana milioni 1 wamenyimwa haki yao ya kupata elimu tangu kupiga marufuku ya shule za Sekondari ya 2021 ilipowekwa nchini Afghanstan.Ni katika Ripoti mpya ya UNICEF yenye kichwa:"Gharama ya kutochukua Hatua kwa Elimu ya Wasichana na Ushiriki wa Nguvu Kazi ya Wanawake nchini Afghanistan.”Kuwanyima wasichana wa Afghanistan fursa ya kupata elimu ya sekondari ni kuinyima taifa zima uwezo wake."Alisema hayo Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kulingana na uchambuzi mpya wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kusaidia Watoto Ulimwenguni, UNICEF, unabainisha kwamba, Afghanistan ina hatari ya kupoteza hadi kufikia walimu 20,000 wa kike na wafanyakazi wa afya 5,400 ifikapo mwaka 2030 kutokana na vikwazo vinavyoendelea dhidi ya elimu ya wasichana na ajira kwa wanawake. Katika Ripoti hiyo iliyotolewa tarehe 28 Aprili 2026 yenye kichwa :"Gharama ya kutochukua Hatua kwa Elimu ya Wasichana na Ushiriki wa Nguvu Kazi ya Wanawake nchini Afghanistan,”iligundua kuwa,  uwakilishi wa wanawake katika utawala wa umma ulipungua kutoka 21% hadi 17.7% kati ya 2023 na 2025. Ripoti hiyo inaonya kwamba,  kupungua kwa idadi ya wataalamu wa kike waliohitimu katika shule na hospitali kutakuwa na matokeo mabaya katika kujifunza kwa watoto, matokeo ya afya, na fursa za baadaye. Vikwazo vya elimu na ajira kwa wasichana na wanawake tayari vinaigharimu nchi dola milioni 84 kila mwaka katika pato la kiuchumi lililopotea, huku hasara zikiongezeka baada ya muda huku wanawake wakiendelea kuzuiwa kupata elimu na ajira.

Kutengwa kwa wanawake kutoka katika huduma ya afya

Ripoti hiyo inaonya kwamba kutengwa kwa wanawake kutoka kwa ualimu na huduma ya afya, sekta mbili ambazo wanaruhusiwa kufanya kazi na pale wanapohitajika, kunawadhuru watoto moja kwa moja, kwani kutasababisha kupungua kwa idadi ya wasichana shuleni na kupungua kwa huduma kwa wanawake na watoto. Athari hiyo ni kubwa zaidi katika sekta ya afya, ambapo muktadha wa kijamii mara nyingi huwazuia wanawake kupokea huduma ya matibabu kutoka kwa wanaume, ikimaanisha kwamba kupungua kwa idadi ya wafanyakazi wa afya wanawake kutapunguza moja kwa moja huduma za afya za mama, watoto wachanga, na watoto. Kwa mujibu wa Catherine Russell, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF alisema: "Afghanistan haiwezi kumudu kupoteza walimu, manesi, madaktari, wakunga, na wafanyakazi wa kijamii wa siku zijazo wanaounga mkono huduma muhimu. Hii itakuwa ukweli ikiwa wasichana wataendelea kutengwa na elimu."  Mkurugenzi huyo aidha alisema kwamba: "Tunawasihi mamlaka za kweli kuondoa marufuku ya elimu ya sekondari kwa wasichana na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuendelea kujitolea kuunga mkono haki ya wasichana ya kupata elimu."

Kupoteza wataalamu wenye ujuzi na kuzuia kizazi kijacho kuchukua nafasi yao

Afghanistan inakabiliwa na mgogoro wa pande mbili: inapoteza wataalamu wenye ujuzi, huku ikizuia kizazi kijacho kuchukua nafasi yao. Kadri wanawake wenye uzoefu wanavyostaafu au kuondoka, wasichana wanazuiwa kuendelea na masomo yao na kuchukua majukumu haya. Kila mwaka wa kuchelewa hugharimu Afghanistan kizazi kingine cha wataalamu wenye ujuzi. Tangu mamlaka ya kweli ilipowazuia wasichana kupata elimu ya sekondari mnamo Septemba 2021, wasichana milioni moja wamenyimwa haki yao ya kupata elimu, katika nchi ambayo tayari ina moja ya viwango vya chini zaidi vya wanawake kusoma na kuandika duniani.

Zaidi ya wasichana milioni 2 watanyimwa kupata elimu ya msingi kufikia 2030

Uchambuzi unaonesha kwamba ikiwa marufuku hiyo itaendelea hadi 2030, zaidi ya wasichana milioni mbili watakuwa wamenyimwa haki yao ya kupata elimu zaidi ya shule ya msingi. Shule tayari zinateseka, huku idadi ya walimu wa kike katika elimu ya msingi ikipungua kwa zaidi ya asilimia 9—kutoka karibu 73,000 mwaka 2022 hadi takriban 66,000 mwaka 2024.

Juhudi za UNICEF katika kukabiliana na changamoto hizi

Licha ya vikwazo hivyo, UNICEF inaendelea kusaidia elimu ya watoto nchini Afghanistan. Mnamo 2025, zaidi ya watoto milioni 3.7 wa shule za umma walipokea msaada wa dharura; watoto 442,000 - 66% yao ni wasichana - wamefaidika na mipango ya kujifunza inayotegemea jamii, na shule 232 zimejengwa au kufanyiwa ukarabati. Huku kizazi kingine cha wasichana kikipoteza fursa ya kujifunza, UNICEF inatoa wito wa hatua za haraka ili kurejesha haki ya wasichana ya elimu ya sekondari na ya juu na kuunga mkono uwekezaji katika elimu ya msingi kama njia muhimu ya maendeleo ya rasilimali watu na kama ushahidi wa athari chanya ambayo ujifunzaji jumuishi unazo kwa wasichana. Kwa pamoja, hatua hizi ni muhimu kwa mustakabali wa afya, elimu, na uchumi wa Afghanistan.

Russell:kuwanyima wasichana fursa ya Elimu ni kuinyima taifa zima uwezo wake

"Kuwanyima wasichana wa Afghanistan fursa ya kupata elimu ya sekondari ni kuinyima taifa zima uwezo wake: itawahukumu wasichana, familia zao, na jamii zao umaskini, kuathiri matokeo ya kiafya, na kukandamiza injini ya kiuchumi ambayo kizazi cha wanawake walioelimika kinaweza kuichochea,"Russell alihitimisha.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here

28 Aprili 2026, 11:58