Kenya,Mafuriko yaacha uharibifu na idadi ya vifo ikiongezeka
Na Sr. Christine Masivo, CPS - Vatican.
Mvua kubwa imesababisha uharibifu mkubwa, na watu 45 kufariki nchini Kenya. Ni taarifa iliyotolewa na idara ya Polisi na maafisa wa Serikali nchini humo. Maafa hayo yameathiri hasa mji mkuu wa Nairobi, ambapo mvua kubwa ilibadilisha barabara kuu kuwa mito inayopita kwa kasi, ikifagia magari na kufurika maji majumbani.
Uharibifu, vifo na kuhama makazi
Mamlaka iliripoti kwamba watu 23 walifariki jijini Nairobi Jumamosi tarahe 7 Machi 2026 pekee, huku idadi ya vifo vya kitaifa vikiendelea kuongezeka na timu za uokoaji zikitafuta vitongoji vilivyofurika na kuondoa miili iliyopatikana. Msemaji wa Polisi Michael Muchiri alithibitisha kwamba visa 45 vya kuzama maji vilirekodiwa, huku watu 2,224 wakihama makazi yao kote nchini, na ripoti za ndani zinaonesha kwamba idadi ya watu waliolazimika kutoka majumbani mwao inaweza kuwa kubwa zaidi. Serikali inakadiria kwamba zaidi ya watu 50,000 wameachwa bila makazi, huku maelfu ya familia zikihama makazi ndani na karibu na Jiji la Nairobi.
Hali hiyo imeelezewa kama 'janga' na Shirika la Msalaba Mwekundu, Kenya, likibainisha kuwa mafuriko hayo yameharibu nyumba, mashamba, na miundombinu muhimu katika kaunti kadhaa. "Kingo za Mto Nairobi zilianguka huku mvua ikiendelea," alisema Fredrick Wasonga, muuzaji wa barabarani jijini. "Magari yalisombwa na maji, na maji yaliingia madukani, na kuharibu mali. Mkazi mwingine, Derrick Juma, ambaye anaendesha duka katika eneo hilo hilo, alisema majirani zake wawili walifariki wakati wa mafuriko, akiwemo mmoja aliyeunguzwa na umeme."
Usafiri kuvurugika
Mvua kubwa ilivuruga usafiri sana, na kusababisha uharibifu wa barabara na zaidi hata barabara kuu zilizofurika. Usafiri wa anga pia uliathiriwa. Kampuni ya Ndege ya Kenya, iliripoti kwamba hali mbaya ya hewa iliilazimisha kusimamisha safari za ndege kwenda Nairobi, huku zingine zikielekezwa katika mji wa pwani wa Mombasa. Maafisa wa serikali wanasema timu za dharura zinafanya kazi ya kurejesha njia za usafiri na kusaidia jamii zilizoathiriwa. Wakazi walielekeza hasira zao kwa Johnson Sakaja, Gavana wa Nairobi, ambaye hapo awali aliahidi kuboresha mfumo wa mifereji ya maji na miundombinu ya barabara baada ya kuanza huduma yake mwaka 2022. Wakosoaji wanasisitiza kwamba mifereji mibaya ya maji mijini na maendeleo yasiyodhibitiwa yamezidisha athari za mafuriko.
Watabiri wa hali ya hewa wa Afrika Mashariki
Wanasayansi wanaonya kwamba matukio mabaya ya hali ya hewa ni ya mara kwa mara zaidi Afrika Mashariki. Tafiti nyingi zimeonesha ongezeko la ukame mkali na mvua kubwa katika eneo hilo katika miongo miwili iliyopita. Wataalamu wanasema kwamba mabadiliko ya hali ya hewa, pamoja na ukuaji wa miji haraka na miundombinu dhaifu ya mifereji ya maji, yanaongeza hatari ya miji kama vile Nairobi kupata majanga ya mafuriko.
Juhudi za uokoaji
Timu za uokoaji na mashirika ya kibinadamu yanaendelea kutafuta watu waliopotea na kutoa msaada kwa familia zilizohamishwa. Mamlaka inafuatilia mvua katika kaunti kadhaa, kwa kuofia kwamba dhoruba zinazoendelea zinaweza kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi zaidi. Kenya inapokabiliana na matokeo ya janga hilo, lengo linabaki kwenye misaada ya dharura na juhudi za kujenga upya kwa makumi ya maelfu ya watu ambao wamepoteza makazi yao.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.